Hii hapa miradi kutoka ‘Hapa kazi tu’ hadi ‘kazi iendelee’

Dar es Salaam. Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege (ATCL), ukamilishaji wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) na daraja la JP Magufuli ni miradi iliyoibeba uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan  ndani ya miaka minne ya uongozi wake.

Utawala wa Magufuli ulitumia falsafa ya ‘Hapa kazi tu’, Samia aliposhika usukani akaibadili kidogo na kuwa ‘Kazi iendelee’

Rais Samia anatimiza miaka minne ya uongozi wake mwezi huu tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 ambapo hadi sasa tayari ameweka alama isiyofutika kwenye miradi ya kimkakati ambayo ilianza wakati wa utawala wa hayati Dk John Magufuli.

 Kifo cha Rais Magufuli kilileta mshtuko na kuibua maswali juu ya miradi ya kimkakati aliyoianzisha, Rais Samia punde tu baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo wa mtangulizi wake aliwaondoa hofu watanzania akisema ‘Kazi Iendelee’ akimaanisha kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.

Kwa mradi wa SGR Rais Samia akihutubia Bunge la Tanzania Aprili 22, 2021 alisema Serikali  itakamilisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora na kuanza ujenzi wa vipande vingine, ikiwemo cha Mwanza – Isaka na kuendelea na loti ya tatu (Makutupora -Tabora) na loti ya nne (Tabora – Isaka) na kisha kumalizia Kaliua- Kigoma na Kaliua – Mpanda.

Kabla ya kuanza majukumu ndani ya awamu yake, Rais Samia wakati akiingia madarakani aliikuta Loti 1 (Dar es Salaam – Morogoro) ikiwa imejengwa kwa asilimia 75 na Loti 2 (Morogoro – Makutupora), ikiwa na asilimia 50, kama alivyoliahidi bunge, alikamilisha vipande hivyo.

Mwaka 2024,   vipande viwili vya SGR vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora vyenye urefu wa kilometa 722 vinakamilika na kuanza kutoa huduma za usafirishaji wa abiria.

Hatua hiyo ilikoleza Agosti 2024 kuanza safari kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma baada ya kuzinduliwa na Rais Samia mwenyewe.

Hadi sasa katika mradi wa reli, kinachosubiriwa ni kuanza usafirishaji huduma ya usafirishaji mizigo baada ya kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo yaliyowasili nchini Desemba 2024.

Kwa upande wa uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuliimarisha hilo kwa kununua ndege mpya.

Awamu ya tano chini ya Rais Dk Magufuli kulikuwa na ndege nane zilizonunuliwa chini ya utawala wake Rais Samia zikaongezwa  ndege zingine saba chini ya awamu yake.

Kwa mujibu wa ATCL ufanisi wa shirika hilo umeongezeka maradufu katika utoaji wa huduma ambapo kwa sasa mteja anaweza kupata huduma za kusafirisha mizigo mikubwa (Cargo) hadi tani 54 kwa mara moja tena kwa bidhaa yoyote ikiwemo zile zenye uzito mkubwa kama magari, upana mkubwa kubwa na zenye kuhitaji joto maalumu.

Eneo lingine ni mradi wa kufua umeme wa bwawa umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) ambapo hayati Magufuli alifariki dunia katika kipindi ambacho utekelezaji wa mradi wa JNHPP umefikia asilimia 33.

Januari 31, 2025 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati akichangia kwenye azimio la Bunge la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyeji wa mkutano wa nishati Afrika (Mission 300) kwa mwaka 2025 alieleza kuwa,

Mitambo minane kati ya tisa inayojengwa katika Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, imekamilika.

Mradi mwingine ni daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi) ambao wakati Magufuli anafariki, utekelezaji wa daraja hilo ulikuwa ni asilimia 16,

Januari 2025 Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega akiwa mkoani Mwanza amesema Daraja la JP MAGUFULI (Kigongo-Busisi) lilifikia asilimia 96.3.

Ulega amesema utekelezaji wa mradi huo wenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66, ulioanza Februari 25, 2020 chini ya Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation.

Siri ya miradi kutekelezwa

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi Dk Paul Loisulie amesema siri ya Rais Samia kutekeleza kwa ufanisi miradi hiyo ni kutokana na yeye kuwa makamu wa Rais na alikuwa msaidizi wa hayati Magufuli.

“Hakuwa mgeni kwenye Serikali uzoefu alioupata akiwa makamu wa Rais umemsaidia sana, Rais Samia ni kiongozi anayependa mwendelezo alijua akitaka usalama lazima aendeleze miradi iliyoachwa na angeacha asingeleweka,” amesema.

Dk Loisulie amesema miradi yote ya kimkakati ilishachukua fedha nyingi hivyo isingekuwa busara kuitekeleza miradi hiyo.

Naye Dk Mwinuka Lutengano amesema wakati wa utawala wa Rais Samia tayari mpango wa maendeleo wa miaka mitambo umeshaanza kutekelezwa na miradi ile ilishawekwa kuwa ya kitaifa.

“Pia Rais Samia amejipambanua kwenye suala la uwekezaji na kushirikiana na sekta binafsi, tulikuwa na ilani ya uchaguzi ambayo ilimulika miradi husika kwa hiyo ilikuwa njia nzuri kwake kuendeleza miradi hiyo,” amesema.

Kwa upande wake Mchambuzi wa Uchumi Oscar Mkude amesema siri ya utekelezaji wa miradi yote chini ya awamu ya sita ni miradi husika kuwa na nembo ya kitaifa.

Akitolea mfano Bwawa la Nyerere amesema ilikuwa ni ngumu kuachwa kutekelezwa kwani Tanzania ilikuwa na uhaba wa nishati hiyo na mradi huo ndio ulionekana mkombozi kutatua changamoto.

Kwa mradi wa daraja la JP Magufuli mkoani Mwanza, Mkude amesema linasaidia usafirishaji wa mizigo na kuunganisha wananchi wa pande mbili hivyo ni lazima ungetekelezwa.

“Miradi yote tayari fedha zimeshawekwa ni ngumu kukubali kutelekeza kwa sababu ni hasara, SGR mikataba tayari imeshasainiwa, kwa hiyo Rais Samia ameonyesha uongozi imara ni kama dereva ambaye tairi la gari lake limepasuka halafu akashika usukani kwa umakini na gari halikuyumba,” amesema.

Mkude amesema Rais Samia anastahili pongezi kwa kuwa amechukua madaraka katika chama ambacho tayari kilikuwa na mfumo dume na hakuwa akiaminika kushika wadhifa huo lakini alishika mamlaka na kutekeleza miradi mikubwa bila kutetereka.

Amesema Rais Samia kutokana na ushupavu wake sasa anaendelea kutekeleza miradi mingine na kama atashinda awamu nyingine atakuja kuanzisha miradi mingine mpya chini ya utawala wake na miradi hiyo itakuwa alama kamili ya utawala wake.

Related Posts