BAADA ya tetesi nyingi juu ya kuajiriwa na Mashujaa kwa aliyekuwa kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga ili kuchukua mikoba ya Mohammed Abdallah ‘Bares’ sasa ni rasmi uongozi wa timu hiyo umemalizana naye.
Mayanga alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakifukuziwa na uongozi wa Mashujaa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Bares na sasa ni rasmi atakuwa kocha mkuu wa kikosi hicho.
Chanzo cha kuaminika kutoka Mashujaa kimeithibitishia Mwanaspoti kuwa tayari wamemalizana na kocha huyo na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa.
Mayanga kwa sasa anakinoa kikosi cha Mbeya Cit na, hivi karibuni alikiongoza kuitoa Azam kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya kutoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Taarifa kutoka ndani ya Mashujaa zinaeleza kuwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu baina ya viongozi na kocha huyo, hatimaye yamekwenda vizuri na muda wowote jambo hilo litawekwa wazi.
“Mazungumzo yamekwenda vizuri Mayanga amepitishwa na viongozi kama chaguo linalofaa kuchukua nafasi ya Bares,” kimesema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Kwa upande wake, Mayanga amesisitiza kuwa hajafanya mazungumzo na timu yoyote na kwa sasa anabaki na Mbeya City ambayo malengo yake ni kuhakikisha anaipandisha Ligi Kuu Bara.