Kocha amchomoa Nouma Simba | Mwanaspoti

KUNA mambo mawili ameambiwa beki wa kushoto wa Simba, Valentine Nouma na kocha wake ayafanyie kazi, huku kubwa zaidi akitakiwa kuchukua uamuzi wa kuondoka kikosini hapo.

Nouma huu ni msimu wa kwanza anaitumikia Simba aliyojiunga nayo akitokea FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo ambapo jambo la pili aliloambiwa ni kupambana kuongeza muda wa kucheza.

Beki huyo wa kushoto ambaye ametoswa kwenye kikosi cha Burkina Faso kinachojiandaa kucheza mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Djibouti na Guinea-Bissau, ameambiwa na kocha wake wa timu ya taifa, Brama Traore, bado ana nafasi ya kumuita lakini anatakiwa kutafuta timu ambayo atakuwa anacheza kwa muda mwingi tofauti na sasa.

Kauli hiyo ni ishara ya kwamba Kocha Traore amemtaka Nouma kufikiria kuondoka Simba kwani amekuwa hapati nafasi kubwa ya kucheza mbele ya nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Traore alisema, Nouma ni beki muhimu kwenye Taifa lao, lakini anaonekana kupata wakati mgumu kujumuishwa kikosini mara kwa mara kutokana na nafasi yake ndogo anayopata klabuni kwake.

“Sio rahisi kwa beki mzuri kama Nouma kutopata nafasi ya kucheza ila mara nyingi uwezo wa mchezaji ndio unaochangia kuwepo kikosi cha timu ya Taifa.

“Huwezi kumchukua mchezaji ambaye hapati nafasi ya kucheza, kwa sababu kama hachezi utatambuaje kiwango chake cha sasa, ndio maana namshauri Nouma akatafute changamoto mpya kama alipo hapati muda mwingi wa kucheza.

“Nouma bado ni beki ambaye kwenye kikosi changu ninamuhitaji, ila ni lazima aishinde changamoto ya kukosa namba ili asipoteze kiwango chake kwa kukaa benchi,” alisema kocha huyo na kuongeza.

Tangu atue Simba, Nouma ameitwa katika timu ya Taifa lake, mara mbili tu, huku safari hii akiachwa na kocha wake akitoa sababu hizo.

Kwa sasa Burkina Faso inajiandaa na michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambapo Ijumaa Machi 21 itaikaribisha Djibouti, kisha Machi 24 ikicheza ugenini dhidi ya Guinea-Bissau.

Related Posts