Sura mbili za utawala wa miaka minne wa Rais Samia

Dar es Salaam. Ilianza siku moja, ukakatika mwezi, mwaka, hatimaye leo ni miaka minne, tangu Samia Suluhu Hassan aapishwe kuwa Rais wa Tanzania.

Kwa mujibu wa wanazuoni mbalimbali, tathmini ya safari ya uongozi wake inabebwa na milima na mabonde, wakirejea mambo yaliyofanyika na ama kurejesha au kupoteza matumaini ya wananchi.

Wasomi hao wabobevu katika taaluma ya utawala na sayansi ya siasa, wanasema mwanzo wa utendaji wa mkuu huyo wa nchi, ulileta matumaini katika mambo mengi.

Hata hivyo, hali hiyo haikudumu kulingana na wasomi hao, kadiri siku zilivyokwenda changamoto ziliibuka na hatimaye baadhi ya mambo kuonekana kusuasua.

Ingawa hali iko hivyo katika utawala bora na siasa, kwa upande wa uchumi, mambo yanatajwa kuwa shwari kwa mujibu wa Aurelia Kamuzora, profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Rais Samia aliapishwa kushika wadhifa huo, Machi 19, 2021 siku mbili baada ya kifo cha mtangulizi wake, hayati John Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo.

Miaka minne ya uongozi wa Rais Samia inatazamwa na Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, kama kipindi cha kurejea kwa kiasi kikubwa kwa matumaini ya wananchi na nyakati zingine kuwepo na changamoto.

Kwa upande wa kurejea kwa matumaini, Dk Masabo anasema ndani ya awamu ya sita wananchi walirejeshewa uhuru wa kujieleza na hata kuimarika kwa utawala wa sheria.

Katika kipindi hicho, anasema kulishuhudiwa Rais Samia akiunda kikosi kazi kukusanya maoni ya wadau kuhusu uendeshaji wa siasa nchini, kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala.

Ni kipindi hichohicho pia, mkuu huyo wa nchi, aliunda tume ya haki jinai iliyolenga kushauri mageuzi ya mifumo katika taasisi za haki jinai.

Kadhalika, Rais Samia alitambulisha falsafa yake ya R4 ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya ukiwa ndio msingi wa utendaji wake.

Kwa mujibu wa Dk Masabo, mambo hayo yote yalirejesha matumaini ya wananchi kuhusu kurejea kwa utawala wa sheria na uhuru wa maoni.

“Hili unalitathmini kwa kuangalia uhuru wa kisiasa, ni kweli taasisi za kisiasa na kiraia zilirejeshewa uhuru wake wa kufanya shughuli zake,” anasema.

Hata katika maendeleo, anasema kulikuwa na matumaini chanya kwa kuwa miradi iliyokuwepo iliendelezwa na mingine mipya ilibuniwa na kutekelezwa.

Lakini yapo baadhi ya matumaini kwa mujibu wa Dk Masabo, yalitoweka hasa baada ya taasisi za kisiasa na kiraia zilipoendelea kufanya shughuli zake kwa kuuhoji utawala, ndipo misukosuko ilianza. Anasema baadhi ya matukio ya kisiasa yalizuiwa, ukiwemo mkutano wa Siku ya Vijana Duniani ulioandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoani Mbeya.

Mwanazuoni huyo anasema pamoja na mafanikio katika uendelezaji wa miradi, lakini kwa upande mwingine utawala wake ni kipindi ambacho nchi imekopa zaidi ukilinganisha na vipindi vingine.

“Maendeleo ya vitu yameonekana, lakini tumetengeneza utegemezi mkubwa, ukiangalia uwiano wa maendeleo na madeni tuliyonayo, wakati fulani ni vigumu kulizungumza hilo suala.

“Tumepunguza utegemezi wa ndani na tumeongeza utegemezi wa nje,” anasema.

Dk Masabo anasema ndani ya kipindi hicho, mamlaka ya wananchi kuamua kiongozi wanayemtaka ilipungua na hilo limeonekana katika uchaguzi wa serikali za mitaa kutokana na malalamiko.

“Wananchi hawakuwa na uhuru wa kuchagua nani awe kiongozi, ilikatisha tamaa na kuturudisha mwaka 2019,” anasema.

Katika kipindi hicho, anasema kulikuwa na mwendelezo wa matukio ya mauaji yenye mazingira ya kutatanisha.

Anasema katika miaka minne hiyo, wadau walidhani kwa kuwa Rais alikuwa sehemu ya Bunge la Katiba angekwamua mchakato huo, lakini matumaini ya kupatikana Katiba mpya bado ni sintofahamu.

“Watu walitarajia mwenyekiti mwenza wa Bunge Maalumu la Katiba angelipa msukumo suala hilo,” anasema.

Katika kipindi hicho, anasema kumekuwa na sheria zisizotekelezwa, ikiwemo Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo licha ya kusainiwa na Rais, haijaanza kutumika ipasavyo.

Mabadiliko, maendeleo, changamoto

Kwa mtazamo wa mwanazuoni mwingine wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe, kipindi hicho kimegawanyika katika mabadiliko, maendeleo na changamoto, hasa kwenye siasa.

Anasema baada ya Rais Samia kuapishwa alichukua hatua kadhaa za kubadili taswira ya kisiasa iliyokuwepo, hasa kwenye muktadha wa demokrasia na utawala bora.

Ni kipindi hicho, anasema baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa kwa sababu mbalimbali vilifunguliwa na kuwekwa msisitizo katika umuhimu wa uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari.

Kwa upande wa mikutano ya kisiasa iliyokuwa imepigwa marufuku kwa miaka kadhaa, anasema ilifunguliwa, hatua iliyosaidia kuimarisha shughuli za kisiasa na demokrasia nchini.

“Mashirikiano na vyama vya upinzani mimi huwa napenda kuviita vyama mbadala. Rais Samia amekutana mara kadhaa na vyama mbadala, akisisitiza mshikamano na kufanya siasa za hoja na zenye ustaarabu,” anasema.

Lakini, anasema katika kipindi hicho kumekuwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa kisiasa.

“Kwa mfano, mauaji ya mwanachama mwandamizi wa Chadema, Ally Kibao, yaliibua wasiwasi kuhusu mazingira ya kisiasa,” anaeleza.

Anaeleza pia, kumekuwa na taarifa ya kuendelea kwa vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wapinzani, licha ya ahadi za mageuzi.

“Kwa ujumla, uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta mabadiliko muhimu katika kuimarisha demokrasia na uhuru wa kisiasa nchini, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha haki za binadamu na utawala bora vinaimarishwa zaidi,” anasema.

Kiuchumi, Profesa Kamuzora anasema katika miaka minne hiyo, ndicho kipindi ambacho Tanzania imeweka mazingira rahisi kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote.

Kwa mujibu wa Profesa Kamuzora, uchumi unaendeshwa na sekta ya biashara na nyumbani, inapotokea mazingira ya biashara yameboreshwa ni kichocheo cha uchumi.

“Naona kwa sasa watu wamechangamkia mikopo, vijana wanachangamkia uanzishaji biashara, watu wazima wanafanya biashara na wawekezaji wanakuja, yote haya yanatokea kwa sababu wanavutiwa,” anasema.

Inapotokea wawekezaji na wafanyabiashara wanavutiwa, anasema maana yake Serikali imetekeleza vema wajibu wake wa kusimamia mazingira ya biashara.

Sambamba na hayo, anasema uchumi pia umekua ndani ya kipindi hicho na vipimo vya ukuaji ni ongezeko la pato la Taifa, kadhalika kushuhudia kwa macho shughuli nyingi zinazoendelea nchini.

“Ukiona kuna msongamano wa magari yanayosafirisha mizigo, hicho ni kipimo cha ukuaji uchumi, ukiona watu wanafanya biashara, hiyo ni dalili ya kukua kwa uchumi. Kwa kipindi hiki naona mambo hayo yameongezeka,” anasema.

Kwa ujumla, anasema Serikali inaonekana kufanya kazi yake ya kusimamia sera na sheria zinazochochea shughuli za uchumi, ndiyo maana yanashuhudiwa matokeo mazuri.

“Hatujawahi kupata Rais ambaye anasimamia vyema uchumi katika kipindi cha miaka minne kama huyu tuliye naye sasa,” anasema.

Related Posts