Kocha ASEC Mimosas amaliza utata wa Aziz KI, Ahoua

KOCHA wa Asec Mimosas, Julie Chevalier, amewachambua viungo washambuliaji Jean Charles Ahoua na Stephane Aziz KI waliowahi kucheza Ligi Kuu ya Ivory Coast kabla ya sasa kukiwasha Ligi Kuu Bara.

Mastaa hao wanaokipiga kwenye klabu mbili kubwa Ligi Kuu Bara, Ahoua anaichezea Simba na Aziz KI Yanga, wote ni tegemeo katika vikosi vyao.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Julie alisema Aziz KI ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na amefanya mengi kwenye ligi zote mbili, Ivory Coast na Tanzania.

Kocha huyo raia wa Ufaransa, amesema ukiwaweka wachezaji hao kwenye mzani sawa wa ushindani, Aziz Ki anakuwa juu ya Ahoua kutokana na walichokifanya Ivory Coast na sasa Tanzania.

“Kama Ahoua amefanya vizuri Tanzania wakati huu ni sahihi kwa sababu ameonyesha njaa ya mafanikio katika msimu wake wa kwanza, lakini bado haiwezi kufifisha ubora wa Aziz Ki.

“Utofauti wao ni kwamba Aziz KI ni mchezaji anayeweza kufanya kitu kwenye mechi kubwa na hata ndogo, sikufanya kazi na Ahoua lakini najua makali yake ni kiungo ambaye kama atakuja kuchangamka zaidi anaweza kuja kuwa hatari huko mbele lakini kwa sasa bado,” alifichua kocha huyo.

Huu ni msimu wa tatu Aziz Ki raia wa Burkina Faso akiwa anaitumikia Yanga aliyojiunga nayo Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambapo wakati anatua Yanga alikuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.

Katika misimu yake mitatu ndani ya Ligi Kuu Bara, amekuwa mfungaji bora msimu uliopita 2023-2024 akifunga mabao 21 na asisti nane huku pia akibeba Tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu Bara. Kabla ya hapo, msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara 2022-2023, alifunga mabao tisa huku hadi sasa akiwa nayo saba. Jumla ndani ya misimu mitatu ana mabao 37.

Kwa upande wa mataji, Aziz Ki ameshinda mawili ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023 na 2023-2024 na mawili Ngao ya Jamii 2022 na 2024, huku msimu wa 2022-2023 akicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger na Yanga kupoteza kwa sheria ya bao la ugenini.

Kwa upande wa Ahoua raia wa Ivoro Coast ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kuitumikia Simba akiwa amejiunga nayo akitokea Stella Club d’Adjamé ya Ivory Coast, ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akifunga 12 na asisti 6.

Msimu uliopita Ahoua akiwa Stella Club d’Adjamé, alitangazwa kuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast huku akiondoka na rekodi ya kufunga mabao 12 na asisti 9.

Related Posts