Mabadiliko ya kiuchumi miaka minne ya Rais Samia

Dar es Salaam. Ukuaji wa pato la Taifa Tanzania unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 6 mwaka huu kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022, huku uwezeshaji wa biashara, utengenezaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji, na ukusanyaji kodi vikitajwa kuwa sababu.

Ukuaji huu unaendelea kushuhudiwa wakati ambapo idadi ya miradi mipya ya uwekezaji inayokuja Tanzania ikiongezeka maradufu, jambo linaloongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

Ukuaji huu ndani ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani unashuhudiwa ikiwa ni baada ya kufanyika kwa mabadiliko mbalimbali ya kiutendaji na mapitio ya sheria za kodi, kanuni mbalimbali, na urejeshaji wa diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na nchi mbalimbali.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021, wakati Rais Samia anaapishwa kushika madaraka hayo, ukuaji wa pato la Taifa ulikuwa kwa asilimia 4.9, lakini ulipungua hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2022. Baadaye, pato hilo la Taifa lilianza kukua hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2023, asilimia 5.4 mwaka 2024, na sasa Benki Kuu inatarajia ukuaji wa asilimia 6 mwaka 2025 kwa upande wa Tanzania Bara na asilimia 6.8 kwa upande wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ukuaji kwa mwaka huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.

Katika hatua nyingine, Tutuba anasema thamani ya shilingi ya Tanzania inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na kuwepo kwa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024, utekelezaji wa sera ya fedha, na uamuzi wa kubakiza riba ya Benki Kuu kuwa asilimia 6.

Samia aliapishwa kushika nafasi hiyo Machi 19, 2021, baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli, kufariki dunia Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, Severini Mushi, alisema kuwepo kwa wepesi wa kufanya biashara na urafiki ni moja ya mambo ambayo yamechochea ukuaji huu katika uongozi wa awamu ya sita.

“Tofauti na zamani ambapo wafanyabiashara walikuwa wanaonekana ni wezi na walikuwa wanapewa kesi za uhujumu uchumi, lakini sasa mambo yamebadilika. Watu wanafanya biashara kwa uhuru, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amekuwa rafiki, anatusikiliza na kutatua changamoto zetu,” anasema Mushi.

Pamoja na kilichofanyika, Mushi bado anasema ipo nafasi ya kuongeza zaidi ukuaji wa uchumi kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ili kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

“Tunatamani kuona ukokotoaji wa kodi katika mizigo ya bandari unakuwa rahisi na rafiki ili kuvutia watu wengi zaidi kufanya biashara nasi, hasa wale wanaotoka nje. Namna kodi zinapokuwa rafiki, bidhaa zinapatikana kwa wingi na kuwafanya watu kuwa na uwezo wa kuzimudu,” anasema Mushi.

Ili kuweka urahisi wa ukusanyaji wa kodi, Januari 20 mwaka huu, TRA ilizindua tovuti mpya na mfumo wa TANCIS ulioboreshwa, utakaosaidia kurahisisha uondoshaji wa shehena bandarini, katika viwanja vya ndege, pamoja na mipakani.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, anasema mfumo wa TANCIS utaleta usawa katika ulipaji wa kodi, ambapo kila mmoja atajua anapaswa kulipa kiasi gani kwa kutumia mfumo, jambo litakaloongeza ukusanyaji wa kodi.

Kilichofanyika ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia, ambaye aliwahi kusema kuwa Serikali inakusudia kufanya mageuzi ya kiutendaji kwenye mfumo wa utozaji na ukusanyaji wa kodi, kuweka mfumo utakaorahisisha na kuvutia walipa kodi, na kutengeneza wigo mpana zaidi wa walipa kodi ikilinganishwa na walipakodi waliopo sasa.

“Hivyo, kuna kila haja ya kutanua wigo wa walipa kodi, na vilevile, kuweka mifumo rafiki ya ulipaji na ukusanyaji wa kodi. Ningependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji, na wananchi wanalipa kodi bila shuruti na matumizi ya nguvu, wakitambua kwamba kodi ni maendeleo yao,” alisema Rais Samia, na kauli hiyo ilifurahiwa na jumuiya ya wafanyabiashara.

Katika sekta ya viwanda, ambayo ndani yake inajumuisha uzalishaji wa bidhaa, alipokuwa akizungumzia miaka minne ya utendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, jumla ya miradi ya viwanda 951 imesajiliwa.

Miradi hiyo inatarajiwa kuleta ajira 124,339 na kuwekeza mitaji ya Dola bilioni 10.5 za Marekani (sawa na takribani Sh27 trilioni).

Katika miradi hiyo, viwanda vinachukua asilimia 45 ya miradi ya sekta zote iliyosajiliwa kati ya mwaka 2021 hadi 2025.

Kwa upande wa mitaji, miradi ya viwanda imechukua asilimia 42 ya mitaji ya sekta zote iliyosajiliwa katika kipindi hicho, na kufanya miradi ya viwanda kuwa sekta inayoongoza kwa idadi ya miradi, mitaji, na ajira,” anasema Msigwa.

Mchanganuo unaonyesha kuwa jumla ya miradi 951 ya viwandani imesajiliwa, ambapo 917 ni mipya, na 36 inahusu upanuzi wa viwanda. Kati ya miradi hiyo, 244 inamilikiwa na Watanzania, 501 ni ya wageni, na 206 ni miradi ya ubia.

Hilo linaenda sambamba na ajira za viwandani 124,339, huku mtaji uliowekwa ukiwa na thamani ya zaidi ya Sh67 trilioni.

Mbali na uwekezaji uliofanywa kwa miaka minne, kwa upande wa Januari hadi Februari mwaka huu, sekta ya viwanda imetengeneza miradi 52, ambapo kati ya hiyo, 14 ni ya Watanzania na 33 ni ya wageni.

Related Posts