Miaka minne yenye tafsiri mbili imekatika. Minne tangu kifo cha Rais wa tano, Dk John Magufuli na minne ya urais wa Samia Suluhu Hassan. Machi 17, 2021, taifa lilitangaziwa kifo cha Dk Magufuli, Rais wa Tanzania wa kwanza kukutwa na mauti akiwa ofisini.
Machi 19, 2021, Samia alikula kiapo kuongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais wa Tanzania wa kwanza kuingia madarakani bila uchaguzi, kwa kufuata mwongozo wa Katiba, ibara ya 37 (5). Hapo kabla, marais wote waliotangulia, waliapishwa baada ya kutoka kwenye uchaguzi.
Miaka minne yenye tafsiri mbili na inayotoa muktadha tofauti kisiasa. Hali ilivyokuwa wakati Magufuli anavuta pumzi ya mwisho miaka minne iliyopita, na mazingira ya miaka minne baadaye, nchi ikiongozwa na Rais Samia. Kabla, ni makabiliano na mapambano. Baadaye, ni mizunguko ya sanaa za siasa bila mshikemshike.
Matokeo wakati wa Magufuli, upinzani ulikuwa hoi. Vyama havikuruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, walipata vipigo uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020. Kabla ya uchaguzi, wabunge na madiwani wengi walihama kutoka vyama vya upinzani na kujiunga CCM, kwa jina la kuunga mkono juhudi za Magufuli.
Matokeo wakati wa Samia, upinzani hauna sura yenye kueleweka. Vyama vinaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara, lakini uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, haukuwa na tofauti yoyote dhidi ya ule wa mwaka 2019. Malalamiko ya wapinzani wagombea wake kuenguliwa, kuchezewa faulo, kisha CCM kuondoka na ushindi mnono.
Mazingira ya kisiasa ni yaleyale. Tofauti ni moja, Magufuli alitaabika dhidi ya upinzani. Alitumia nguvu kubwa kuwadhibiti. Matokeo yake, kuna viongozi wa kisiasa walikimbilia nje ya nchi; Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje na mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Godbless Lema.
Rais Samia, anaonekana anastarehe kisiasa, maana hafanyi makabiliano, ila wapinzani wanapitia kipindi kigumu. Imebaki takriban miezi saba ufanyike Uchaguzi Mkuu 2025. CCM, wameshapata wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vilevile Zanzibar.
Chadema, hadi sasa hawajaeleweka. Wanasema “No Reforms No Election” – “Bila mabadiliko ya kikatiba hakuna uchaguzi”. Katiba, sheria na mazingira ya kimfumo, hayawapi Chadema mwanya wa kutekeleza azma hiyo ya kuzuia uchaguzi ili kulazimisha mageuzi ya kikatiba.
Watafanikisha mabadiliko ya Katiba lini na kujiandaa na uchaguzi lini? Halafu waanze mchakato wa kupata wagombea, kuanzia urais, ubunge hadi udiwani. Wakati huo, CCM wanajipanga. Hawahitaji tena Mkutano Mkuu, labda waitishe kwa mapenzi yao, kwani wajumbe wa Mkutano Mkuu walishamaliza kazi tangu Januari 19, 2025, walipompitisha Rais Samia kuwa mgombea urais, Dk Emmanuel Nchimbi, mgombea mwenza na Dk Hussein Mwinyi, mgombea urais Zanzibar.
Chadema bado wanaugulia majeraha ya kuvurugana wenyewe. Lissu na Mwenyekiti aliyepita, Freeman Mbowe, wakitambua kuwa wote ni muhimu kwa afya ya chama chao, walichagua kushughulikiana. Lissu alimshinda Mbowe, lakini chama kikabaki vipandevipande. Hivi sasa wanapambana kuunganisha vipande ili kirejee kuwa kimoja tena. Je, uunganishaji huo utakamilika lini?
Wakati CCM, walipokuwa wanafanya mkutano mkuu kumpata Makamu Mwenyekiti, Tanzania Bara, ambaye alichaguliwa Stephen Wasira, vilevile kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, walikuwa kwenye shamrashamra, maana Chadema nyumba ilikuwa inateketea, sababu ni mvutano wa Lissu na Mbowe. CCM kwa sababu walijiona wapo upande wa raha, wakapitisha na wagombea, nje ya agenda, vilevile tofauti na utamaduni wa chama hicho.
Hutakosea ukisema kuwa CCM wanastarehe ndiyo maana wanafanya mambo watakavyo. Ingekuwa wapinzani wapo imara na wanawapa presha, pengine uamuzi wa Januari 19, 2025, Dodoma, usingefanyika. Hii inapalilia hoja kwamba miaka minne ya Samia, imejaa starehe ya kisiasa, wakati Magufuli alitumia nguvu kubwa.
Angalau Zanzibar, ACT-Wazalendo wapo imara na inafahamika mgombea urais wao ni Othman Masoud Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Uchaguzi wa Muungano, tangu kipigo cha uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, vyama vya upinzani havijaamka sawasawa. Matamko ni mengi kuliko kuchukua hatua.
Wakati wa Uchaguzi Chadema, mtangazaji wa Clouds FM, Ally Masoud “Kipanya”, alipata kuziuliza pande mbili zenye kusigana: “Mmerogwa?” Lilikuwa swali la msingi, maana Chadema walifahamu kuwa mpinzani wao (CCM), ana nguvu, kwa hiyo walihitaji mshikamano.
Wao waliamua kujidhoofisha kwanza, ndiyo wamwendee mshindani aliyekamilika. Kama siyo kurogwa ni nini?
Magufuli aliwaona wapinzani ni kikwazo kwake, akasema ndiyo ambao walikuwa wanamchelewesha kuwapa Watanzania maendeleo. Akapambana nao. Rais Samia, yeye haonekani akihangaika na wapinzani, lakini huoni vyama vya upinzani vikinyanyuka na kuonyesha dalili za ushindani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Mahali ambako Magufuli alitumia nguvu, Rais Samia anastarehe. Ukiwa na imani haba, utaweka jibu “ndiyo”, katika swali la Kipanya, kwamba wapinzani wamerogwa. Januari na Februari 2023, vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo, vilinyanyuka kwa kishindo, baada ya mikutano ya hadhara kuruhusiwa.
Usingetarajia mwaka 2025, karibu kabisa na uchaguzi mkuu, kuwe na hali ya kigugumizi kisichoeleweka. Mazingira ya sasa yanajenga taswira kuwa ama wapinzani wameshindwa kupona madhara waliyoachiwa na Magufuli, kuna sanaa kubwa ya kisiasa inachezwa na Rais Samia.