Ripoti maalumu: Dampo la Pugu latajwa kutokidhi viwango -3

Dar es Salaam. Ukisema cha nini, mwenzako anajiuliza atakipata lini? Msemo huu unaelezea hali halisi ya maisha katika Dampo Kuu la Jiji la Dar es Salaam lililopo Pugu Kinyamwezi, kilomita 35 kutoka katikati ya jiji hilo.

Ni sehemu ambayo ukifika mandhari inayokukaribisha ni lundo la takataka mithili ya mlima, huku sauti za magari ya taka yanayoingia na kutoka eneo hilo zikirindima.

Nilipigwa bumbuwazi nilipoona eneo hilo lenye harufu kali, ni sehemu ya kazi ya watu wanaojitafutia riziki.

“Leo nimetoka na redio ya ‘bluetooth’ na hiki kidude cha saluni (ananionyesha dryer),” anasema Emmanuel Karanda, miongoni mwa kijana wanaoshinda dampo kuokota taka na kwenda kuziuza au kupeleka kwa mafundi.

Dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo jijini Dar es Salaam. Picha na Mpigapicha Wetu

Karanda sawa na vijana wengine niliokutana nao dampo hufanya kazi ya kukusanya taka zinazoweza kutumika kwa shughuli nyingine, ikiwamo kurejelezwa.

Wakati nikiendelea kuangalia shughuli za vijana wale, mita chache kabla ya kufika eneo la dampo kuna vibanda lukuki vya mama lishe.

Harufu ni nzito, maji machafu yanatiririka katika mitaro iliyopo karibu na dampo, nzi wamekithiri juu ya meza za vibanda hivyo, lakini bado chakula kinauzwa.

Wateja hapa ni madereva wa magari ya taka, “kuna wakati nzi wanazidi na harufu inakuwa kali sana, wanakuja watu wa manispaa kumwaga dawa katika maeneo haya… pia moshi unaotokana na kuchomwa takataka unatuathiri.

“Hatuna namna, ndiyo kazi tunayoifanya kwa sababu wateja ni hawa madereva wa magari ya taka na hawa vijana wanaoshusha takataka,” anasema Fatuma Ntula, mama lishe katika eneo hili anayezungumza nami wakati nikiendelea kunywa chai aliyoniuzia, ambayo niliinywa kwa shida kutokana na nzi waliokuwapo na harufu kali.

Hamis Malale, mkazi wa Mbagala Charambe anayefanya kazi ya kupakua takataka kutoka kwenye magari anasema amewahi kuugua mara kadhaa kutokana na mazingira ya chakula cha eneo hilo.

Lundo la takataka katika dampo la Pugu jijini Dar es Salaam

“Mazingira ya pale siyo ya kuridhisha, unaweza kukuta mama ntilie anapika na nzi wamejaa mezani, lakini bado tunakwenda kula. Nadhani kuna haja ya Serikali kutoa elimu kuhusu haya yanayoendelea.

“Nimewahi kuumwa tumbo mara nyingi tu, lakini sina jinsi kwa sababu ni sehemu ya kazi na familia yangu inanitegemea, mazingira haya yanatukwaza ndiyo maana watoto tunawafukuza wasisogelee maeneo ya dampo,” anasema.

Josephine Marambo, maarufu mama Muh, mkazi jirani na dampo anasema hali ya usalama ni ndogo hasa kwa watoto, kwani kuna wakati taka zinashushwa nje ya dampo hasa wakati wa mvua.

“Mvua ikinyesha magari yanashindwa kuingia ndani, yanaruhusiwa kumwaga taka nje hapo, sasa kama watoto wakiwa wanacheza inatulazimu kuwachunga kweli-kweli,” anasema.

Daktari wa binadamu na mtaalamu wa afya ya jamii, Zainabu Hussein anasema madhara ya kiafya wanayoweza kupata watu wanaoishi jirani na dampo ni magonjwa ya mlipuko.

“Kwa wanaoishi jirani na dampo kama dawa zitakuwa hazipulizwi kuua vimelea vya magonjwa basi wapo hatarini kupata magonjwa ya mlipuko,” anasema.

 Kauli ya Serikali ya mtaa

Mjumbe wa mtaa huo wa Mustafa linapopatikana dampo hilo, Juma Jokolo anasema licha ya kuwa na manufaa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini ni changamoto kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na harufu na moshi wa mara kwa mara.

“Tunapata shida, kuna nzi wengi na harufu kali, hapa ikinyesha mvua hali inakuwa mbaya zaidi kwenye hii barabara ya kuingilia dampo,” anasema.

Jokolo (79) anasema kabla ya dampo kuanzishwa eneo hilo lilikuwa mashimo yaliyosababishwa na uchimbaji mchanga.

Akizungumzia changamoto zilizoainishwa na Jokolo na watu wengine, Meneja wa Dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo Manispaa ya Ilala, Richard Kishere anasema: “Inapotokea barabara kutopitika huwa tunakodisha mashine na kukarabati zile zinazowezekana kufanyiwa matengenezo ya haraka.”

Kuhusu taka kujaa mpaka nje anasema: “Unaona hali ya dampo? Kipindi kama cha mvua njia za kuingia ndani hazipitiki. Je, tuzuie magari? Huwezi kuzuia, kwa hiyo eneo lile tumeweka ili magari (yashushe pale) yasikae, kipindi cha mvua kikiisha tutapeleka kwenye maeneo ya ndani zaidi.”

Anasema wanapokea wastani wa tani 900 za taka kwa siku za mwishoni mwa juma na wastani wa tani 1,500 siku nyingine.

“Kuna siku zinafika hadi tani 2,500 kama magari yakiwa mengi,” anasema.

Hata hivyo, Kishere anasema taka zinazopelekwa dampo zimepungua katika miaka ya karibuni.

“Miaka ya 2015 au kabla ya 2018 tulikuwa tunapokea hadi tripu 200,” anasema.

Wakati kukiwa na changamoto ya dampo kujaa, huku takribani nusu tu ya taka zinazozalishwa jijini Dar es Salaam ndizo zinazopelekwa dampo kwa siku, wadau wametaja urejelezaji kuwa suluhu ya tatizo hilo.

Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuzalisha tani 4,600 za taka kwa siku. Kati ya hizo ni asilimia 45 hadi 50 tu zinazopokewa dampo sawa na tani 1,200 hadi 2,000 za taka zinazokisiwa kuzalishwa kwa siku.

 Taka zinazobaki huishia kwenye maeneo ya wazi, mitaro ya maji, barabara na makazi.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayojihusisha na urejelezaji wa takataka ya Rootgis, Antidius Kawamala anasema iwapo vikundi vya urejelezaji taka vikiongezeka na vikawezeshwa tatizo litapungua.

“Bado nasisitiza sera wezeshi na mitaji ikiwekwa vikundi vya urejelezaji vitasaidia kupunguza taka,” anasema.

Sera ya Urejelezaji wa Taka Ngumu ya Jiji la Dar es Salaam ya mwaka 2020 inaeleza:“Uchunguzi umeonyesha kuwa sekta ya urejelezaji taka bado haijatambuliwa na kurasimishwa katika mfumo wa Serikali.

“Kwa sasa kazi hizo zinafanywa na baadhi ya vikundi na kampuni binafsi na wamekuwa wakifanya kazi hizo bila uratibu wa taasisi yoyote ya Serikali, aidha kwa kuwatambua wadau husika na maeneo wanayofanyia kazi za urejelezaji.

“Pia, utafiti mdogo uliofanyika umeonyesha masoko ya bidhaa za taka zinazorejelezwa yanapatikana nchini na nje ya nchi. Aidha, inaonyesha sekta ya urejelezaji wa taka ikisimamiwa na kuratibiwa vyema itaongeza ajira kwa vijana na jamii kuliko ilivyo sasa.”

“Sera inaeleza urejelezaji wa taka ngumu unaweza kusaidia kuongeza viwanda vidogo-vidogo, teknolojia mpya na kipato ambacho kimekuwa kikipotea na kupunguza uchafuzi wa mazingira (hewa, maji na ardhi) hali ambayo huongeza hewa ukaa na kuchangia mabadiliko ya tabianchi.

Madampo ya kisasa Mbeya, Tanga

Wakati dampo linalotegemewa jijini Dar es Salaam likiwa na ukubwa wa hekta 65, likiendeshwa kwa mtindo wa kupokea taka na kushindilia ambao si wa kitaalamu, majiji ya Tanga na Mbeya yanatajwa kuwa na madampo ya kisasa yanayokidhi vigezo kwa mujibu wa Sera ya Mazingira ya Mwaka 2017.

Akizungumzia siri ya kufanya vizuri na kuendesha kitaalamu dampo jijini Mbeya, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Taka Ngumu na Usafishaji, Ramadhan Likwina anasema wanatumia mitambo ya kisasa.

Pia, wanahamasisha  programu ya urejelezaji taka kwa kuruhusu wachakataji kuondoa makopo na mabaki ya vyakula vya mifugo.

“Kufanyia mitambo matengenezo kunasaidia  kuongeza ufanisi wa  kuendesha mifumo ya  usukumaji taka ndani ya dampo kwa kuongeza   uwezo mkubwa wa kuhifadhi na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya dampo,” anasema.

Likwina anasema kwa Mbeya wastani wa asilimia 80 ya taka zinazozalishwa zinakwenda dampo, huku asilimia 20 zilizobaki zinafanyiwa urejelezaji katika programu maalumu.

“Kwa siku wastani wa tani 379 za taka huzalishwa Mbeya ambazo asilimia 80 zinakwenda dampo na asilimia 20 zinazobakia zinafanyiwa urejelezaji, mara nyingi huwa mabaki ya vyakula na makopo,” anasema.

Kwa upande wa Jiji la Tanga, Ofisa Mazingira, Kizito Nkwabi anasema dampo linatajwa kuwa bora kwa sababu kanuni zote zinafuatwa, ikiwamo magari ya taka kupimwa kabla ya kuruhusiwa kuingia.

“Gari la taka linapofika, linapimwa kisha taka zinapelekwa katika eneo husika. Pia, kwa ajili ya kulinda mazingira, miti imepandwa eneo la dampo.

“Utunzaji wa dampo unaanzia mtaani zinapokusanywa taka, hapa Tanga tuna mpango mkakati wa kudhibiti taka kutoka ngazi ya mtaa hadi kata kwa kushirikiana na sekta binafsi,” anasema.

Nkwabi anasema dampo hilo la kisasa lilijengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) kwa gharama ya Sh8 bilioni.

“Dampo letu lilijengwa kwa kufuata vigezo vya kitaalamu, hivyo wananchi wanapaswa kulitunza liweze kudumu, kabla ya kujengwa, lilifanyiwa uchunguzi wa kina kulingana na vigezo vya Benki ya Dunia,” anasema.

Nyongeza na Hawa Mathias (Mbeya) na Raisa Said (Tanga)

Related Posts