SIMBA imetuliza presha kwa Kibu Denis ambaye imefanikiwa kumbakisha, lakini sasa kuna jipya tena na ikizubaa kidogo yule mido asiyechoka mithili ya mnyama punda atang’oka baada ya kutengewa mamilioni ya fedha.
Kiungo huyo, Mzamiru Yassin ambaye kusikia jina lake linavuma ni mara chache sana, ingawa akiwa uwanjani anapiga kazi kubwa kuifichia aibu timu hiyo.
Mkataba wa mchezaji huyo na Simba unafikia tamati mwisho wa msimu huu na timu hiyo inataka kumbakisha ingawa inajivuta kumalizana naye.
Wakati Simba ikisuasua na ahadi zake, Azam imedhamiria kumbeba mido huyo wa kazi na ofa yao ni nzito ambayo tayari imeshautingisha moyo wa Mzamiru, akipima mapenzi yake na Simba aliyoitumikia kwa takribani miaka nane kuanzia Julai 2016 hadi sasa na fedha za matajiri hao wa Chamazi.
Azam inataka kumpa zaidi ya Sh100 milioni kwa mkataba wa miaka miwili ili akavae uzi wa bluu na nyeupe kuanzia msimu ujao, lakini Simba iko chini ya kiwango hicho.
Inaelezwa kwamba Azam hesabu zake inaamini kwamba ataisaidia msimu ujao baada ya kupata changamoto ya majeruhi wengi eneo la kiungo mkabaji, ambapo nyota tegemeo Sospeter Bajana anauguza majeraha baada ya kufanyiwa upasuaji.
Mbali na Bajana, James Akaminko anayecheza eneo hilo ana hesabu za kutaka kuondoka Chamazi jambo ambalo limemshtua kocha Youssouph Dabo akawaambia mabosi wake kuwa kama watampata Mzamiru utakuwa usajili mzuri.
Kwa mujibu wa chanzo cha Mwanaspoti, Azam inawatumia marafiki wengi wa Mzamiru waliopo kwenye kikosi hicho kumlainisha wakimueleza pia kwamba ataungana na baadhi ya wachezaji ambao anacheza nao Simba msimu huu.
Achana na Azam, chanzo kimeeleza kwamba pia Ihefu imetia mguu kwenye hesabu za kumchukua Mzamiru na ikienda mbali na kumtengea Sh150 milioni akitakiwa na kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime.
Inadaiwa Maxime amewaambia mabosi wake kwamba Mzamiru anaishi kwenye eneo ambalo hawajui thamani yake na lifanyike lolote atue ili atengeneze safu ngumu ya kiungo na vigogo hao wameingia msituni kusaka saini yake.
Meneja wa Mzamiru, Carlos Sylvester ameliambia Mwanaspoti kuwa hakuna klabu iliyomalizana na mchezaji huyo, lakini wataendelea kupima ubora wa ofa zote tatu alizonazo mteja wake.
“Nikweli bado Mzamiru hajamalizana na Simba na hii ni heshima kwa Simba ambayo tulitoa kama klabu ambayo mchezaji anamaliza mkataba kwa kuwapa kipaumbele, ila wako kimya,” alisema Carlos ambaye pia ni meneja wa Kibu Denis.
“Kuna ofa zingine kweli, lakini tunaendelea kuzipima kati yangu na mteja wangu, tutakapoona kumetuvutia basi tutamalizana nako kwa maisha ya mchezaji wangu.”
MAFANIKIO YA MZAMIRU SIMBA
Kiungo huyo aliyejiunga na Simba Julai 2016 akitokea Mtibwa Sugar ana miaka minane Msimbazi akicheza kwa mafanikio ambapo amebeba mataji 14 ambayo ni Ngao ya Jamii (5), Ligi Kuu Bara (4), Kombe la FA (3), Kombe la Mapinduzi (1) na Kombe la Muungano (1).
NGAO YA JAMII (2017, 2018, 2019, 2020, 2023)
LIGI KUU BARA (2017–18, 2018–19, 2019–20, 2020–21)
KOMBE LA FA (2016–17, 2019–20, 2020–2021)
KOMBE LA MAPINDUZI (2022)