Trafiki wamwagwa kukagua daladala za Chanika, Kigogo, Kisarawe, abiria walalama

Dar es Salaam. Mamia ya abiria wanaotoka ama kwenda maeneo ya Chanika, Kigogo na Kisarawe wanakutana na adha ya usafiri kwa kushushwa kwenye daladala kutokana na ukaguzi wa makosa mbalimbali kwenye gari hizo unaofanywa na Polisi Kikosi cha usalama barabarani.

Ukaguzi huo umefanyika leo Jumatano Machi 19, 2025 na jeshi hilo katika kituo cha Shule ya Msingi Pugu Kajiungeni ambapo kila daladala iliyopita aidha inakwenda au inarudi maeneo hayo ilikuwa ikisimamishwa.

Mwananchi imeshuhudia zaidi ya daladala 20 zikiwa zimesimamishwa eneo hilo pande zote za barabara huku kukiwa na trafiki zaidi ya 15 wakizikagua gari hizo.

Kwa zile zilizokutwa na makosa, trafiki hao walikuwa wakiwashusha abiria, kung’oa namba za usajili na kuamuru madereva kuzipeleka kituoni.

Pia, Polisi hao walikuwa wakiwasimamia makondakta kuhakikisha wanawarudishia abiria nauli zao.

Adha hiyo imewakumba pia wanafunzi ambao wameonekana kuhaha kutafuta usafiri mwingine na wengine wakilazimika kutembelea, huku abiria wengine wakilazimika kutumia bodaboda kuwahia maeneo waliyokuwa wanakwenda.

Mmoja wa Kamanda aliyekuwa katika shughuli hiyo na kutotaka kutajwa jina lake kwa kuwa yeye sio msemaji wa jeshi hilo, amesema ukaguzi huo ni wa kawaida na ulianza saa 12:00 asubuhi na kati ya makosa waliokuwa wanayaangalia ni kutokuwa na leseni na ubovu wa gari.

Aidha amesema kwa saa mbili walizofanya ukaguzi huo wamebaini madereva wengi wanaoendesha vyombo hivyo hawana leseni.

Kondakta akiwa anawarudishia abiria nauli zao  baada ya kushushwa kwenye gari na Polisi wa kikosi cha Usalama barabarani waliokuwa kwenye ukaguzi wa kawaida eneo la Pugu shule ya Msingi, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Dalaam.

Mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema tangu kutokea ajali Machi 17, 2025 eneo la Pugu Mwisho wa Lami na kumuua aliyekuwa Mkuu wa Polisi Chanika, Awadhi Mohamed Chiko, wamekuwa wakipata adha ya kukaguliwa mara kwa mara.

“Huu ukaguzi wa hivi haujaanza leo hata jana ulikuwepo eneo la pale mwisho wa lami na hii ni tangu ile ajali ilivyotokea juzi, hadi baadhi ya wenzetu wanaojijua magari yao hayapo sawa imebidi wasiingie barabarani siku mbili hizi,” amesema dereva huyo.

Ajali anayoizungumzia dereva huyo ilitokea saa 1:20 asubuhi ya Machi 17, 2025 katika Barabara ya Nyerere maeneo ya Pugu Mwisho wa Lami jijini Dar es Salaam ikihusisha gari aina ya Tata inayofanya safari zake kati Zingiziwa Chanika na Machinga Complex Ilala ikitokea Pugu kwenda Gongo la Mboto iligongana na gari ndogo aina ya Toyota Prado.

Katika ajali hiyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chanika (OCD), Awadh Chico alifariki dunia na kumjeruhi askari, Zubeda Sadala.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele akitoa taarifa za ajali hiyo Machi 17, 2025 alisema ilitokea baada ya dereva wa daladala kuyapita magari yaliyokua mbele yake bila kuchukua tahadhari na kusababisha kugongana uso kwa uso.

“Jeshi la Polisi linamtafuta dereva wa daladala ambaye hajafahamika aliyetoroka baada ya kusababisha ajali hiyo,” alisema Mafwele.

Baadhi ya wananchi waliokumbwa na adha hiyo ya usafiri akiwemo Pili Hassan, mkazi wa Kigogo, amesema amechelewa kwenye biashara yake ya mama lishe kutokana na kushushwa na kulazimika kutafuta gari jingine.

“‘Hapa nilipo nilikuwa nasubiriwa nipeleke mkaa kwa ajili ya kupika, mpaka muda huu wa saa mbili wafanyakazi wangu wananisubiri huko,” amesema Pili.

Charles Boniface, Mkazi wa Chanika amesema utaratibu wa kuwashusha abiria wakiwa katikati ya safiri sio mzuri.

Badala yake Boniface amependekeza kaguzi kama hizo ziwe zinafanyika yanapoanzia magari ili iwe rahisi abiria kutafuta usafiri mwingine.

“Hakuna eneo lina shida kupata usafiri kama hapa kituo cha shule kwa kuwa gari zote zinapita zimejaa, tunaomba trafiki wabadili utaratibu wa ufanyaji kazi zake kwa kuwa nasi tunaelekea kazini asubuhi hii na mabosi wengine sio waelewa,” amesema.

Catherine Msemwa, mkazi wa Kisarawe, amesema ameingia gharama kubwa kupata usafiri ukizingatia alipotoka alizunguka na gari.

Abiria wakiwa wanasubiria kupata usafiri mwingine baada ya kushushwa kwenye daladala walizokuwa wamepanda.

“Hapa kwa kuwa nimeshachelewa imebidi nichukue bodaboda na mwenyewe hadi Kariakoo ni Sh10,000, bajeti ambayo haikuwa kwenye akili zangu lakini kwa kuwa namuwahi mteja ambaye amefika tangu saa moja ananisubiri inanibidi nifanye hivyo ili nisijepoteza,” amesema.

Wakati abiria wakilalamika, bodaboda kwao imekuwa neema kwani kutokana na umati wa watu waliokuwa eneo hilo wakihaha kupata usafiri, sehemu ya kwenda Sh1,000 walifanya hadi Sh3,000 ikiwemo kwenda Gongolamboto.

Related Posts