Waendesha kampeni Lissu apate gari jipya

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kukabidhiwa gari lake lililokuwa limehifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dodoma, baadhi ya watu, wakiwamo makada wa chama hicho, wameanzisha mchango kwa ajili ya kumnunulia gari jipya.

Lissu alikwenda kituoni hapo juzi kuchukua gari hilo ikiwa imepita miaka saba tangu lilipohifadhiwa, baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka bungeni jijini Dodoma Septemba 7, 2017.

Baada ya tukio hilo alipelekwa kwa matibabu Nairobi, nchini Kenya, kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Mei 18 2024, Lissu amesema anautambua mchango huo na ameridhia.

“Huo mchango nautambua, watu wameniambia wanichangie ninunue gari, wakichanga hela ya kutosha nitanunua, hela isipotosha nitatengeneza hili,” amesema.

Akiandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X, mwanaharakati wa mitandao, Maria Sarungi Tsehai amesema amewasiliana na @TunduALissu na ameafiki aweke akaunti zake achangiwe aweze kununua gari.

Aliweka namba zake za simu, akaunti za benki na Swift Code ya benki ya CRDB.

Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini ya Chadema na Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliandika katika ukurasa wake wa X akisema gari hilo halipaswi kutengenezwa hata kidogo.

“Inapaswa kubaki kama kumbukumbu, ili watoto na wajukuu wetu waweze kukumbuka sacrifice (gharama) za wazazi wao katika kupigania demokrasia.

“Tunaweza kabisa kumtafutia Lissu gari nyingine na imara kwa ku pledge only our very small donations (kuahidi michango yetu midogo) na gari hii ikabaki kuwa kumbukumbu ya majaribu tuliyopitia bila kukata tamaa wakati wa ujenzi wa demokrasia.”

Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boniyai, amesema anachangia Sh2 milioni.

“Kwa niaba ya Boniyai Company Ltd, kupitia taasisi yetu Boniyai Foundation nitamchangia Sh2 milioni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kwa ajili ya kutengeneza gari lake au kununua gari mpya kwa jinsi atakavyoona inafaa,” ameandika.

Onesmo Mushi, ambaye ni mwanaharakati amesema umma una wajibu wa kumwezesha Lissu kufanya shughuli zake.

“Nitaungana na wengine kumchangia Lissu apate gari. Pledge (ahadi) – 100,000. Tutamnunulia gari because we care (kwa sababu tunajali), weka mchango wako hapo chini, #IwekweMakumbusho.”

Mwingine aliyehamasisha uchangiaji huo kupitia X ni Joel Msuya, akisema Lissu ni kiongozi  muhimu na mwenye mchango mkubwa katika Taifa.

“Nawaomba Watanzania tuungane kumchangia anunue gari jipya (V8) ikiwezekana tuchange michango mingi anunue magari zaidi ya manne ili moto wake wa mapambano uzidi kukolea kwa kasi.”

Magiri (@Kiganyi_) aliandika, “Kule Zimbabwe wanachama na wapenzi wa upinzani walimchangia kiongozi wao Nelson Chamisa zaidi ya $120,000 (309.77 milioni) kwa ajili ya ununuzi wa gari jipya.Tumchangie Lissu.”

Related Posts