Tshisekedi, Kagame uso kwa uso Qatar, wakubaliana haya

Doha. Baada ya kutoleana maneno makali kupitia vyombo vya habari na wawakilishi hao, hatimaye mahasimu wawili, Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wamekutana ana kwa nama jijini Doha nchini Qatar.

Mkutano huo unafanyika wakati kukiwa na hali ya hatari kutokana na mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC ambapo, Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo, FARDC na waasi wa M23 wanaotajwa kufadhili wa Rwanda.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, imeelezwa kuwa katika mazungumzo hayo mbali na uhusiano wa Tshisekedi na Kagame, pia wamezungumzia hatma ya mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC.

Qatar kupitia kwa kiongozi wake Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, ambaye amesimamia mazungumzo hayo imetaka kusitishwa kwa mapigano kati ya FARDC na wapiganaji wa M23 bila masharti.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Qatar, Kagame na Tshisekedi wote wametaka kusitishwa kwa mapigano hayo mara moja.

“Marais wa nchi hizo walikubaliana haja ya kuendelea na mazungumzo yaliyoanzishwa Doha ili kuweka misingi imara ya amani ya kudumu,” imesema taarifa hiyo.

Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya wawakilishi wa M23 kususia mkutano uliopangwa kufanyika Jumanne nchini Angola kati yao na Serikali ya DRC, baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa juu wa kundi hilo, akiwemo kiongozi wa Muungano wa Waasi (AFC/M23), Bertrand Bisimwa.

Katika taarifa yake, M23 imesema vikwazo hivyo vinahatarisha kwa kiasi kikubwa mazungumzo ya moja kwa moja ya kurejesha amani Mashariki mwa DRC na kuzuia maendeleo katika eneo hilo.

Ulaya pia umeweka vikwazo makamanda watatu wa Jeshi la Rwanda na Mkuu wa Shirika la Madini la nchi hiyo kwa madai ya kuwaunga mkono wapiganaji wa M23.

Mapigano Mashariki mwa DRC yalizidi kuwa makali mapema mwezi Januari, 2025 wakati waasi waliposonga mbele na kuteka mji wa kimkakati wa Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini kisha Bukavu, ambalo ni Jiji kubwa eneo la Kivu Kusini.

M23 ni mojawapo ya makundi takriban 100 yenye silaha yanayopigania udhibiti wa eneo lenye utajiri wa madini Mashariki mwa DRC karibu na mpaka wa Rwanda.

Mgogoro huo umesababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu, ambapo zaidi ya watu milioni saba  wameyakimbia makazi yao na kupewa hifadhi kwenye kambi za wakimbizi huku wengine wakivuka mpaka hadi nchi jirani.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts