Iran imeonya na imekemea kwa nguvu madai ya hivi karibuni yaliyotolewa na viongozi wa juu wa utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump na kuyataja kuwa ni yasiyo na msingi kabisa huku ikilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen.
Amir Saied Iravani, alitoa kauli hii jana Jumatatu kwa njia ya barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja w Mataifa na mwenyekiti wa Baraza la Usalama.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema: “Ningependa kueleza wasiwasi wangu wa kina na kukemea vikali kauli za kivita za hivi karibuni kutoka kwa viongozi wa juu wa utawala wa Marekani, ikiwa ni pamoja na rais wa Marekani, wakati walijaribu kwa nguvu zote kutetea hujuma na uhalifu wa kivita dhidi ya Yemen, ambapo wametoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutishia wazi kutumia nguvu dhidi ya Iran.”
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, tishio lolote litakalotekelezwa dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu kali, zito na la uharibifu.
Kwa uchache watu 53, haswa wanawake na watoto, waliuawa na 101 waliujeruhiwa baada ya Marekani kufanya mashambulio ya kwanza dhidi ya Yemen tangu Trump aingie madarakani Januari.
Trump, katika taarifa yake ya Jumamosi, alisema kuwa Marekani inaitazama Iran kuwa inabeba dhima kamili kwa kuunga mkono harakati za HAMAS.