Mayanga awavuruga Mbeya City akitajwa kuibukia Mashujaa

Tetesi za kuondoka kwa Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga zimeonekana kuwashtua vigogo wa timu hiyo wakieleza kuwa bado hawajapata taarifa rasmi, huku wakitoa msimamo mzito.

Mayanga alijiunga na Mbeya City msimu uliopita, kwa sasa ameonekana kuwa na mafanikio makubwa katika kufikia malengo ya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara huku akitajwa kufikia makubaliano na Mashujaa FC kuziba pengo la Abdallah Mohamed ‘Baresi’.

Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwamo Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, kwa sasa ameonekana kuwa bora baada ya kuivusha Mbeya City hadi robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), akiwatoa Azam FC na Mtibwa Sugar.

Kama haitoshi, katika Ligi ya Championship, Mbeya City ipo nafasi ya pili kwa pointi 49, wakiachwa alama tano dhidi ya vinara Mtibwa Sugar baada ya timu hiyo kucheza mechi 23 wakibakiwa na saba kumaliza msimu.

Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma ameliambia Mwananchi leo Machi 19, 2025 kuwa hawajapata taarifa rasmi zaidi ya kuona mitandao ya kijamii, akieleza kuwa hadi sasa wanafahamu Mayanga ni kocha wao.

Amesema kwa sasa Mayanga anaendelea na majukumu yake kuiandaa timu kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Trasnist Camp, utakaopigwa Machi 21 jijini Dar es Salaam.

“Msimamo juu ya kocha huyo siwezi kusema, kwakuwa Mbeya City ni taasisi, hivyo menejimenti itakaa na kuamua, japokuwa bado hatuna taarifa rasmi, hao wanaotajwa hawajafika kwetu na kocha hajasema chochote,” amesema Nnunduma.

Katibu Mkuu wa Mashujaa FC, Edward Swai amesema taarifa hizo zinabaki kuwa tetesi tu kwani hadi sasa hawajafanya mazungumzo na Mayanga na kufafanua kuwa hakuna kocha waliyemsainisha.

“Hizo ni tetesi tu, lakini kiukweli hatujafanya mazungumzo na Mayanga wala kumsainisha kocha yeyote, ila hadi kesho Alhamisi tutamtangaza kocha mpya kwakuwa kila kitu kinaenda vizuri,” amesema katibu huyo.

Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza kuwa makocha watano, Mayanga, Zuberi Katwila anayeinoa Bigman ya Championship, Adolf Rishard, Malale Hamsini na Charles Mkwasa mmojawapo anaweza kuchukua mikoba ya Baresi aliyesitishiwa mkataba Februari mwaka huu.

Related Posts