Msajili Sanya aanza mchakamchaka kwa mashirika, taasisi za umma Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Unguja

MSAJILI wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammed Ibrahim Sanya, ameanza ziara ya kikazi katika mashirika ya umma na kutoa maagizo kwa menejimenti ya mashirika hayo.

Ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya kila siku ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar katika kuleta ufanisi, uweledi wa taasisi na mashirika ya umma na kutekeleza maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza katika ziara hiyo na menejimenti ya Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Waheed alisema kila shirika lina wajibu wa kufanya vizuri na kuongeza gawio serikalini

Alisema malengo na nia ya Rais Dk. Mwinyi ni kuwa na mashirika yenye ufanisi ambapo maagizo hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Tumeanza ziara ya kikazi, lengo likiwa ni kuimarisha utendaji wa mashirika ya umma kwa kuhakikisha kila shirika linakuwa na mafanikio makubwa” alisema

Alieleza ” Ziara tumeanza toka Machi 17 na inatarajiwa kufanyika hadi Mei 8 kwa Unguja na Pemba kwa mashirika yote ya umma yenye ofisi maeneo hayo.”

Kwa mujibu wa Sanya, katika hiyo ziara anapokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa robo ya Oktoba hadi Disemba 2024.

” Tunajadili mafanikio na changamoto za shirika.Utekelezaji wa Sheria ya Msajili wa Hazina pamoja na kuyaangazia miradi ambayo Shirika inatekeleza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.” alisema.

Aidha, alisema kwa upande wa Bodi za wakurugenzi, Msajili wa Hazina anapokea taarifa za utendaji wa bodi, anapokea taarifa za mafanikio na changamoto zao

Pia, alisema wanajadili na kuweka mikakati ya pamoja na Bodi za mashirika katika kusaidia maendeleo ya mashirika ya umma Zanzibar.

Alisema hadi sasa ameshafanya ziara katika mashirika ya umma mbalimbali ikiwemo Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Shirika la Bima Zanzibar (ZIC).

Hivyo, alisema watakapomaliza ziara hiyo ataandaa ripoti itakayoonesha hali halisi ya kila shirika kwa upande wa menejimenti na bodi za wakurugenzi na baadae atatoa mapendekezo kwa Serikali Kuu juu ya ufanisi wa kila Shirika la Umma.

Related Posts