Waislamu Chato wamuomba Rais Samia kusaidia ujenzi wa msikiti ulioanzishwa na Magufuli

Geita. Waislamuwilayani Chato Mkoa wa Geita wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kusaidia kukamilisha ujenzi wa Msikiti wa Al-huda unaojengwa katika Kata ya Muungano wilayani humo.

Ujenzi wa msikiti huo ulianzishwa kwa juhudi za aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli lakini sasa umegeuka kuwa gofu kutokana na ujenzi kusimama kwa zaidi ya miaka mitano.

Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 2015 alifariki dunia akiwa madarakani Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa makaburi ya familia yake, yaliyopo Chato, mkoani Geita.

Msikiti huo ulioanzwa kujengwa mwaka 2019 na uliwekwa jiwe la msingi Disemba 18, 2019 na Hayati Magufuli na umeishia hatua za ‘lenta’ kwa takribani miaka mitano sasa.

Akizungumza kwenye hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli, jana Jumanne, Machi 18, 2025, Shehe wa Wilaya ya Chato, Abdulrahaman Abdalah amesema msikiti huo ulianzishwa baada ya Magufuli kuomba kujengwa wakati wa mashindano ya Qur’an yaliyokuwa yakiandaliwa na Al-Hikma.

“Hayati Magufuli aliuomba msikiti huu kwa ajili ya wananchi wa Chato, aliweka jiwe la msingi lakini tangu afariki hakuna kilichoendelea, tunaomba Serikali na wadau wamalizie ujenzi huu kwa manufaa ya Waislamu na kama kumbukumbu ya kiongozi wetu mpendwa,” amesema Shehe Adalah

Amesema Msikiti huo unaokadiriwa kuchukua waumini 10,000, umesimama kwa miaka mitano bila maendeleo yoyote, hali inayosababisha eneo hilo kuwa maficho ya wahalifu.

“Kuwepo kwa msikiti huu bila kukamilika kumesababisha eneo hili kuwa pango la wahalifu. Watu wanakabwa usiku hata juzi juzi mtu alikabwa hapa na kunyang’anywa simu lakini ujenzi ukikaa mda mrefu bila kukamilishwa hata majengo yanaharibika,” amesema.

Shehe wa Wilaya ya Chato, Abdulrahaman Abdalah akizungumzia kutokamilika kwa msikiti wa Al-Huda unaojengwa Chato

Shekhe amesema ili kuboresha mazingira ya ibada na kuhifadhi kumbukumbu ya kiongozi huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nyumba za ibada nchini wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie ili kumuenzi Magufuli kwa kumaliza alichokianza.

Amesema kwa mujibu wa mfadhili aliyekuwa akiusimamia ujenzi huo tathmini ya ujenzi inaonyesha zinahitajika zaidi ya Sh1.6 bilioni ili kuukamilisha.

Diwani wa Muungano, Mangesayi Ludomya amesema kutokamilika kwa msikiti huo kunahatarisha usalama wa wananchi kutokana na wahalifu kuutumia kama sehemu ya wao kujificha.

“Tuna imani na Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameendeleza miradi mingi mikubwa ya Hayati Magufuli tunaomba na msikiti huu pia umaliziwe ili kuweka kumbukumbu ya kiongozi wetu aliyekuwa mstari wa mbele kusaidia ujenzi wa nyumba za ibada kwa dini zote,” amesema Ludomya.

Jamila Abdi, mkazi wa Chato ameungana na viongozi hao kuomba msaada wa serikali na wadau kwa ajili ya kumalizia msikiti huo na kusema endapo, endapo utakamilika itakuwa sio tu heshima kwa kiongozi huyo bali pia urithi wenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Hayati Magufuli alijenga maeneo mengi, ikiwemo shule, hospitali na nyumba za ibada hili pia ni jambo alilolitamani kuona Chato inakuwa na msikiti mkubwa na wa kisasa, tunamuomba Rais Samia atusaidie kutimiza ndoto yake,” amesema Abdi.

Amesema katika kipindi cha uongozi wake, Hayati Magufuli alihamasisha na kusaidia ujenzi wa nyumba za ibada za madhehebu mbalimbali, akiamini kuwa nyumba za ibada ni msingi wa maadili mema kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Magufuli, Venance Martin amesema wao kama familia wataungana na Waislamu kuhakikisha msikiti huo unamalizika ili kutimiza ndoto za Hayati Magufuli aliyetamani kuona unajengwa na kukamilika.

Related Posts