‘Vumbi barabara za Kigoma imebaki historia’

Kigoma. ’Vumbi sasa basi.’ Ni kauli ya matumaini kwa wananchi wa Kigoma, wakielezea adha waliyokuwa wakipitia kabla ya ujenzi wa barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu.

Ujenzi wa barabara hiyo ambayo ipo kwenye ushoroba wa kimataifa wa Magharibi unaounganisha pia nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umefikia asilimia 83.

Ujenzi wake umegawanywa katika sehemu nne za utekelezaji, ikijumuisha pia barabara ya Kimataifa ya Tanzania/Burundi, Rumonge Gitaza ya kilomita 45 na ile ya Kabingo-Kasulu -Manyovu ya kilomita 260.6 ambao ujenzi umefikia asilimia 83.

Wakieleza matumaini yao baada ya kukamilika kwa barabara hiyo baadhi ya wananchi wa Kigoma na mikoa jirani wamesema ujenzi wake ni mkombozi, ikiwarahisishia usafiri na kuwaondolea adha ya vumbi nyakati za jua na tope kipindi cha mvua.

“Tulikuwa tunapata tabu, unasafiri kutoka Kigoma kwenda Shinyanga unafika umechafuka kwa vumbi, sisi wenye aleji tunafika tunaumwa, lakini sana adha hiyo haipo tena,” amesema Issa Nurdin mkazi wa Kasulu.

Nyalusi Maira wa Kibondo anasema nyakati za mvua ilikuwa changamoto kwao kusafirisha mizigo hasa mahindi ambalo ni zao linalolimwa kwa wingi eneo hilo.

“Mvua ikinyesha ilikuwa ni tope, tunasafiri kwa tabu, hadi kufikisha mahindi sokoni gharama inaongezeka, lakini sasa tumerahisishiwa, vumbi na tope vimebaki historia, hata gharama za usafirishaji zimekuwa za kawaida,” amesema.

Askofu mstaafu wa Kanisa katoliki, Methodius Kilaini amesema hakuwahi kutarajia kuona barabara ya Kigoma kwenda Bukoba iwe ni lami.

“Nimepita hiyo njia nimeshangaa ni lami kutoka Kigoma hadi Bukoba, ukweli hatuna budi kuishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Askofu Kilaini.

Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Kabingo- Kasulu -Manyovu inayopita katika majimbo matano ambayo ni la Buhigwe, Kasulu Mjini,  Kasulu Vijijini, Muhambwe na Jimbo la Buyungu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema utekelezaji wake unafanyika katika sehemu nne kwa upande Tanzania.

Sehemu ya kwanza ni kipande cha Kasulu – Manyovu cha kilomita 68.25 ambacho ujenzi umefikia asilimia 84.3 na kitakamilika Mei 31, 2025.

Sehemu ya pili ni kipande cha Kanyani Junction – Mvugwe cha kilomita 70.5 ujenzi wake umefikia asilimia 75.3 kitakamilika Oktoba 30, 2025.

“Sehemu ya tatu ni Mvugwe – Nduta Junction kilomita 59.35 uliofikia asilimia 90.7 itakayo kamilika Mei 7, 2025 na sehemu ya nne ni Nduta Junction – Kabingo kilomita 62.50  ambayo imekamilika ipo katika kipindi cha uangalizi,” amesema.

Amesema usanifu wa barabara hiyo ulijumuisha barabara kutoka miji ya Rumonge – Gitaza ya kilomita 45 kwa upande wa Burundi na Kabingo – Kasulu – Manyovu kwa upande wa Tanzania.

“Usanifu ulizingatia uimara wa barabara wa TLC 20; Upana wa mita 11, makalavati makubwa na madogo, mifereji ya maji ya mvua katika maeneo yenye mmomonyoko wa udongo na kuweka alama za usalama barabarani.

“Mradi huu ni muhimu katika kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maeneo ya Mkoa wa Kigoma, Mikoa ya jirani pamoja na nchi za jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na DR Congo,” amesema.

Amesema kukamilika kwa mradi huo ni muhimu katika kufanikisha usafirishaji na kufungua uchumi wa eneo hilo na maeneo jirani.

“Wizara ya ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), itaendelea kusimamia kuhakikisha makandarasi wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mkataba,” amesema, Dk Msonde.

Akizungumza jana Jumanne, Machi 18, 2025 baada ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), mwenyekiti wa kamati hiyo Augustine Vuma Holle amesema ujenzi unaridhisha.

“Tumetembelea mradi kuanzia barabara yenyewe na daraja, unaridhisha, sisi ni wanufaika na watumiaji wa huu mradi  umekuwa ni mkombozi wa Mkoa wa Kigoma,” amesema Holle ambaye pia ni mbunge wa Kasulu Vijijini.

Hata hivyo, mjumbe wa kamati hiyo, Francis Ndulane, alihoji kuhusu kuongezeka zaidi ya Sh80 milioni za gharama za ujenzi wa mradi huo wa Sh400 bilioni.

Akijibu swali hilo, Naibu Katibu Mkuu, Msonde amesema ongezeko hilo limetokana na kipande cha barabara kilichokatika na kuharibiwa kutokana na mvua za El Niño.

“Ni sababu za kimazingira, katika hali isiyokuwa ya kawaida maji yalichimba dongo lote likaporomoka wakati wa mvua za El Nino,” amesema.

Kipande hicho ni cha mita kadhaa kwenye eneo la Busungu lililopo sehemu ya tatu ya ujenzi ya kipande cha kutoka Mvugwe – Nduta Junction.

“Mvua kubwa za msimu zilisababisha changamoto hiyo ya kimazingira, Tanroads wamelisimamia kwa hatua zaidi huku mkandarasi akiongeza nguvu kazi pamoja na vifaa,” amesema.

Hata hivyo, Holle aliiagiza wizara kuhakikisha Tanroads inawasimamia makandarasi wamalize ujenzi kwa muda uliopangwa.

“Huu ni mradi mkubwa ambao umegharimu Sh400 bilioni, tumekagua ubora na uimara, mradi unakwenda vizuri, utekelezaji wake umefikia asilimia 83, ni mradi ulioleta mabadiliko katika Mkoa wa Kigoma, ile adha ya vumbi kwa watu wa Kigoma kufika Mwanza, Shinyanga wamechafuka, haipo tena,” amesema.

Related Posts