Chuo Kikuu Ardhi chapata mwarobaini uhaba wa madarasa

Dar es Salaam. Moja ya kikwazo ambacho Chuo Kikuu Ardhi (ARU) jijini hapa, kinakumbana nacho cha upungufu wa madarasa, kinakwenda kupata ufumbuzi ifikapo Agosti 2025, yatakapokamilika majengo mapya yanayoendelea kujengwa chuoni hapo.

Kwa muda mrefu, Chuo Kikuu Ardhi, kama vilivyo vyuo vingine, kimekuwa kikikabiliwa na uhaba wa madarasa, jambo linalosababisha kushindwa kudahili wanafunzi wengi zaidi.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo manne ifikapo Julai 2025, chuo hicho kitakuwa na uwezo kudahili wanafunzi 6,956, zaidi hivyo kuwezesha kuhudumia jumla ya wanafunzi 14,000.

Haya yamebainishwa leo Jumatano, Machi 19, 2025 na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, ilipotembelea na kukagua ujenzi wa majengo hayo manne yanayojumuisha ofisi za utawala, maabara ya kisasa na madarasa.

Mradi wa majengo manne ni sehemu ya miradi mingi ya vyuo vikuu na mageuzi ya kiuchumi inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ambapo imetengewa Sh972 bilioni kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo.

Profesa Liwa ameiambia kamati hiyo, kuwa chuo hicho kilikosa studio, maabara na karakana, akisema kabla ya hapo walilazimika kwenda kuazima majirani zao ili kuwezesha wanafunzi kusoma.

“Baada ya majengo haya kukamilika adha hiyo haitakuwepo tena na tutaokoa fedha nyingi, maana tulikokuwa tunakwenda tunalipia. Jambo jingine udahili utaongezeka hadi wanafunzi wa ziada 6,956, ambao ukiwajumlisha waliopo watafikia 14,000,” amesema Profesa Liwa.

Kwa mujibu wa Profesa Liwa, majengo hayo yamejengwa na mkandarasi kutoka China, lakini kwa ushirikiano wa walimu na wanafunzi chuo hicho, waliojifunza ujuzi ambao hawana ili baadaye kuwasaidia wengine.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Husna Sekiboko amesema endapo Serikali isingepeleka fedha katika chuo bado changamoto ya uhaba wa madarasa, ukosefu wa karakana ya kujifunzia ingeendelea kuwepo chuoni hapo.

“Majengo haya yanakwenda kupunguza au kutatua changamoto zilizokuwa zikiwasumbua wenzetu wa Ardhi. Msisitizo wetu kwa Serikali miradi yote ikamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane,” amesema Sekiboko.

Mbali hilo, Sekiboko amesema kamati hiyo, inakipongeza chuo hicho, kwa namna ilivyotekeleza mradi kwa viwango vinavyohitajika, akisema wameyatendea haki majengo hayo.

Mjumbe wa kamati hiyo, Hassan Zidadu aliungana na wanakamati wenzake, kukipongeza chuo hicho kwa kutekeleza vizuri mradi huo, ambapo upo mbele ya muda kwa makadirio waliyopewa.

“Baada ya kukagua majengo nilikuwa namuuliza mjumbe mwenzangu, hawa wanatumia rula kujenga maana kuta za zilivyonyooka, hata ukichukua pima maji utaona upo sawa hapa ni kwa wajenzi wenyewe,”amesema Zidadu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema kati ya Sh972 bilioni, chuo kilipata zaidi ya Sh50 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, katika kampasi kuu ya Dar es Salaam, na ya Sengerema mkoani Mwanza.

“Kwa wastani mradi huu, umefikia asilimia 80 ikitarajiwa kukamilika ifikapo Julai mwaka huu. Tuliposema ipo mbele ya muda, kwa hesabu za kawaida sasa hivi tupo asilimia 80, zilizobaki asilimia 20, lakini muda uliobaki ni zaidi ya asilimia 20,” amesema Kipanga.

Related Posts