Mashindano ya Gofu ya ‘NBC Waitara Trophy 2025’ Yazinduliwa Rasmi, Benki ya NBC Yaridhishwa Kasi ya Uibuaji Vipaji Mchezo wa Gofu

Mashindano ya Gofu ya ‘NBC Waitara Trophy’ msimu wa mwaka 2025 yamezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam huku mdhamini Mkuu wa mashindano hayo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau wa mchezo huo hususani katika kuibua vipaji vipya vya mchezo huo.

Hafla ya uzinduzi wa mashindani hayo yanayotarajiwa kufanyika Machi 22 kwenye Uwanja wa klabu la Gofu ya Lugalo jijini Dar es Salaam imefanyika leo klabuni hapo ikihusisha wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo viongozi wa klabu hiyo huku Benki ya NBC ikiwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa benki hiyo Bw David Raymond.

Akizungumza na waandishi wa Habari Bw Raymond alisema udhamini wa benki hiyo kwa miaka minne mfululizo kwenye mashindano hayo yanayolenga kukuza na kuendeleza mchezo wa golf sambamba na kumuenzi muasisi wa mashindano hayo Mkuu wa majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara, umekuwa na mafanikio makubwa kutoakana na ongezeko la kubwa la vipaji vipya vya mchezo huo vinavyoibuliwa kupitia mashindani hayo kila mwaka.

“Kinachotuvutia zaidi kwenye mashindano haya ni kuona kuwa mbali na ongezeko la washiriki wa ndani na nje ya nchi kila mwaka, kumekuwa na ushiriki mkubwa wa watoto ambao kupitia mashindano haya wamekuwa wakifanya vizuri kiasi cha kuwashangaza hadi washiriki wenye uzoefu mkubwa wa mashandano haya. Hatua hii inatuthibitishia uwepo wa vipaji zaidi katika siku zijazo ambavyo vitaendelea kupeperusha bendera ya mchezo huu kimataifa na kuliongezea heshima taifa kupitia mchezo huu,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Bw Raymond, ushiriki wa wadau mbalimbali wa mchezo huo kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi utasaidia kuchochea sekta ya utalii, muunganiko wa kibiashara miongoni mwa washiriki pamoja na kutoa fursa kwa wadau wa ndani wa mchezo huo kuweza kujifunza zaidi na kubadilishana mbinu mbali za mchezo huo na wenzao kutoka mataifa mbalimbali.

“Kama ambavyo tunaendelea kushuhudia maendeleo kwenye michezo mingine tunayoidhamini na kuiandaa ikiwemo NBC Premiere League , NBC Championship League, Ligi ya vijana na mashindano ya riadha ya kila mwaka ya NBC Dodoma Marathon yanayolenga kukusanya fedha kwa ajili kukabiliana na saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama pamoja na kusomesha wakunga ndivyo pia tutaendelea kuwa karibu na mchezo huu wa gofu’’ Aliongeza Bw Raymond

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa muendelezo wa udhamini huo, alisema maandalizi ya mashindano hayo ya siku moja yanaendelea vizuri huku akibainisha kuwa wanatarajia kupokea washiriki kutoka vilabu vyote nchini watakaoshiriki ‘categories’ zote za mashindano hayo yakiwemo mashindano ya wanawake na watoto.

“Muitikio ni mkubwa sana washiriki wanaendelea kuthibitisha ushiriki wao kutoka vilabu vyote kutokana na imani yao kubwa kwenye mashindano haya sababu ikiwa ni pamoja na ubora wake kutokana na maandalizi mazuri kwa kushirikiana na benki ya NBC. Hali ya hewa pia ni rafiki kwa washiriki na hali ya uwanja ni nzuri kutokana na mvua zinzoendelea kunyesha hususani hivi karibuni hali ambayo imesaidia kufanya viwanja vyetu virejeshe hali yake ya ukijani,’’ alisema.

Nahodha wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kepteni Japhet Masai aliwashukuru wadhamini hao kwa kuendelea kufanikisha mashindano hayo kila mwaka huku akiwaomba washiriki mbalimbali kutoka vilabu vyote vya mchezo huo wakiwemo wanawake na watoto kuendelea kujisajili kwa wingi ili kuongeza ushindani kwenye mashindano hayo yatakayohusisha zawadi mbalimbali kwa washindi.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko NBC, David Raymond (katikati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu udhamini wa benki hiyo kwenye mashindano Gofu ya kila mwaka ya ‘NBC Waitara Trophy’ yanatarajiwa kufanyika Machi 22 , mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo (kulia) na Nahodha wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kepteni Japhet Masai

Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu ujio wa mashindano Gofu ya kila mwaka ya ‘NBC Waitara Trophy’ yanayotarajiwa kufanyika Machi 22, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko NBC, David Raymond (katikati) na Nahodha wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kepteni Japhet Masai

Nahodha wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kepteni Japhet Masai (kushoto) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu ujio wa mashindano Gofu ya kila mwaka ya ‘NBC Waitara Trophy’ yanayotarajiwa kufanyika Machi 22, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi. Wanaomsikiliza ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko NBC, David Raymond (katikati) na Mwenyekiti wa Klabu ya Golf ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo (kulia)

Related Posts