Mgodi wa Bulyanhulu mguu sawa kuukabili Ukimwi.

-Wapokea ushauri wa Kamati ya Bunge ya Afya

Na Mwandishi wetu,

Kahama. UONGOZI wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga umeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi kwamba mbali na kushiriki kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya, pia itaelekeza nguvu katika kusaidia jamii inayozunguka mgodi huo kupambana na maambukizi ya VVU.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia wajumbe wa kamati hiyo kutaka kujua ikiwa mgodi huo umeweka mikakati yoyote ya kuisaidia jamii katika kupambana na VVU Ukimwi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilifanya ziara ya kutemebelea mgodi wa Bulyanhulu unaomilikiwa kwa ubia kati ya Barrick Gold na serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals kwa lengo la kujionea pamoja na mambo mengine, utekeleza wa sera ya afya na mikakati ya kupambana na ukimwi.

Meneja wa Mazingira na Mahusiano ya Jamii katika mgodi wa Bulyanhulu Agapiti Paul ndiye aliyetoa ufafanuzi huo na kuiambia kamati kwamba suala hilo litaingizwa katika mipango ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambayo mgodi huo umekuwa ukiitekeleza katika halmashauri za wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga na halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali Meneja Mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu Victor Lule amebainisha miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya ambayo mgodi huo umekuwa ukiitekeleza katika halmashauri za wilaya za Msalala na Nyang’wale.

Anaitaja miradi ya afya iliyotekelezwa na mgodi huo hadi sasa kuwa ni ujenzi wa chuo cha uuguzi Ntobo uliogharimu shilingi milioni 400, upanuzi wa kituo cha afya Bugarama chenye uwezo wa kuhudumia wananchi 50,000 pamoja na ujenzi wa jumla ya zahanati 28 katika halmashauri za wilaya ya Msalala na Nyang’wale.

Meneja huyo wa mgodi wa Bulyanhulu anaitaja miradi mingine ya maendeleo iiliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na mgodi kuwa ni ujenzi wa chuo cha ufundi (Bugarama Vocational Training Authority College-VETA) unaogharimu shilingi milioni 292.5 na ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana Bulyanhulu uliogharimu shilingi milioni 822.

Miradi mingine anaitaja kuwa ni ujenzi wa shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza (Nyang’wale English medium primary school uliogharimu shilingi milioni 300 na ujenzi wa stendi katika mji mdogo wa Segese uliogharimu shilingi milioni 250.

Kwa mujibu wa Lule, miradi mingine ya maendeleo iliyotekelezwa na mgodi wa Bulyanhulu kupitia program ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) anaitaja kuwa ni ujenzi wa stendi ya kuegesha malori ya Isaka uliogharimu shilingi milioni 485 na mradi wa kusambaza mabomba ya maji yenye urefu wa kilometa 55.7 utakaonufaisha jumla ya wananchi 100,000 ukiwa umegharimu shilingi Bilioni 4.

Aidha amesema mgodi wa Bulyanhulu pia umetoa fedha dola za kimarekani milioni 40 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 100 za kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama hadi Kakola ulipo mgodi huo.

Meneja huyo mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu anautaja mradi wa kusambaza umeme katika miji ya Kakola, Bugarama na Ilogi uliogharimu dola za kimarekani Milioni 5 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 13 za kitanzania pamoja na ujenzi wa jumla ya madarasa 87 kati yake madarasa 55 katika halmashauri ya Msalala na madarasa 32 katika halmashauri ya Nyang’wale kuwa ni miongoni mwa utekelezaji wa program ya uwajibikaji kwa jamii uliofanywa na mgodi huo.

Akizungumzia mikakati ya mgodi katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma za afya za uhakika, Lule anasema kwamba kila mfanyakazi amekatiwa bima ya matibabu ikijumuisha mwenza wake pamoja na watoto wasiopungua wane.

“Katika kuhakikisha wafanyakazi wetu wanakuwa na afya bora wakati wote mgodi pia umeanzisha huduma ya ushauri nasaha kwa saa 24, program za mazoezi na michezo mbalimbali pamoja na mfumo wa maisha unaolinda afya zao”anasema.

Akifanya majumuisho ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Hassan Mtenga amepongeza mikakati iliyowekwa na mgodi wa Bulyanhulu katika kuhakikisha wafanyakazi wake wanapata huduma bora za afya pamoja na kujikinga na maambukizo ya VVU.

Anasema kwamba kamati yake imeridhishwa na jinsi menejimenti ya mgodi huo ilivyojipanga katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya hususani mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa.

 

Related Posts