Udom wabuni mfumo kudhibiti madalali wa bei za mazao

Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimeanzisha mfumo wa kisasa wa kurahisisha mnyororo wa ugavi wa mazao kutoka kwa wakulima hadi sokoni kwa kutumia teknolojia ya mtandao (blockchain), utakaosaidia kudhibiti madadali.

Mfumo huu unalenga kuondoa changamoto ya soko, ambapo wakulima wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya ukosefu wa taarifa sahihi za masoko, bei za mazao kubadilika kila wakati, na kupandishwa kwa bei na madalali.

Mfumo huu umeanzishwa kama sehemu ya mradi wa miaka mitatu unaolenga kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa njia ya mtandao, huku ukiepuka kuingiliwa na madalali, ambao mara nyingi wamekuwa wakiwanyonya wakulima kwa kuuza mazao kwa bei za juu.

Hayo yamesemwa leo na Dk Hilda Mwangakala, ambaye ni mhadhiri mwandamizi na mtafiti mkuu katika Idara ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu ya Udom.

Amesema utafiti uliofanywa katika mikoa ya Tabora (kwa tumbaku), Ruvuma (kwa soya), na Mtwara (kwa korosho) umeonyesha mafanikio makubwa.

“Mfumo huu unawasaidia wakulima kupata taarifa za masoko duniani na kuwa na uhakika wa kuzalisha kwa mkataba au kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, kwa kuwa wanajua ni wapi watapata masoko,” amesema Dk Hilda, wakati akizungumza katika kikao cha kutathimini mafanikio ya mfumo huo.

Mfumo huu ni sehemu ya mradi wa miaka mitatu wa kusaidia wakulima kuuza mazao yao kupitia mtandao, huku ukiondoa madhara ya madalali wanaowanyonya wakulima kwa kupandisha bei ya mazao. Mradi huu unafadhiliwa na Canada kupitia Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Utafiti cha nchi hiyo.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Razack Lokina amesema mfumo huo ni hatua muhimu kwa wakulima kwani unaleta mageuzi katika sekta ya kilimo, hasa kwa kuongeza uwazi na kupunguza urasimu katika biashara ya mazao.

“Mfumo huu utasaidia wakulima kupata taarifa muhimu kuhusu masoko kupitia mitandao mbalimbali ya kielektroniki,” alisema Profesa Lokina.

Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Dodoma, Bernard Abraham, alisema kuwa mfumo huo utawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa njia ya mtandao bila kuingiliwa na madalali, ambao mara nyingi wanapandisha bei ya mazao na hivyo kuwaweka wakulima katika hali ngumu.

Abraham amesema mfumo huu utakuwa chachu ya maendeleo katika Mkoa wa Dodoma, na kwa ujumla, utaimarisha biashara ya mazao kwa njia ya kisasa na ya haki.

Katika kikao hicho, mkulima kutoka Chitego, Kongwa, Asha Mwinyi amesema changamoto za madalali katika mchakato wa kuuza mazao ambapo wakulima wengi wamejikuta wakivunja mikataba na wanunuzi wa mazao baada ya madalali kuingilia kati, kuvunja mikataba na kuuza mazao kwa bei ya chini.

“Mfumo huu utatufanya tuwe salama kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeingilia mchakato wetu wa kuuza mazao,” mesema.

Related Posts