Matumizi ya mbolea yameongeza tija kwenye kilimo

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imebaini ongezeko kubwa la matumizi ya mbolea nchini, ambapo matumizi ya virutubisho kwa hekta yameongezeka kutoka kilo 19 mwaka 2020/21 hadi kufikia kilo 24 mwaka 2024/25.

Hali hiyo imeonyesha ni ishara ya mafanikio makubwa katika juhudi za kuboresha kilimo nchini, hasa kwa wakulima wa mazao ya kibiashara.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Machi 18, 2025, na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, wakati akizungumza mafanikio ya Serikali ya awamu wa sita na mwelekeo wa TFRA.

Laurent amesema matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 363,599 mwaka 2020/21 hadi tani 840,714 mwaka 2023/24. Ongezeko hili limechangia katika kuboresha uzalishaji wa mazao na kuongeza tija katika kilimo cha kisasa.

“Lengo letu ni kufikia matumizi ya kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033, kulingana na makubaliano ya wakuu wa nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024,” amesema.

Amesema TFRA imejizatiti kuhakikisha upatikanaji wa mbolea unaendelea kuongezeka, huku akibainisha kuwa upatikanaji umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/21 hadi tani milioni 1.21 mwaka 2023/24.

Laurent amesema kufuatia ongezeko hili, uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/21 hadi tani 728,758 mwaka 2023/24.

Pia, amesema uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 hadi tani 158,628 katika kipindi hicho.

Laurent ametaja pia kuongezeka kwa idadi ya viwanda vya kuzalisha mbolea na visaidizi vya mbolea, kutoka viwanda 16 mwaka 2020/21 hadi viwanda 33 mwaka 2023/24, na kwamba kati ya viwanda hivyo, viwanda vikubwa ni vitatu, vya kati ni 11, na vidogo ni 19.

Amesema kampuni ya ESSA Group kutoka Indonesia imeonesha nia ya kujenga kiwanda cha kuzalisha tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka, ambacho kinatarajiwa kugharimu Sh3.94 trilioni na kutoa ajira 4,500 za moja kwa moja wakati wa ujenzi na 5,000 wakati wa uzalishaji. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza kujengwa mwaka 2029.

Mkulima wa alizeti kutoka Wilaya ya Kongwa, Joackim Peter ameiomba Serikali kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya mbolea, akisema wengi wanaacha kutumia mbolea kutokana na kukosa uelewa wa kutosha kuhusu faida na matumizi yake.

Related Posts