Dar es Salaam. Baada ya kukamilika kwa hatua za manunuzi, hatimaye Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe kwa kiwango cha lami.
Hatua hiyo inakuja miezi miwili baada ya wakala huo, kuweka wazi kwamba ilikuwa kwenye hatua za manunuzi ili kumsaka mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, unaotarajiwa kuwa mworobaini wa msongamano wa magari.
Hata hivyo, kusainiwa kwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika eneo hilo na Dar es Salaam kwa ujumla.
Hafla ya utiaji saini mikataba huo wa ujenzi, imefanyika leo, Jumanne Machi 19, 2025 katika ofisi za Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam.
Meneja wa Tanroads mkoani humo, Alinanuswe Kyamba, amesema mradi huo utaanza baada ya kusainiwa kwa mkataba.
Amesema mradi huo, unatarajiwa kugharimu Sh54 bilioni na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 kuanzia sasa.
“Leo tumetia saini mkataba wa ujenzi wa njia nne kwa kiwango cha lami kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, wenye urefu wa kilometa 3.8,” amesema.
Kyamba amesema mradi huu ni moja ya hatua madhubuti za Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam, kama ilivyoelekezwa na Rais Samia.
“Tunatarajia baada ya ujenzi kukamilika, changamoto ya foleni kuanzia Mbagala Rangi Tatu itakuwa historia,” amesema.
Utekelezaji wa mradi huo, amesema ni juhudi zinazoendelea za Serikali kuboresha miundombinu ya barabara nchini, ili kuwezesha maendeleo na kurahisisha maisha ya wananchi.
Mradi huo utatekelezwa na mkandarasi kutoka China, STECOL Corporation, ambaye ameahidi kukamilisha kazi kwa ubora na kwa muda uliopangwa.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, Ma Ziheng amesema, “Tutahakikisha tunazingatia viwango vya ubora na kukamilisha kazi kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza.”
Awali, Desemba 28, mwaka jana, Mtendaji Mkuu wa Tanroads alisema ujenzi wa barabara hiyo utakwenda sambamba na Daraja la Mto Mzinga uliofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).