Kaseja hesabu kali dhidi ya Tabora Utd

WAKATI Ligi Kuu imesimama kupisha kalenda ya FIFA kwa mechi za kimataifa ambapo Taifa Stars itashuka uwanjani Machi 26 kucheza na Morocco katika mchezo wa kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026, kocha wa Kagera Sugar, Juma Kaseja ameanza hesabu kali kuiwinda Tabora United katika mechi ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

Kaseja amewarejesha wachezaji wa Kagera kambini tayari kujiweka fiti kabla ya kukabiliana na Nyuki wa Tabora ili kuwania nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo kuzifuata JKT Tanzania, Mbeya City na Singida Black Stars zilizotangulia mapema kutinga hatua hiyo.

JKT Tanzania ilitangulia kwa kuing’oa Mbeya Kwanza kwa mabao 2-0, wakati Mbeya City iliifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1 na Singida iliichapa KMC bao 1-0 na sasa zinasubiri kujua wapinzani watakaoumana nao katika hatua hiyo ya robo fainali.

Kagera iliinga 16 Bora baada ya kuing’oa Namungo kwa mabao 3-0 katika mechi ya hatua ya 32 Bora ikiwa nyumbani na safari hii itaifuata Tabora Utd katika mechi hiyo ya 16 Bora itakayoochezwa Machi 28 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseja alisema wameamua kurudi mapema kambini ili kujiweka tayari kwa ajili ya mchezo huo, na pia kulinda ubora wa wachezaji wa timu hiyo ambayo imepata matokeo mazuri katika mechi mbili ilizocheza tangu iwe chini yake, moja ikiwa ni ya Ligi Kuu Bara.

“Tayari wachezaji tangu jana (juzi) wamerudi kambini kwa vile tuna mchezo mgumu mbele yetu ugenini dhidi ya Tabora United ukiondoa umuhimu wa mchezo huo pia tunahitaji kujiweka tayari kwa ajili ya mechi za ligi zilizobaki ambazo pia ni muhimu zaidi kwetu kwasababu ndio zitatuhakikishia kucheza tena msimu ujao,” alisema Kaseja na kuongeza;

“Sio rahisi kuwaacha wachezaji muda mrefu wakiwa majumbani kwao hasa katikati ya mashindano naamini kuwarudisha kambini haraka itasaidia kuwaweka kwenye hali ya ushindani ukizingatia wametoka kushinda hivyo wapo kwenye morali nzuri.”

Kaseja alisema ni muda sahihi wa wachezaji wake kila mmoja kuwajibika kwa lengo la kuipambania timu hiyo ambayo imecheza ligi kwa muda mrefu hivyo sio jambo zuri kuiteremsha daraja.

“Wachezaji wote wamerejea kambini, hatuna majeruhi yeyote kwa sasa, ratiba ya benchi la ufundi jana tumefanya mazoezi mepesi mepesi kwaajili ya kurudisha utimamu baada ya timu kutoka mapumziko ya muda na kesho ratiba itaendelea kama kawaida.”

Kaseja alisema kuwapigisha kwata la kutosha vijana wake katika kujenga utimamu wa mwili pamoja na umakini uwanjani yakiwa ni maandalizi kabambe kuelekea mchezo wao dhidi ya Tabora United.

Related Posts