Kambi ya matibabu ya kibingwa Ruangwa yaacha vilio, DC atoa ombi JAI

MKUU wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma amefunga rasmi kambi maalumu ya Uchunguzi na Matibabu kwa Wakinamama iliyokua ikitoa huduma za matibabu ya kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa na bobezi wa magonjwa tofauti huku ukiacha vilio kwa wananchi hao wenye hali duni za kimaisha wakiwa hawajui hatma yao baada ya kubaini changamoto zao. Anaripoti Yusuph Kayanda, Lindi … (endelea).

Akifunga kambi hiyo katika Hafla ya kuwaaga na kuwapongeza Madaktari hao katika ukumbi wa hoteli ya Ruangwa Pride walipofikia madaktari hao katika kambi iliyoratibiwa na Taasisi ya JAI na kudhaminiwa na Benki ya Amana, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma amewapongeza madaktari hao kwa kufanya kitendo cha kiutu na kizalendo kwa kuokoa uhai wa wanarungwa.

Ngoma ameeleza zaidi ya wagonjwa 1,500 walioonwa na kupatiwa huduma za kibingwa imekua bahati kwao kwa kupata usaidizi wa huduma za kitabibu za kibingwa kwani msaada huo umekua na tija kubwa katika kuokoa Maisha yao baada ya kuteseka na maradhi yao ya muda mrefu.

“Niwahakikishie, kwamba pasipofanyika jambo lolote kama hili, hawa wagonjwa kwa maana ya uwezo wao wa kifedha, hawa ni maiti watarajiwa ndani muda mfupi, kwa sababu nikuhakikishieni, hayupo mwenye uwezo wa kwenda kupata matibabu hata mmoja katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na hivyo hawa wagonjwa 1,500 mliowaona na huduma za kibingwa mlizowapatia, Hawa wangebakia na magonjwa yao mpaka wangekufa na wasingeweza kutafuta huduma hizi,” alisema Ngoma.

Aidha amesisitiza kuwa halmashauri hiyo imeguswa na wananchi wao kupatiwa huduma za kibingwa, kwani bila wao wananchi wake uwezo wa kuzifikia huduma za kibingwa hawana, huku akiiomba Benki ya Amana kuguswa na baadhi ya wagonjwa waliobainika kukutwa na changamoto zaidi zinazowalazimu kusafirishwa kwenda Muhimbili.

Kwa upande wake, Amir Mkuu wa Taasisi ya JAI, Sheikh Yahya Masao ambao ndio waratibu wa kambi hiyo amepongeza mapokezi na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka uongozi wa wilaya ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk. Feisal Said kwa kulifanya zoezi hilo kuwa jepesi.

Masao ameeleza umuhimu wa zoezi hilo kwa jamii ikiwa pamoja na kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji wa matibabu ya kibingwa kwa jamii huku akiishukuru Benki Amana kwa kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na taasisi ya JAI likiwepo jambo kubwa la kuwahudumia wagonjwa wenye uhitaji.

Asha Ibrahim ni miongoni mwa wananchi walioshiriki kupata huduma hizo za kibingwa ameeleza uitikio mkubwa wa wananchi hao unatokana na kuwepo kwa changamoto kubwa za maradhi ya muda mrefu miongoni mwa jamii huku akiiomba JAI na Benki ya Amana kurudi tena kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanaotakiwa kwenda kupata huduma zaidi hospitali ya Taifa Muhimbili.

Naye Afisa wa Kitengo cha Sharia na Bidhaa kutoka Benji ya Amana, Ahmad Nassoro amekiri kuwepo kwa uitikio mkubwa wa wananchi wa Ruangwa katika kambi na kupokea idadi za wagonjwa wanaotakiwa kupatiwa huduma za haraka ambapo wagonjwa 22 wakihitaji matibabu zaidi na wakinamama 20 wakitaji matibabu ya haraka na wengine sita wakihitaji kusafirishwa kwenda Muhimbili ambapo amelipokea ombi la Mkuu wa Wilaya na wananchi na kuahidi kulifikiwa kwa uongozi wa Benki ya Amana.

Related Posts