TRA yapiga ‘stop’ magari kuegeshwa vituo vya mafuta

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepiga marufuku magari yanayopita nchini kuelekea nchi jirani kuegeshwa katika vituo vya mafuta na maeneo mengine ambayo hayajaidhinishwa, ikieleza imebaini njama ya kukwepa kodi.

Hata hivyo, Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa) kwa pamoja vimesema vitatoa tamko.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na TRA jana Ijumaa Mei 17 2024 imeeleza kuwa ni marufuku kwa magari yanayopita nchini kuelekea nchi jirani (IT in Transit) pamoja na magari yanayobeba mizigo inayopita nchini kuelekea nchi jirani kuegeshwa katika vituo vya mafuta.

Mbali na vituo vya mafuta TRA imesema sehemu yoyote ambayo haijaidhinishwa au kupata ruhusa kutoka kwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa magari hayo hayapaswi kuegeshwa.

“TRA inawakumbusha madereva, wasafirishaji na mawakala wa forodha kufuata sheria ya usimamizi wa forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004 pamoja na kanuni zake za mwaka 2010, kinyume cha hapo adhabu kali itatolewa kwa watakaokiuka agizo hili,” inaeleza taarifa hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Hudson Kamoga akizungumza na Mwananchi amesema mizigo inayopaswa kuvuka kwenda nchi jirani haipaswi kukaa nchini kwa zaidi ya siku nne baada ya kugombolewa.

Kutokana na ufuatiliaji walioufanya alisema wamebaini maeneo tajwa kumekuwa na ucheleweshaji wa magari kutoka ndani ya nchi bila sababu.

“Kama gari limeharibika watoe taarifa kwa muda kwa kamishna wa forodha. Tulibaini wafanyabiashara wanatengeneza mazingira mizigo wanayosafirisha kuvuka mipaka ibaki nchini ili kupoteza kodi ya Serikali, hivyo tunawakumbusha kutimiza wajibu wao,” amesema.

Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani alisema hawaoni mantiki ya tangazo hilo na Mei 20, 2024 atawasiliana na TRA na watatoa tamko.

Amesema wanapoingia kwenye vituo vya mafuta hawavunji sheria kwa kuwa vituo hivyo vipo ndani ya mita 100 na wao hawatoki nje ya umbali huo kama sheria ilivyowaelekeza.

Amesema gari linapopata hitilafu eneo pekee wanapoweza kuliegesha ili  kufanya matengenezo ni ndani ya vituo vya mafuta, hivyo TRA wanapaswa kufafanua katazo hilo kwa undani.

Makamu Mwenyekiti wa TAT, Omary Kiponza amesema watatoa tamko rasmi baada ya kuwasiliana na TRA kupata ufafanuzi zaidi.

Related Posts