Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewasimamisha kazi watumishi wa mizani waliokuwa zamu katika mizani kutoka Tunduma, Mkoa wa Songwe, hadi Vigwaza, Mkoa wa Pwani, kupisha uchunguzi.
Agizo hilo limetolewa leo, Alhamisi, Machi 20, 2025, na Waziri Ulega, ambaye ameunda timu ya wataalamu kuchunguza tuhuma zinazowagusa watumishi hao waliokuwa zamu Machi 13, 2025.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa picha mjongeo katika mitandao ya kijamii ikimuonesha dereva aliyetambulika kwa jina moja la Pamela akilalamikia kunyanyaswa katika mzani wa Vigwaza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ulega amesema hatua hizo zimechukuliwa baada ya yeye kushauriana na menejimenti pamoja na wataalamu baada ya Pamela, aliyekuwa akiendesha gari la mzigo lenye tela, kulalamika kuhusu tabia na maneno ambayo yalijitokeza dhidi yake.
“Sasa, baada ya kufanya utaratibu wa kusikiliza kile ambacho alikilalamikia, nilitoa maelekezo kwa wataalamu wangu kupitia Katibu Mkuu kunipatia taarifa ya nini ambacho kimesababisha kadhia ile. Niseme baada ya kupata taarifa ile, inanionyesha zipo sintofahamu ambazo zilijitokeza kutokana na jambo hili,” amesema.
Amesema kwa kusikiliza pande mbili hizo, unagundua kuna tatizo liko wazi ambalo limesababisha kufika katika hatua hiyo iliyofikiwa.
Amesema baada ya kugundua lipo tatizo, ameamua kuchukua hatua za kumwelekeza Katibu Mkuu kuwasimamisha kazi wasimamizi wa mizani wa barabara nzima, kuanzia Tunduma hadi Vigwaza.
“Nimeamua kutoa maelekezo ya kuwasimamisha wale wote waliokuwa katika shifti ile wakati tukio hilo linatokea. Tumefanya hivyo kwa lengo la kufanya uchunguzi, ambapo tumeshaunda timu ya uchunguzi,” amesema.
Amesema timu hiyo itafanya uchunguzi kuanzia mahali ambapo gari hiyo iliingia nchini hadi kufika katika kituo cha Vigwaza, ambako tukio limetokea.
Ulega amesema ili kuwa na uchunguzi huru wa mwenendo wa tukio hilo, watachunguza pia mengine yanayoendelea katika mizani hiyo nchini.
Amesema timu hiyo itahusisha maofisa wa Serikali, ambao wanaamini kuwa watafanya kazi kwa haki na kwa weledi mkubwa.
“Hii timu pia inaweza kutuletea mapendekezo mengine, na hatua zaidi za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote wale ambao wataonekana wamefanya ama wamekuwa na vitendo visivyoridhisha,” amesema.
Amesema kwa kuwa tatizo hilo ni la kujirudiarudia kwa miaka nenda rudi, hali iliyosababisha mtazamo wa Watanzania kuhusu mizani kuwa hasi, ameamua kuchukua hatua madhubuti.
Ulega amesema mizani zinaendeshwa na wanadamu, hivyo mambo yamekuwa mengi, ikiwemo lugha mbaya na baadhi ya watumishi kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa.
Amesema kutokana na hilo, amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani nchini kwa kuwatangazia watu waende na teknolojia za ‘automatic’ badala ya watu kujadiliana.
Amesema mkakati wa muda mrefu ni kuhakikisha mizani zote 78 zinaendeshwa kwa mfumo ambao utapunguza mwingiliano kati ya watu kwenye maeneo hayo.
“Tunataka dereva akifika awe anaongea na mifumo na mashine, na mifumo isomane kwamba kila kituo na kituo kiwe na mawasiliano ya kimfumo. Jambo hili Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwe na mifumo inayosomana,” amesema.
Aidha, Ulega amesema amegundua mizani zote ziko chini ya mameneja wa Tanroads, lakini hivi karibuni wameacha kusimamia ipasavyo mizani hiyo.
“Mameneja ni lazima wawe wasimamizi wa mizani zetu zote hivi… Lakini hapo mbele tutaanza mara moja kuchukua hatua kwa mizani zitakazolalamikiwa, na mameneja tutawachukulia hatua pia. Isiwe ni kwa ajili ya watu wanaosimamia tu. Kwa muda mrefu wamekuwa wakijiweka kando kusimamia hili,” amesema.
Katika picha mjongeo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ilionesha dereva huyo wa magari makubwa ya mizigo, ambaye anafanya kazi kwenye Kampuni ya Simba Logistics, akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari, akisimulia safari yake ya kutoka DRC akiwa amepakia mzigo wa tani 32.
Amesema Machi 13, 2025, alifika katika mzani wa Vigwaza akiwa anatokea nchini Congo, ambapo gari lake lilizuiliwa kwa madai kuwa limezidi uzito.
Alifafanua kuwa alipobisha, akisema amepita mizani yote na hakukuwa na shida, maofisa hao walianza kumnyanyasa, wakimwambia asiwafundishe kazi, na waliingiza gari lake kwenye maegesho huku wakimtaka kulipa faini ya Sh956,400. Alipokataa, waliendelea kumshikilia bila huduma yoyote.
“Nikamuita mwenye mali, akaja na akawaambia wapime ili alipe faini, wakasisitiza wao wapo sahihi. Nikahoji, ‘Kwa nini ni sahihi wakati mizani mingine nimepita bila tatizo, lakini hapa kwenu kuna tatizo?’” amehoji.
“Ndipo mtafaruku ukaanza. Hawakutaka kunisikiliza. Nikachukua jukumu la kuomba vyombo vya habari vije vinisikilize ili nisikike na mamlaka kama Meneja wa Tanroads, Waziri, na Rais, asikie kilio cha madereva kwa kuwa mzani huu ni wa mwisho.”
Kwa mujibu wa maelezo ya dereva huyo, safari yake ilianzia Mpemba, ambako alipita vizuri, Makambako, Mikumi, Mikese, lakini alipofika Vigwaza akaambiwa mzigo wake umezidi.
“Siyo sawa kutokana na nyaraka nilizonazo. Nimeandika barua kwa mamlaka, nikaonekana mkaidi. Naomba Waziri atuangalie sisi madereva wa Tanzania; hatuthaminiki, tunadharaulika, na watumishi wa mizani wamekuwa na mtandao wa kutufuatilia ili ‘tuyaongee’ na wao watu ‘saidie.’ Je, ni haki?” amehoji.
Amedai kuwa ndani ya miezi miwili ya safari zake kutoka Congo, kila anapofika kwenye mzani wa Vigwaza, kiongozi mmoja aliyemtaja kwa jina la Charles humpigia simu na kumkashifu kuwa asiwafundishe kazi kwa kuwa yeye ni mwanamke, hivyo anapaswa kuwa nyumbani kwani hizo ni kazi za wanaume.
“Nataka nipime tena mzani nijihakikishie, kwa kuwa walichoniandikia sina uhakika nacho. Na kama itatokea kupimwa upya, naomba waje watu wapya kutoka wizarani wasimame pale kwenye mashine wanipimie, na ikiwezekana asiwe mimi dereva, bali achukuliwe mwingine apime gari hii ili nijiridhishe, ndipo nitakapokuwa na uhakika wa kulipa.”
“Sijakataa kulipa, wala sijaigomea mamlaka. Namuomba Rais aangalie watu wanaomsaidia kwenye Wizara, kwani wanamgombanisha na madereva, ambao ndiyo wapigakura wake,” amesema.