Unguja. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imezindua ripoti kuhusu ukatili wa kijinsia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuundwa kwa sheria kamili inayoshughulikia tatizo hilo.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika Mjini Unguja leo Machi 21, 2025, Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Shaaban Ramadhan Abdalla amesisitiza umuhimu wa kuwa na sheria moja itakayohakikisha lengo la Serikali kupambana na ukatili wa kijinsia linatimia kikamilifu.
Amesema uzinduzi wa utafiti huo ni hatua moja kuelekea kuwa na sheria inayoendana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Vitendo hivi vimeshamiri na kwa kweli vinaumiza, hivyo hatua hii sasa itatufikisha kupata sheria inayokidhi mahitaji,” amesema.
Shaaban amesema kupatikana kwa ripoti hiyo kutatoa fursa ya kuendelea na hatua nyingine hadi kupatikana kwa sheria kamili.
Akizungumzia ripoti hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Dk Mahfoudh Massoud Ali amesema ina mapendekezo muhimu ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa sheria maalumu ya kusimamia masuala ya ukatili wa kijinsia na utaratibu wa hatua zinazostahiki kuchukuliwa na taasisi kama Jeshi la Polisi, Mahakama, waendesha mashtaka na taasisi nyingine zinazohusika.
Amesema ripoti imependekeza utaratibu wa ufunguzi wa mashauri, haki za waathirika, msaada wa kisheria na uanzishwaji wa nyumba salama kwa waathirika na kulinda watoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Sambamba na hayo, amesema ripoti inapendekeza kuanzishwa mfuko wa kupambana na ukatili wa kijinsia na kuwasaidia waathirika wa vitendo hivyo na kuanzishwa kituo jumuishi ambacho kitahusisha wadau muhimu wa haki jinai.
“Tunapendekeza kuanzishwa chombo maalumu cha udhibiti sambamba na kuanzishwa kituo jumuishi kitakachohusisha wadau muhimu wa masuala hayo ambao watashirikiana katika mapambano,” amesema.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalofanya kazi kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake (UN-Women), Lucy Tesha amesema ukatili wa kijinsia ni tatizo kubwa linalohitaji usimamizi maalumu.
Amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanatiliwa mkazo.
Tesha amesema ripoti hiyo itatoa mwongozo katika kuboresha mifumo ya kisheria na kiutendaji katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Amesema hatua hizo zitasaidia kutoa msaada wa haraka kwa waathirika na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.
Ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa utafiti huo unaolenga kutoa mapendekezo ya kisheria na kiutendaji yatakayosaidia kutatua changamoto kwa lengo la kuboresha mifumo ya kisheria iliyopo.
Ripoti hiyo iliyoanza kufanyiwa kazi mwishoni mwa 2023, imefadhiliwa na UN-Women ikilenga kubainisha changamoto zinazokabili mfumo wa kisheria na kutoa mapendekezo ya kuboresha udhibiti wa ukatili wa kijinsia Zanzibar.