Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema ifikapo Aprili 7, 2025 wawekezaji ambao walikodishwa visiwa vidogo lakini hawajaviendeleza watanyang’anywa.
Kauli hiyo ni mwendelezo wa zilizotolewa awali kwa nyakati tofauti na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua hoteli ya Kisiwa cha Bawe, Unguja wakati wa shamrasharama za sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi, Januari mwaka huu.
Dk Mwinyi alitoa miezi mitatu kwa waliokodishwa visiwa na hawajaanza kuviendeleza wanyang’anywe wapewe wengine, kauli iliyorejewa na Rais Samia aliyesema ikipita miezi mitatu, Dk Mwinyi asirudi nyuma kuchukua hatua.
Akizungumza Machi 20, 2025 na waandihi wa habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff akitoa taarifa kuhusu tamasha la uwekezaji litakalofanyika Pemba amesema visiwa vinne vya uwekezaji vimetolewa kwa wawekezaji ndani ya miaka mitatu lakini bado wawekezaji hawajafanya miradi, hivyo ifikapo Aprili 7, mwaka huu ikiwa hawajaanza utekelezaji vitachukuliwa na kupewa wawekezaji wengine.
Amevitaja visiwa ambavyo vilitolewa lakini havijaendelezwa kuwa ni vya Misali, Matumbini, Mkwata na Mtangani.
“Ikifika mwezi wa nne hawa waliopewa visiwa kama hawajaanza utekelezaji wananyang’anywa rasmi, tayari tumeshawapelekea barua kwa hiyo hakutakuwa na nyongeza,” alisema.
Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (Zipa), ilianza kukodisha visiwa vidogo mwaka 2021, mpaka sasa imekodisha visiwa 16.
Akizungumzia tamasha hilo lililoandaliwa na Zipa, amesema ni maalumu kwa ajili ya uwekezaji litakalofanyika kisiwani Pemba, likilenga kufungua fursa.
Waziri Shariff amesema tamasha hilo litavutia uwekezaji katika uchumi wa Zanzibar, likiwa ni mkakati wa kupata fursa za ushirikiano wa moja kwa moja kati ya wawekezaji, viongozi wa biashara na taasisi za Serikali.
“Tamasha hili linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu Mei 7 hadi 10, katika eneo la uwekezaji Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba,” amesema.
Amesema Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Tamasha hili linawakilisha hatua muhimu katika kuharakishi mabadiliko ya kiuchumi na kukiweka Kisiwa cha Pemba kama kituo cha uwekezaji cha kimataifa,” amesema.
Amesema katika tamasha hilo kutakuwa na mjadala kuangazia mifumo ya sera na mikakati inayolenga kuboresha urahisi wa kufanya biashara na kukuza maendeleo jumuishi kupitia miradi ya uwekezaji yenye tija.
Amesema Serikali inaendelea kuwa thabiti katika kuweka mazingira mazuri ya biashara yanayonufaisha wawekezaji na wananchi wa eneo husika.
“Pemba ina fursa kubwa za uwekezaji, tumejizatiti kuhakikisha mazingira bora ili kuzifanya biashara zistawi na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika visiwa vyetu,” amesema.
Amesema miradi 880 imeshasajiliwa Pemba katika Mamlaka ya uwekezaji ikiwa sawa na asilimia 20.
Waziri amesema kaulimbiu ya tamasha hilo ni “Pemba imefunguka” ikiwa na maana ya mwanzo mpya wa upanuzi wa kiuchumi likionyesha fursa kubwa za kisiwa hicho katika sekta zinazoibuka na kiasili.
Shariff amesema Serikali inatoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kushiriki tamasha hilo ili kuboresha maisha ya wananchi na kuibua fursa mpya za uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohammed amesema katika juhudi za kukifungua Kisiwa cha Pemba, Serikali imewekea vifungu vitatu katika Sheria namba 10 ya 2023 iliyofanyiwa maboresho mwaka jana vinavyoelezea kisiwa hicho juu ya uwekezaji.
Amesema wawekezaji zaidi ya 300 wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hilo kutoka nje ya Tanzania.
Tamasha hilo amesema linahusisha michezo, madarasa maalumu juu ya uwekezaji, taratibu za ajira na vivutio vya biashara vinavyopatikana kisiwani humo.