Wanayopitia wanaume, wanawake wanaoachana kumtunza mtoto

Dar es Salaam. Wakati wimbi la watoto wanaolelewa na mzazi mmoja likiendelea kushika kasi kutokana na ongezeko la wazazi na wenza kutengana baada ya kupata mtoto, imebainika wenza hao hupitia madhila katika mchakato wa malezi ya watoto hao.

Miongoni mwa madhila hayo ni kushindwa kuaminika, hasa wanapoingia kwenye uhusiano mpya na kujikuta wakiishia kuingia kwenye migogoro na wenza wao, kwa sababu ya kuendeleza mawasiliano na wazazi wenzao wa awali.

Hivi karibuni, gazeti hili liliripoti taarifa ya baba wa kambo aliyemuua mtoto wa mke wake na kuufukia mwili wake kwenye shimo la takataka, kwa kile kinachodaiwa alihisi mama wa mtoto huyo ana uhusiano na mzazi mwenzake.

Kilichotokea kwenye familia hiyo ni mfano wa wanayopitia wanawake wengi, ambao hawako kwenye uhusiano na wanaume waliozaa nao na kujikuta wakipita kwenye sintofahamu pale wanapotekeleza jukumu la malezi.

Sintofahamu hii imedaiwa kutengenezwa na wanaume pale mama mwenye mtoto au watoto anapokuwa kwenye uhusiano mwingine, kukiwa na tuhuma kuwa upo uwezekano mkubwa wa wao kurudisha uhusiano kwa kisingizio cha kumlea mtoto.

Mwananchi Digital imezungumza na Juma James (si jina halisi), huyu ni baba wa watoto watano, ameelezea utaratibu wa familia yake ambayo inahusisha pia watoto wawili aliomkuta nao mkewe kabla ya kumuoa.

“Nina watoto watano, wawili niliwazaa kabla ya kukutana na mke wangu wa sasa, yeye pia nilimkuta na watoto wawili, baadaye nikazaa naye mtoto mmoja. Mke wangu anawalea vizuri watoto wote bila kuwabagua.

“Nilichokifanya baada ya kuanzisha uhusiano na huyu mke wangu, nilimfuata mwanaume mwenzangu nikamuuliza kama anataka watoto aliozaa naye waende kwake au tubaki nao sisi. Akaridhia tubaki nao, lakini nikamwambia asije akamsumbua mke wangu,” anasema James.

Anasema walikubaliana akitaka kuwaona watoto wake awasiliane naye, atawapeleka bila shida. “Tumejipangia utaratibu huo,” anasema.

Hata hivyo, anasema shida anayoiona kwa wanaume wengi ni kushindwa kuweka utaratibu wa namna ya kuwaona watoto hao.

Anasema bila kufanya hivyo, kunatoa mwanya wa wawili hao kujikuta wakikumbushana mapenzi yao ya zamani na kujikuta wakiangukia kwenye hatari ya kudhuriana.

 “Ni kweli kama utaona watoto wanatumika kama sababu ya wao kukutana, lazima uwe mkali, ndiyo hayo unazuia kusiwepo ukaribu baina ya baba na mtoto kitu, ambacho si sahihi lakini mazingira ndiyo yanalazimisha wengi kufikia uamuzi huo,” amesema.

Hilo linaelezwa pia na mwanaume mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe aliyesema; “Nimewahi kuwa kwenye uhusiano na mwanamke mwenye mtoto, lakini sikuwahi kuufurahia ule uhusiano kwa sababu kulikuwa na ukaribu kati yake na mwanamume aliyezaa naye.

“Mnaweza kukaa inapigwa simu ya maelekezo, nikaona inawezekanaje mwanamke wangu apewe maelekezo na mwanamume mwingine. Nikaamua kuachana naye na sitaki tena mwanamke mwenye mtoto, maana najua tu baba wa mtoto ataleta usumbufu.”

Hata hivyo, akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema kinachotakiwa ni wazazi kuweka utaratibu mzuri wa kumhudumia mtoto bila kuathiri uhusiano mwingine ulioanzishwa na mzazi mmoja au wote wawili.

Anakiri kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa wazazi waliochana kurudisha uhusiano kwa kutumia mwanya wa kumuangalia mtoto.

“Kuhudumia mtoto hakulazimishi baba awe na ukaribu na mama, kama wameshatengana na mwenza wa awali. Ukaribu kupita kiasi ukiruhusiwa, unaweza kuleta shida kwa sababu ni rahisi kwa watu ambao walishakuwa na uhusiano kukumbushia.”

Hali hiyo ndiyo husababisha wivu, hasa kwa mwanamume aliyemuoa huyo mwanamke kiasi cha wengine kujikuta wakitekeleza ukatili wa kujeruhi na wengine huua watoto au mke mwenyewe.

Anasema Bakwata wanakutana na kesi za aina hiyo nyingi, lakini mara zote huwashauri wahusika waweke utaratibu wa kuwatumia ndugu ili wawe katikati ya baba na mtoto.

“Anaweza kutumika ndugu wa mwanamke au mwanaume ambaye yeye ndiye atakuwa anamchukua au kuwa na taarifa zote za mtoto linapotokea lolote, atahusika kuwaunganisha baba na mtoto,” amesema Sheikh Mataka.

Lakini amesema wapo baadhi ya wanaume wanaelewa, kama mtoto au watoto wake wanaishi na mama yao na ameolewa tena, anaweza kujenga ukaribu na mume.

Amesema hiyo yote analenga kujiweka karibu na watoto wake na hataki mume wa huyo mama ahisi kitu kibaya aendapo kuwaona wanawe.

Hata hivyo, amesema ili kuepukana na kadhia hizo, ni vema kuhakikisha baba na mama wanaishi pamoja na wanalea watoto wao na ikitokea hilo limeshindikana, uwepo utaratibu mzuri wa malezi.

“Nisifiche wapo wanaotumia mtoto kama ndoano na wengine wanakwenda mbele hadi kuwashawishi watoke kwenye ndoa warudi kwao, sasa hapa ndipo matatizo yanapotokea. Suluhisho ni baba na mama kuwa pamoja kwenye ndoa na ikitokea imeshindikana mmeachana na mmoja akaanzisha familia nyingine, basi uwepo utaratibu mzuri wa malezi usio na hila,” anasema.

Mwanasaikolojia Jacob Kilimba anasema ili kumjenga vema mtoto kisaikolojia, ni muhimu alelewe na wazazi wote wawili kwa sababu kukua kwake kuna vitu anavyovitegemea kutoka kwa pande zote mbili.

“Kuna vitu ambavyo hata kama mama ana uwezo kiasi gani, mtoto wake hawezi kuvipata, hivi viko kisaikolojia. Hali ya mtoto kujiamini, ujasiri inatengenezwa na baba yake. Sauti ya baba ni muhimu kwenye malezi ya mtoto. Mama anamtengenezea hali ya huruma, upendo, uwezo wa kusikiliza, kuchangamana na kuwaelewa watu.

“Hivi vitu vinaweza kuonekana vya kawaida, lakini vinatoa taswira ya mtu, kuna mtu kwa tabia zake utajua amelelewa na mzazi mmoja, maana inawezekana tabia fulani zikaonekana zaidi kwake kuliko nyingine ambazo pia ni muhimu,” amesema Kilimba.

Mwanasaikolojia huyo amesema inapofikia hatua ya wanandoa wakaachana, kuna uwezakano mkubwa wa mmoja kubaki na maumivu.

“Hapo sasa ndipo panapoleta athari zinazoanzia kwao na kama wasipopata msaada wa kisaikolojia, zinaweza kwenda kwa mtoto,” anasema.

Anasema wakati mwingine ikitokea mmoja kati yao akabaki na mtoto kisha akaenda kuanzisha uhusiano mwingine, changamoto inaweza kuwa kubwa zaidi.

“Kisaikolojia hii inaweza kumfanya mtoto awe anajiuliza kwa nini mimi naitwa hivi halafu hawa wenzangu wanaitwa jina lingine. Hapo huwezi kumwambia achukulie huyo ndiye baba yake, kwanza si haki kumwambia mtoto baba yako ni huyu wakati uhalisia hauko hivyo,” amefafanua.

Kilimba anasema shida nyingine inaweza kutokea pale baba mzazi anapoamua kuhusika kwenye malezi ya mtoto, wakati kwenye maisha ya yule mtoto kuna mwanamume mwingine.

Anasema hali hiyo lazima imchanganye mtoto na inawezekana kabisa ikamuathiri hadi anapofikia utu uzima.

“Sasa inapotokea kuna mwanamume mwingine anataka kuhudumia au kuingia kwenye familia yake, kisaikolojia ile hali ya uanaume inainuka na kutaka kudai nafasi yake na anaweza asiseme, ila hali hiyo inaweza kumsukuma kufanya kitu kibaya, mfano ukatili au kama hivyo tunavyosikia matukio ya mauaji,” anasema.

Kama alivyoeleza Sheikh Mataka, mwanasaikolojia huyo anakiri kuwa kuna hatari kubwa kwa watu waliowahi kuwa kwenye uhusiano kuwa na ukaribu kwa sababu ni rahisi kwao kurudiana au kuangukia kwenye mtego wa kukutana kimwili.

Amesema watu walioachana huwa na muunganiko wanaokuwa nao ambao huwawezesha kurejeana kivingine.

“Hii inapaswa wanaume waliowaoa wanawake wa aina hii walitambue hilo na watafute namna ya kuzuia hilo lisitokee,” amesema Kilimba.

Mikasa wanayokutana nayo wanawake

Maneno ya mwanasaikolojia huyo yanathibitishwa na visa mkasa ambavyo Mwananchi imevikusanya kutoka kwa wanawake mbalimbali walioachana na wenza wao, wakieleza namna wanavyolazimika kutumikishwa kingono na wazazi wenzao, kama kigezo cha kupata matumizi na huduma kwa watoto.

Moja ya simulizi za wanawake wanaokumbana na hali hiyo, Asma Magana (si jina halisi) anakiri kuwa hulazimika kushiriki ngono na mzazi mwenzie kwa kuwa ndiyo sharti alilompa ili aweze kumhudumia mtoto.

“Sina jinsi, nahitaji huduma ya mtoto, nalazimika kukubaliana na matakwa yake licha ya kujua kwamba ana maisha mengine na mke wake,” anasema Magana.

Kisa kingine ni cha mwanamke aliyetengana na mumewe na kuachiwa watoto wawili akajikuta akibeba ujauzito wa mtoto wa tatu, kisa matunzo ya watoto aliokuwa nao.

Anasema mwanamume huyo ambaye alikuwa tayari ameshaanzisha familia nyingine, alikuwa akikutana naye kimwili alipokuwa akimpelekea huduma za watoto.

Wakati wanawake wakieleza kupata madhila hayo wanaposaka matumizi ya watoto kutoka kwa wazazi wenzao, kilio cha wanaume ni watoto kutumika kama fimbo ya kuwachapia.

Deus Lyimo, mkazi wa Vikindu, Dar es Salaam anasema wapo wanawake wanaowatumia watoto kama silaha ya kuwaumiza wazazi wenzao, hasa linapokuja suala la matunzo ya watoto.

“Unakuta mwanamke umempatia mahitaji yote ya mtoto lakini haachi kukusumbua, mara mtoto anaumwa mara anataka kile wakati huyo mtoto ana bima ya afya. Wakati mwingine si kwamba huyo mtoto ana tatizo kubwa au kuna uhitaji huo wa kusababisha muwasiliane mara kwa mara, lakini anafanya kusudi, hasa akijua kuna mwanamke mwingine uko naye,” amesema Lyimo.

Kwa upande wake, Said Ngomelo, mkazi wa Mtoni amesema licha ya kutambua umuhimu wake kama baba katika kumtunza mtoto,  ananyimwa fursa hiyo kwa sababu ya kutoelewana na mzazi mwenzake.

“Mimi nina mtoto lakini kwa kuwa sina maelewano na mama yake na ameshaolewa na tena nimejikuta niko mbali na mwanangu. Yule mwanamke hataki nimhudumie,” anasema Ngomelo.

Ofisa ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Saalam, Elisha Nyamara anasema changamoto kubwa iliyopo kwa wengi wanaovunja ndoa ni kutofikia makubaliano ya uangalizi wa mtoto au watoto.

“Na mara nyingi watu wanapokwenda mahakamani, huishia kuomba amri moja ya kuvunjwa kwa ndoa, hii ni kwa sababu wakati huo shida yake ni kutokuwa pamoja na huyo mwenza, anasahau kuna suala la mali na haki ya uangalizi wa mtoto au watoto,” anasema Nyamara.

Hata hivyo, anasema inapotokea hali kama hiyo, huwa wanashauri wahusika waende mahakamani kwa hatua zaidi.

Ofisa ustawi huyo anasema mara nyingi migongano huanza linapokumbukwa suala la watoto nje ya utaratibu wa mahakama, huku kila mmoja akitaka haki ya uangalizi na matunzo ya watoto.

Anasema: “Kwenye amri inayohusu watoto, mahakama inatoa maelekezo mawili, kwanza ni haki ya uangalizi na pili ni haki ya kumuona au kuwaona watoto. Kwa kuwa sheria iko wazi hakuna mzazi anayezuiwa kumuona mtoto wake.”

Nyamara anafananua kuwa ikitokea mama anayeishi na watoto tayari ameanzisha maisha mengine, baba anapaswa kutafuta utaratibu wa kuonana na watoto, si kuonana na huyo mama.

“Hapa changamoto ni kutaka kuwa na ukaribu na mwanamke wa mtu kwa kisingizio cha mtoto. Baba anatakiwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwaona watoto wake tu,” anasema.

Wakili Bashir Yakub anasema suala la matunzo ya mtoto, lipo kisheria kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2019, inayoeleza kuwa ni lazima kwa wazazi kumtunza mtoto.

“Kisheria kutoa matunzo ya mtoto ni lazima, hakuna dharura unayoweza kutoa na ukaeleweka kama huwezi kumhudumia mtoto. Pia si sawa kuweka masharti yoyote ili mzazi aweze kumhudumia mtoto wake, huo ni wajibu wake. Kitu ambacho ni wajibu ni lazima kifanyike na haitakiwi kuwekewa sharti lolote.

“Ikiwa mtu anakutana na masharti ya aina hii, ni vyema akachukua hatua za kutafuta msaada wa kupata matunzo ya mtoto au watoto bila kulazimishwa kufanya kitu chochote kisichofaa. Unaweza kwenda polisi kwenye dawati la jinsia na watoto, mhusika ataitwa na kuambiwa anachotakiwa kufanya,” anasema Yakub na kuongeza:

“Njia nyingine ni kwenda ustawi wa jamii ngazi ya wilaya au kata upeleke malalamiko yako, utasikilizwa na kupatiwa msaada”.

Related Posts