Unguja. ACT Wazalendo inasubiri kikao cha Kamati ya uongozi ya chama hicho kufanya tathmini ya mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ili kuamua kuendelea au kukaa pembeni.
Wakati ikisubiria hatua hiyo, chama hicho kimewaagiza viongozi wa majimbo na matawi kupita nyumba kwa nyumba kufanya sensa na kuwatambua wanachama wa chama hicho ukiwa ni mkakati wa kujiandaa kushika dola mwaka 2025.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho wa mikoa ya Kaskazini A na B Mkokotoni Unguja leo Mei 18, 2024, amesema kadri wanavyoendelea kuwa ndani ya SUK watu wanaamini mambo yapo sawa.
“Tuliingia SUK sote tukiwa na imani tukakubaliana ya kutekelezwa lakini hatukutegemea yapuuzwe na mpaka sasa hatuoni dhamana yoyote,” amesema Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Amesema kuendelea kuwemo ndani ya SUK ni kuwaaminisha wananchi na dunia kuwa mambo yanakwenda vizuri tofauti na ilivyo.
Amesema baada ya kuona mambo yanakwenda kinyume iliundwa kamati ya uongozi na kubainisha mambo kadhaa ambayo waliyawasilisha kwa wenzao (ambao hakuwataja) ili yatekelezwe.
Kwa mujibu wa Othman hoja zilizowasilishwa ni pamoja na kila mwenye haki ya kupata cheti cha kuzaliwa apate, mweye haki ya kupata kitambulisho cha Mzanzibari (Zan ID) na kila mwenye haki ya kuandikishwa kupigwa kura aandikishwe.
Mengine ni mfumo wa uchaguzi ufanyiwe marekebisho, sheria ya uchaguzi na sekretarieti vifanyiwe marekebisho na kura ya siku mbili lazima ziondoke.
“Haya ni mambo ya msingi ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho haraka ili kumhakikishia kila Mwananchi kupata haki zake za msingi,” amesema.
Amesema baada ya kuwasilisha mambo hayo waliambiwa wapewe muda wakae wajadiliane.
Hata hivyo, amesema hawana muda wa kusubiri tena, ndani ya mwezi huu watakutana kikao cha kamati hiyo ya uongozi kufanya tathmini na kufanya uamuzi.
“Kwa hiyo wengi walikuwa wanajiuliza kwamba tunakwenda hivi, kwa hiyo hili tunamaliza nalo hivi, jibu ni hapana hatuendi kama mambo yalivyo.”
Othman amesema utofauti wa chama hicho na vyama vingine ni kwamba chama hicho kipo kwa ajili ya masilahi ya nchi lakini wengine wapo kimaslahi binafsi.
“Dhamira yao ni kupata vyeo, sasa hayo ni maradhi tukiyaruhusu yaje kwetu tutapata shida na tutakuwa tumewasaliti wazee walioanzisha harakati hizi,” amesema Othman.
“Kwa hiyo tunaposema dhamira yetu kuikoa nchi hii ni kwa sababu ya haya na leo tusipofanya hivyo tutakuja kupata shida sana na haya hayawezi kupatikana katika chama chochote tofauti na ACT.”
Othman amesema wananchi kisiwani humo wanaishi katika uduni kwa sababu ya kukosa viongozi wenye maono ya kuwakomboa wananchi wake.
Akizungumzia kuhusu ardhi, Othman amesema iwapo ingefuatwa misingi ya sheria wananchi wasingekuwa wanalalamika kuporwa na kunyang’anywa Ardhi zao.
Kwa mujibu wa Othman, ardhi ya Serikali ni fukwe na ardhi nyingine ni mali ya umma lakini imekuwa tofauti.
Amewataka viongozi hao ili kufanikiwa na kufika wanapotakiwa kwenda lazima wajipange vyema na kuzingatia nidhamu katika uongozi.
“Umepewa dhamana, onyesha uongozi na lazima kuwa na kifua cha kuweza kuhimili mambo makubwa na madogo hata usiyoyapenda kuyasikia,” amesema Othman.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema wamepitia misukosuko yote lakini mwisho wa yote yataisha mwaka 2025 kazi iliyoanzishwa na Maalim Seif Sharif Hamad kuipata Zanzibar yenye mamlaka kamili baada ya kushika dola.
Amesema hana wasiwasi kwamba zama za ukoloni wa chama tawala zinafikia mwisho mwakani.
Amewataka viongozi wa majimbo na matawi ndani ya miezi miwili wapate takwimu kamili za wanachama wake kupitia sensa ya nyumba kwa nyumba katika maeneo yao.
“Tupate kila nyumba tujue kuna nani na yupi wa ACT na yupi wa chama kingine na mkishajua wa ACT mjue pia kama ana kitambulisho cha Mzanzibari (Zan ID) na kama amepata kitambulisho cha mpigakura na iwapo hana, ijulikane shida ipo wapi,” amesema Jussa.
Amesema kazi inayofanywa na chama hicho chini ya Othman hawatakubali tena mtu kunyimwa haki yake na kwamba mwaka huu ni wa maandalizi ya kuikomboa Zanzibar kuelekea mwaka 2025.
Jussa amewatahadharisha kuwa wanapopanga mipango yao sio kwamba watu wanafurahia kwa hiyo wajihadhari katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo wasije kuingia vishawishi vya kununuliwa.
“Haya ya tamaa na fitina tutaendelea kuletewa lakini ni muhimu kuendelea kujipanga kuhakikisha tunaikamilisha safari yetu,” amesema.