Mhe. Dkt. Kijaji aitaka Bodi TVLA kusimamia nidhamu kwa watumishi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala uliofanyika Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameitaka Bodi ya Ushauri wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuhakikisha inasimamia nidhamu watumishi wote ambao hawatekelezi majukumu waliyopangiwa.

Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema Machi 21, 2025 kwenye uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.

“Nisisitize kwa wajumbe wa Bodi, msisite kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi watakaothibitika kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali pamoja na watakaotengeneza mazingira ya kupata chochote kwenye huduma ambayo aliiomba kuwahudumia Watanzania.”

“Tufanye kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa, watanzania wanatutegemea sana. Sisi ni watoaji wa huduma lakini pia ni wadhibiti, baadhi ya Taasisi zinajisahau kwenye utoaji huduma, zinajikita kwenye udhibiti. Kwa mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita, udhibiti ni lazima uwe wa kuwezesha uwekezaji na ufanyaji biashara, maelekezo tuliyonayo ni ya kuwezesha wawekezaji wetu.” Alisema Mhe. Dkt. Kijaji.

Mhe. Waziri ameitaka Bodi hiyo itakapoandaa mpango mkakati mpya wa TVLA kujikita kwenye mpango wa Dira yetu ya Taifa ya miaka 25 ijayo ili mpango wa Wakala usomane na Dira ya Taifa inayoanza mwaka 2026 mpaka mwaka 2050.

Sambamba na hilo Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka Bodi ya TVLA kuhakikisha inasimamia kwa ufanisi afya za mifugo nchini ambapo ameitaka Wakala kuwa kituo cha umahiri kutoa bidhaa na kufanya tafiti za Magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao ndani na nje ya nchi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Ndg. Abdul Mhinte alisema kuwa Wizara ina Taasisi nyingi kwenye sekta ya Mifugo lakini TVLA ni Taasisi mama kwani inachangia kwa kiasi kikubwa sekta ya Mifugo isiyumbe kwa hiyo wizara kwa sasa inategemea uwepo wa Bodi uwe na mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya Mifugo.

“Kipindi hiki ambacho mmeteuliwa kwenye hii bodi kwa hakika tunategemea muiendeshe hii Taasisi kiuchumi. Na katika kuonesha hilo tumeona mnashiriki hata kwenye zabuni za kusambaza chanjo nchini. Tunategemea huko mbele tuendako, Taasisi hii itafanya zaidi ya vile inavyofanyika. Na kwa uongozi wenu tunategemea Taasisi hii mbali na kushiriki kwenye zabuni hapa nchini iwe na uwezo wa kushiriki hata nje ya Tanzania, tuweze kuuza chanjo nje na kutoa huduma. Kipindi hiki ni kipindi muhimu, na tunategemea mabadiliko makubwa kwenye Taasisi yetu.” Alisema Ndg. Mhinte.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri TVLA, Prof. Amandus P. Muhairwa amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuwaamini na kuwateua kushika dhamana ya kusimamia na kushauri maendeleo ya TVLA ambayo ni Taasisi muhimu katika uimarisaji wa afya za Mifugo nchini.

“TVLA imekuwa ikifanya kazi muhimu katika kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya Mifugo, uzalishaji, usambazaji na usimamizi wa matumizi bora ya chanjo za Mifugo pamoja na kufanya tafiti za kisayansi zinazosaidia kukuza sekta ya Mifugo nchini. TVLA ni kichocheo muhimu katika kuhakikisha Mifugo inakuwa na afya bora na hivyo kusaidia kuongeza uzalishaji na kipato kwa wafugaji wetu. “ Alisema Prof. Muhairwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) alipokwenda kuzindua Bodi ya Ushauri ya Wakala uliofanyika Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akimkabidhi kitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Prof. Amandus P. Muhairwa Machi 21, 2025 alipokwenda kuzindua Bodi ya Ushauri ya Wakala uliofanyika kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Ndg. Abdul Mhinte akitoa neno la utangulizi pamoja na kumkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kuzindua Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) pamoja na kuongea na wajumbe wa bodi Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Prof. Amandus P. Muhairwa akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuzindua Bodi ya Ushari ya TVLA Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akitoa taarifa kuhusina na kazi zinazofanywa na Wakala kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani) kwenye uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya TVLA uliofanyika Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) aliyoizundua Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa Wakala ulipo Temeke Jijini Dar es Salaam.

Related Posts