Vituko, karaha mikataba ya nyumba za kupanga

Dar es Salaam. Umewahi kupangiwa mtindo wa maisha kwa masharti yaliyomo kwenye  mkataba wa nyumba ya kupanga unayoishi au uliyowahi kuishi?

Swali hili linaakisi uhalisia wa karaha, vituko na maajabu ya masharti yaliyopo kwenye mikataba ya nyumba za kupanga yanayowakumba baadhi ya Watanzania.

Masharti hayo kwa mujibu wa baadhi ya wapangaji, yanalazimu kubadili mtindo wa maisha na wakati mwingine kuenenda na itikadi ambazo ni kinyume cha asili yao.

Wapo waliokwenda mbali zaidi, wakieleza masharti ya mikataba hiyo yamewahi kuwaondoa kwenye nyumba siku chache baada ya kuhamia, wakiacha kodi za miezi kadhaa.

Kuzaa ni wajibu na haki ya binadamu, lakini kwa baadhi ya nyumba ni haramu kwa mujibu masharti ya mikataba yake, kama inavyosimuliwa na mmoja wa wapangaji, daddys_heart kupitia mtandao wa Instagram.

“Hataki mtoto (mwenye nyumba), sasa nimpeleke wapi, ndani mwisho watu watatu,” aliandika daddys, akijibu swali lililoulizwa katika ukurasa wa Instagram wa Mwananchi_official linalohoji ‘Umewahi kukutana na sharti gani la ajabu kwenye mikataba nyumba za kupanga.’

Ukistaajabu ya daddys, yaliyomkuta auntyabdallahrava yatakushangaza. Alikutana na sharti linalokataza mpangaji kupokea wageni, eti watajaza choo.

Sashajacob naye alikutana na sharti la kutoruhusiwa kuwa na uhusiano kimapenzi na mpangaji mwenzake.

Marufuku ya kuingiza mwanamke zaidi ya mmoja, kula kitimoto, miguno kusikika wakati wa tendo la ndoa na hata kuwasha redio kwa sauti kubwa, ni masharti mengine ambayo ni kero zinazoibuliwa na wapangaji.

Licha ya kulalamikiwa kuweka masharti magumu katika mikataba ya nyumba zao, wamiliki wa nyumba wanasema ili kuyaepuka, jenga nyumba yako.

“Kama wanaona masharti magumu wajenge za kwao, nyumba yangu, mimi ndiye ninayeweka masharti,” anasema Mzee Lilla, anayemiliki nyumba ya wapangaji jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ngumu kwa Lavina Joseph kuishi kwenye nyumba ambayo, pamoja na mambo mengine inakatazwa kutandika shuka jekundu, jeupe na kupika pilau.

Kwa mujibu wa Levina, katazo hilo halikutoka mdomoni mwa mwenye nyumba, bali ni sharti la mkataba wa moja ya nyumba za kupanga Tegeta, Dar es Salaam.

Sambamba na sharti hilo, Levina anaeleza kustaajabishwa na sharti la wapangaji kuepuka kuringishiana wenza, alilolikuta katika nyumba ya kupanga Mbezi Beach, jijini humo.

“Nilipouliza wakaniambia kuringishiana kulikomaanishwa ni ile tabia ya leo upo na huyu umeachana naye, kesho na yule unaachana naye keshokutwa mwingine,” anasema.

Juma Abdallah anaeleza alishindwa kumaliza miezi sita katika nyumba ya kupanga Mabibo, Dar es Salaam, baada ya kulazimishwa awe na uhusiano wa kimapenzi na mtoto wa mwenye nyumba.

“Nilikuwa nikimleta mwanamke wangu, yule mama anakaa sebuleni anaimba nyimbo za ajabu, kila muda ananiita. Mwisho wa siku akaniambia niwe na uhusiano na mwanawe na si wanawake wengine,” anasema.

Ingawa halikuwa sharti la mkataba, Juma anasema alilazimika kuhama kutokana na vituko alivyoonyeshwa na mwenye nyumba huyo.

Pamoja na wapangaji kuwa na mita yao, mwenye nyumba wa Rehema Kassim aligoma kuwaruhusu wajinunulie wenyewe umeme.

Badala yake, katika mkataba wa nyumba, ameweka sharti la kila mpangaji kumpa Sh15,000 kwa ajili ya umeme kwa mwezi, hiyo ni tofauti na kodi.

“Wapangaji tuna mita yetu, lakini mwenye nyumba analazimisha hela ya umeme tumpe yeye ndiyo atununulie. Ukimwambia tukusanye wenyewe anatuambia tujenge nyumba zetu.”

“Ukiomba risiti ya luku hataki kuonyesha, tunalipa hela tu. Tupo wapangaji 10, lakini umeme unaisha kabla ya nusu mwezi,” anasena Rehema.

Katika nyumba nyingine, mpangaji hana ruhusa ya kuwa na baadhi ya vifaa vya umeme, likiwemo jokofu.

Kwa mujibu wa Suzan Setao, kwenye nyumba anayoishi hawaruhusiwi kutumia jokofu na hilo ni moja ya masharti ya mkataba.

“Mwenye nyumba anasema jokofu linamaliza umeme, kwa hiyo hatutumii na kama unalo, anakuja kukagua kama limewashwa au la,” anasema.

Katika maelezo yake, Mzee Lilla anasema namna pekee ya kuepuka masharti ni kujenga nyumba yako.

“Mimi kibanda changu (nyumba) siyo cha urithi, nilipambana mwenyewe nikajenga, kwa hiyo naweka masharti kulinda nyumba yangu, mpangaji ni mtu wa kupita, usipokuwa mkali ataharibu kisha anaondoka,” anasema.

Kwa mujibu wa Mzee Lilla, kwa watu, hasa vijana wenye uelewa, masharti hayo wanapaswa kuyageuza changamoto na wawe na shauku ya kujenga nyumba zao.

Aurelia Kimaro, mmiliki wa nyumba Magomeni, Dar es Salaam, anasema tabia za wapangaji ndizo zinazochangia wenye nyunba waweke masharti magumu.

“Kweli ukimpangisha mtu chumba kinakuwa chini ya himaya yake, lakini kwa sababu wewe ndiye unayejulikana chochote atakachofanya aibu ni kwako,” anasema.

“Unakuta mpangaji kila siku analeta mpenzi mpya, nyumba inageuka danguro. Ili kuyaepuka hayo unaweka masharti mapema,” anasema.

Mwanazuoni wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shagembe alisema masharti hayo ni hatari kwa utimamu wa akili.

Hatari hiyo inatokana na alichosema mpangaji analazimika kuingia katika mgogoro wa nafsi kutokana na kusongwa na mawazo.

Mawazo hayo, kwa mujibu wa Shagembe, ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania, yanatokana na kulazimishwa kuishi itikadi usiyoendana nayo.

“Kila binadamu kwa namna alivyolelewa na alivyozoea ana mtindo wake wa maisha, akilazimishwa kuubadili atapata mgogoro wa nafsi.

“Mgogoro wa nafsi husababisha msongo wa mawazo na hatimaye kuathiri afya ya akili ya mpangaji,” alisema.

Ili kuepuka hayo, mwanasaikolojia huyo alipendekeza, ni vema kabla ya kupanga nyumba ukapitia vizuri masharti ya mkataba.

Pia alitaka wapangaji wahoji maswali kwa wenye nyumba kabla ya kulipa fedha ili kujiepusha na matatizo

Licha ya masharti hayo, mtaalamu wa sheria, Patience Mlowe anasema mara nyingi wapangishaji hawafuati masharti ya kisheria.

Anaeleza upangishaji ni biashara rasmi na inatambulika kisheria, chini ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na ndani yake imeeleza nini kinampasa mpangaji na mpangishaji na namna mkataba wa nyumba ya kupanga unavyopaswa kuwa.

“Kwa kawaida wanaofuata sheria ni wale wapangishaji wa nyumba kubwa kama ghorofa na apartments, hawa wa nyumba za kawaida wanaishia kwenye mikataba wanayoandikiana wenyewe,” anasema.

Hata hivyo, sheria hiyo kuanzia kifungu cha 88 inaweka wazi haki za mpangaji, ikiwemo kukaa kwenye nyumba kwa muda aliolipa bila kubughudhiwa.

Matakwa mengine kwa mujibu wa sheria hiyo ni mpangaji kukaa kwenye nyumba ambayo ina uhakika wa ubora.

iwapo kutatokea hali tofauti mwenye nyumba anapaswa kuirekebisha.

Sheria hiyo inatambua kuhusu makubaliano ya mpangaji na mpangishaji ingawa yenyewe imeweka masharti ya jumla.

Related Posts