Maokoto ya gofu hadi mazoezini

KWENYE gofu kuna maokoto ya hapa na pale na yamekuwa yakiwasaidia vijana kupunguza makali ya maisha, pia yanaongeza chachu ya nidhamu ya kazi na kujituma ili kuhakikisha viwango vyao vinakua.

Mzuka wa gofu kwenye Gazeti la Mwanaspoti, linafichua jinsi mazoezi ya gofu yanavyoweza kumfanya mchezaji akaondoka na kibunda cha maana cha pesa, pia yanavyojenga afya zao, kwani wapo baadhi wakiingia kwenye viwanja saa 12 :00 asubuhi wanatoka saa 12:00 jioni, kwa maana wanafanya mazoezi saa 12.

Katika mchezo huo, wanapofanya mazoezi, wachezaji wanachanga pesa na anayeibuka mshindi kwa kupiga mipira michache shimoni anapewa pesa, lakini wapo matajiri wanaoweka pesa mezani ili watu washindane.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na wachezaji kutoka klabu mbalimbali na wamezungumzia jinsi wanavyopata maokoto ya gofu na yanawasaidia kujikimu kimaisha.

Mchezaji wa klabu ya Lugalo, Daud Isiaka anaeleza anavyonufaika na mashindano yasiyo rasmi, wanayachukulia kama mazoezi, lakini wanapata pesa zinazowasaidia kupunguza ukali wa maisha.

“Siku za wikiendi Jumamosi au Jumapili, kuna tajiri anaweka pesa mezani, tunaanza kuzishindania na hiyo kwa upande wa Lugalo imeanza hivi karibuni,” anasema na kuongeza;

“Baada ya kucheza Jumamosi iliopita, nilijinyakulia Sh100,000, siku iliyofuata nikapata Sh40,000, tunawashukuru wanaoweka pesa zao, kwanza inatuongezea ushindani, pia tunapata pesa za kujikimu kimaisha.”

Anasema mashindano hayo yasiyo rasmi, yanawasaidia utimamu wa mwili, kwani wanachukulia kama mazoezi na wakiingia viwanjani saa 12:00 asubuhi wanamaliza saa 12:00 jioni.

“Viwanja vipo 18 hadi kuvimaliza vyote unaweza ukatumia saa tatu hadi nne, ukirudia kucheza mara tatu tunakuwa tumetumia saa 12, hilo linakuwa zoezi tosha,” anasema na kuongeza;.

“Nafanya yote hayo kwa sababu nazingatia kula chakula sahihi, nakunywa maji ya kutosha na matunda kwa wingi, ili kuufanya mwili wangu uwe na nguvu.

Anasema mwanzoni alikuwa mtu mmoja aliyekuwa anatoa pesa na alikuwa anashindana na Isiaka, lengo lilikuwa ni kuwapa motisha ya kupambana, ila kwa sasa ameongezeka wa pili na yanatanuka na kuwa mashindano makubwa.

“Japokuwa siyo rasmi, idadi ya wachezaji imeongezeka na wanaotoa pesa (wadhamini) wapo wawili, naona kinakwenda kuwa kitu kikubwa, kwanza inatujenga kimazoezi na tunapata pesa za kujikimu kimaisha,” anasema na kuongeza;

“Kitendo cha kuwania pesa mazoezini kinatia moyo na kinaongeza umakini, ili kuhakikisha unazipata, hata ukikosa kesho utafanya bidii ili uzipate.”

Pro Rodrick John kutoka klabu ya Dar Gymkhana, anasema wanapokuwa na mashindano mbele yao, wanajikusanya watu wanane na wanajigawa katika makundi mawili kwa maana ya wanne kila upande, hivyo wanachanga pesa na anachukua mshindi wa kwanza na wa pili.

“Tunachukulia kama moja ya mazoezi, tukimaliza viwanja 18 haturudii mara mbili, inasaidia kujituma zaidi mazoezini na tunajipatia kipato, kwani kila mmoja anakuwa ameweka Sh40,000,” anasema.

Mchezaji Lucas Mrundi (handcup moja), kutoka klabu ya TPC, Moshi anasema; “Ni kawaida kufanya mazoezi ya kuwekeana pesa kwenye klabu yao, kila mchezaji anatoa Sh10,000 hadi Wachanga ‘junior’ wanashiriki, mshindi wa kwanza anajinyakulia Sh55,000 zinazobakia zinakwenda kwa mshindi namba mbili.

Anaongeza “Kwa upande wa Junior inawajenga na kuamini mchezo huo ni fursa kwao, kwani katika mazoezi hayo, wanajituma na wanajua anayefanya vizuri kuna kitu anakipata, pia inawajengea uwezo.”

Related Posts