Unguja. Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imemteua Khamis Yusuph Mussa kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Kwahani visiwani Zanzibar.
Hatua hiyo imetokana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika jimbo la hilo, baada ya aliyekuwa mbunge wake (CCM), Ahmada Yahya Shaa kufarini dunia Aprili 8, mwaka huu.
Katika taarifa yake INEC, ilisema uchaguzi huo mdogo utafanyika Juni 8, 2024.
Hayo yameelezwa leo Jumapili Mei 19, 2024 na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alipozungumza na waandishi wa habari Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar.
Kamati Kuu imefanya uteuzi huo, kwenye kikao chake kilichoketi leo Mei 19, 2024 Makao Mkuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar, chini ya Makamu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
CCM imefanya uteuzi huo, huku vyama vikubwa vya upinzani, vya ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF) vikisusia uchaguzi huo. Chadema kwa upande wake ilishaweka msimamo wa kutoshiriki uchaguzi mdogo wowote, unaotokana na uchaguzi wa mwaka 2020.
ACT Wazalendo na CUF vimeususia uchaguzi huu kushinikiza viongozi wa INEC wajiuzulu kuruhusu mchakato wa kupatikana watendaji wapya kulingana na sheria mpya.
CUF mbali na mabadiliko ya viongozi wa tume hiyo, inasisitiza inataka INEC iajiri watumishi wake kwa utaratibu maalumu.
Sambamba na uteuzi wa mgombea huyo, Kamati kuu kwa niaba ya NEC imemteua Suzan Kunambi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), nafasi iliyoachwa wazi na Jokate Mwegelo, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).
Kabla ya uteuzi huo, Suzan alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharib Zanzibar.
Amesema uamuzi wa kumteua Yusuph umezingatia utoshelevu wake katika kuipeperusha bendera ya chama hicho katika jimbo hilo.
“Chama kimejiridhisha kwamba ndugu Yussuf anatosha na ataweza kupeperusha bendera ya chama chetu na kukiletea ushindi,” amesema.
Baada ya uteuzi wa wagombea, kwa mujibu wa INEC, Aprili 24 kampeni za uchaguzi zitaanza hadi Juni 7, mwaka huu, kabla ya uchuguzi wenyewe utakaofanyika Juni 8.
Katika mkutano huo na wanahabari, Makalla amerusha kijembe kwa vyama vilivyosusia kushiriki uchaguzi huo, akisema pengine tathmini waliyoifanya imeonyesha hawana uwezo wa kupambania jimbo hilo.
“Tumefanya uteuzi kwenda kushindana, hivyo inawezekana ACT Wazalendo wamefanya tathmini kwamba jimbo hili hawaliwezi kwa hiyo wakaona wasipoteze nguvu ila tunaamini vyama vingine vinakwenda kushiriki kwa kushindana,” amesema Makalla.