UBORA wa kikosi cha Yanga kwenye misimu mitatu mfululizo, kimemwibua aliyekuwa straika wa timu hiyo, Jerson Tegete na kuwapa tano mabosi kwa kusajili watu wa kazi.
Tegete aliyekuwa mmoja wa nyota wakongwe walioisaidia Pamba ya Mwanza kupanda Ligi Kuu msimu ujao, alisema Yanga ina kikosi kipana na wachezaji wenye uwezo mkubwa, anayeingia na kutoka viwango vinawiana.
Yanga imechukua ubingwa mara ya tatu mfululizo na Tegete alisema ni kutokana na kamati ya usajili kufanya kazi kwa manufaa ya klabu na siyo masilahi binafsi.
“Yanga imesajili wachezaji walioonyesha kiwango kinachostahili kuitwa wa kigeni, wanachokifanya uwanjani kinaonekana wazi, ndio maana imetwaa ubingwa wa tatu mfululizo,” alisema na kuongeza.
“Nikiangalia wachezaji wa Yanga kila mmoja ana uwezo, ukiachana na wanaoanza kikosi cha kwanza, hicho ndicho kinachoitofautisha kidogo na timu pinzani, ilikuwa hivyo kwa Simba ilivyokuwa ikichukua mataji mfululizo, ilikuwa na kikosi bora.”
Tegete pia kazungumzia jinsi ilivyokuwa ngumu Ligi ya Championship, akitofautisha na Ligi Kuu inayotumia mbinu na ufundi, hivyo inakuwa rahisi kuona burudani.
“Ligi ya Championship inatumia nguvu zaidi, nimeona ugumu wake, hivyo timu zinazopanda si kitu rahisi kama wengi wanavyofikiria, huko bila kuwa fiti ni ngumu,” alisema.
Baadhi ya timu alizopitia ni Yanga (2007–2015), Mwadui FC (2015–2017), Majimaji (2017–2018), Kagera Sugar (2018–2019), Alliance (2019) na Pamba aliyopanda nayo Ligi Kuu.