Simba yafuata straika Mzambia, aliyewafunga 2021

SIMBA imefungua mazungumzo na mshambuliaji  Mzambia, Ricky Banda kwa hesabu za kumshusha nchini katika kuboresha safu yao ya ushambuliaji iliyokuwa na kiwango kibovu msimu huu.

Banda ambaye anaitumikia Red Arrows ya Zambia, kwa sasa ndiye roho ya Wazambia hao katika kikosi chao ndani ya Ligi ya Zambia na Simba inapiga hesabu za kumshusha nchini wakifungua naye mazungumzo ya awali.

Ingawa bado hawajafikia mwisho kwenye hatua ya makubaliano, lakini Banda amewaambia Simba hana shida katika kuja kuendelea kuvaa uzi mwekundu baada ya huu anaovaa sasa wa Red Arrows.

Red Arrows ndiyo inayoongoza msimamo wa ligi ya Zazmbia ikiwa na pointi zao 67 ikikimbizana na Zesco yenye pointi 56 na katika mabao yao ya kufunga 43, 10 yamefungwa na Banda, akiendelea kumfukuza Freddy Kouablan aliye Simba kwa sasa na ana mabao 11 kwenye ligi ya nchini humo.

Alisajiliwa na wekundu wa Msimbazi dirisha dogo msimu huu. Andrew Phiri wa Maestro United FC naye ana 11.

Katika kumwania mchezaji huyo, Simba itakumbana na upinzani wa Zesco inayomwania pia na matumaini pekee ya wekundu hao ni ofa yao ni kubwa kuzidi ya timu hiyo inayomilikiwa na Shirika la Umeme la Zambia.

Kama Simba itafika bei kwa Banda, ni wazi mchezaji huyo akachagua kusaini kwa wekundu hao kutokana na shauku yake kubwa ya kuachana na Ligi ya Zambia.

Mshambuliaji huyo amewahi kuifunga Simba mwaka 2021 kwa shuti kali la mguu wa kushoto kwenye mchezo wa marudiano wa mtoano wa Kombe la Shirikisho akifunga moja ya mawili kwenye ushindi wa Red Arrows wa mabao 2-1 nyumbani.

Hata hivyo, Simba ilisonga mbele baada ya ushindi wa mabao 3-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 3-2.

Simba inataka kuachana na mshambuliaji Par Omar Jobe mwisho wa msimu huu baada ya Kouablan kukimbia panga hilo baada ya kuanza kufunga na ana mabao sita hadi sasa ligi kuu, akibakiza bao moja tu kuwafikia viungo washambuliaji Clatous Chama na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wenye mabao saba kila mmoja.

Pia Koublan anahitaji mabao mawili ili kumfikia Jean Baleke aliyepishana naye dirisha dogo.

BANDA NI MSHAMBULIAJI GANI

Akiwa Red Arrows, Banda mwenye mwili mkubwa na urefu wa kutosha wa futi 1.86, msimu huu amekuwa moto akifunga mabao ya aina zote, vichwa na miguu yote miwili na ni mwiba kwa timu pinzani.

Related Posts