YANGA imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa na kutinga fainali.
Ushindi huo uliopatikana kwa bao la Stephane Aziz Ki baada ya kumalizia pasi murua ya Pacome Zouzoua dakika ya 101, umeifanya Yanga kutinga fainali ya mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo.
Mbali na hilo, pia Yanga imeingia fainali ya tano ya michuano hiyo tangu iliporejea msimu wa 2015-2016 na kubeba ubingwa mara tatu.
Fainali ya kwanza Yanga ilicheza msimu wa 2015-2016 ikiifunga Azam mabao 3-1, msimu wa 2020-2021 ikafungwa 1-0 na Simba, huku 2021-2022 ikiichapa Coastal Union kwa penalti, kabla ya 2022-2023 kuinyuka Azam bao 1-0.
Dakika 45 za kwanza zilianza kwa timu zote kushambualiana kwa zamu ambapo Yanga walianza kwa kutengeneza nafasi ya kupata bao kupitia kwa Clement Mzize lakini mshambuliaji huyo akashindwa kufanya hivyo ndani ya boksi baada ya kupiga shuti mtoto ambalo halikumsumbua mlinda lango wa Ihefu, Khomen Abubakar.
Yanga walifanya majaribio mengine kadhaa kupitia kwa Mzize na Aziz Ki ambapo katika mchezo huo ni kama miguu yao ilishindwa kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo waliofurika uwanjani hapo.
Pamoja na kashkashi hizo za Yanga lakini pia Ihefu FC nao walijibu mapigo kupitia kwa nyota wake Duke Abuya, Marouf Tchakei na Elvis Rupia ambao katika mchezo wa leo wamekuwa katika kiwango bora zaidi.
Rupia alifanya majaribio kadhaa ikiwemo ya dakika ya 15 na 16 akiwa ndani ya boksi la Yanga akashindwa kuukwamisha mpira wavuni baada ya kupiga nje na mwingine kumgongesha beki Ibrahim Bacca.
Kukosa umakini kwa safu za ushambualiaji za timu zote ilipelekea dakika 45 za kipindi cha kwanza kukamilika kwa suluhu.
Hata hivyo dakika ya 44 Yanga ilifanya mabadiliko ya lazima baada ya beki wake Nickson Kibabage kudondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Joyce Lomalisa.
Kipindi cha pili kilikuwa kama cha kwanza hakukuwa na mnyonge kila timu ilikuwa imefunguka kutaka kusahiisha makosa ya kipindi cha kwanza lakini tatizo likabaki palepale kushindwa kuzitumia vizuri nafasi.
Joseph Mahundi dakika ya 45 alishindwa kuwanyanyua mashabiki wa Ihefu baada ya kushindwa kuweka kambani mpira akiwa amebaki yeye na kipa wa Yanga, Djigui Diara ambapo mpira ulienda nje.
Aziz Ki naye dakika ya 51 baada ya kuwageuza walinzi wa Ihefu FC alishindwa kuweka mpira kimiani baada ya kupaisha akiwa peke yake dhidi ya mlinda lango la Ihefu.
Licha ya mchezo mzuri ambao umeonyeshwa na timu zote lakini kukosa umakini kwa pande zote ndio imefanya dakika 90 kukamilika bila kushuudiwa bao lolote.
Dakika 15 za kwanza ndani ya zile 30 za nyongeza zilikuwa upande wa Yanga ambao waliweza kunufaika dakika ya 101 kupitia kwa Aziz Ki baada ya kumalizia pasi ya Pacome akiwa ndani ya boksi, bao ambalo limeifanya Yanga kuendelea kuwa na matumaini ya kutetea tena ubingwa wao wa michuano hiyo.
Dakika 15 za pili Yanga walirudi na mikakati mipya ya kuzuia huku wakishambulia kwa kushtukiza ambapo kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi alimtoa Farid Mussa ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kennedy Musonda na nafasi yake akaingia Bakari Mwamnyeto.
Kikosi cha Yanga; Djigui Diara, Yao Kouassi, Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Stephane Aziz Ki na Kennedy Musonda.
Kikosi cha Ihefu; Khomen Abubakar, Faria Odongo, Benson Mangolo, Joash Onyango, Benjamin Tanimu, Kelvin Nashon, Joseph Mahundi, Morice Chukwu, Elvis Rupia, Marouf Tchakei na Duke Abuya.
MABADILIKO YANGA
Waliotoka: Kibabage, Mzize, Maxi, Musonda, Farid Walioingia: Pacome, Guede, Farid, Mwamnyeto na Lomalisa.
MABADILIKO IHEFU
Waliotoka: Kelvin Nashon na Elvis Rupia Walioingia: Amanda Momande na Emanuel Lobota