Helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran, Ebrahim Raisi imeripotiwa kuanguka baada ya kupata shida katika kutua.
Kwa mujibu wa televisheni ya Taifa ya Iran, helikopta hiyo imeanguka leo, Mei 19, 2024 karibu na Mji wa Jolfa, uliopo mpakani na Azerbaijan.
Hata hivyo, taarifa hiyo haijaweka wazi chanzo cha moja kwa moja cha ajali hiyo, ingawa imearifiwa mkuu huyo wa nchi alikuwa safarini katika Mkoa wa Azerbaijan Mashariki wa Iran.
Waokoaji wanasema walijaribu kufika eneo la tukio, lakini hali ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo, ilikwaza jitihada zao, kwa mujibu wa ilivyoripotiwa katika televisheni ya taifa hilo.
Bado haijawekwa wazi kuhusu athari zilizosababishwa na ajali hiyo na hata afya ya kiongozi huyo mkuu wa Iran haijabainishwa.
Lakini wanaodaiwa kuwepo katika helikopta hiyo ni Rais Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian, Gavana wa Azerbaijan Mashariki Malek Rahmati na Mwakilishi wa Viongozi Wakuu wa Iran Mashariki mwa Azerbaijan, Ayatollah Ale-Hashem.
Raisi alikuwa nchini Azerbaijan leo kuzindua bwawa akishirikiana na Rais wa taifa hilo, Ilham Aliyev ikiwa ni la tatu kujengwa na mataifa hayo mawili kwenye Mto Aras.
Tayari Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Muhammad Bukheri amelitaka jeshi la taifa hilo, lile la Jumuiya ya kiislamu na mengine kutumia vifaa vyote kutafuta helikopta hiyo.
Msemaji wa Serikali, Bahadori Jahromi amesema Makamu wa Rais wa Iran, Mohammad Mokhber ameshasafiri kwenda Tabriz karibu na eneo la tukio.