Maumivu ya bei yaja, usafirishaji kwenye meli juu

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na malalamiko ya kupanda kwa bei za bidhaa za chakula kutokana na kupaa kwa mafuta ya dizeli na petroli, huenda kilio hicho kikaongezeka baada ya ongezeko kubwa la gharama za usafirishaji wa mizigo kwa meli.

Sababu ya ongezeko hilo inaelezwa ni ukosefu wa usalama katika safari za meli zinazotoka Ulaya na Asia.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya kampuni zinazosafirisha mizigo kutoka nchi za mabara hayo zimetoa  matangazo ya kuwataka waagizaji kujiandaa na ongezeko la bei, ambalo kwa vyovyote maumivu yake yataishia kwa walaji wa mwisho.

Mwananchi limeona baadhi ya matangazo likiwamo la kampuni ya Mo Cargo, lililoeleza kuwepo kwa ongezeko la bei kwa huduma za usafirishaji mizigo kutoka China na Dubai hadi Dar es Salaam.

“Gharama za usafirishaji zitapanda kiasi ili kukabiliana na changamoto hiyo kwa manufaa ya wateja na kampuni kwa ujumla.”

Mayasa Mpangala anayewakilisha kampuni hiyo amesema wametoa tangazo hilo kutokana na gharama zilizoongezeka.

“Chanzo ni kuongezeka kwa gharama za usafirishaji kwa karibu asilimia 50, hasa nchi za Asia na Ulaya.

Awali, tulikuwa tunasafirisha kontena moja kwa Dola za Marekani 7,000 (Sh18.07 milioni), lakini sasa imepanda hadi Dola 10,000 (Sh25.81 milioni),” amesema.

Hata hivyo, amesema bado wanasubiri kupewa ongezeko la bei na kampuni zilizo nje ya nchi.

“Kuanzia kesho (leo) hadi Jumatano tutajua bei rasmi kutoka kwa kampuni za meli za Ulaya na Asia.

Suala hili limeanza wiki hii yaani, Jumatatu (Mei 13, 2024), kuna mizigo ilikuwa kwenye maghala, mingine ilikuwa imeshapakiwa kwenye makontena, ndio maana tumetoa tangazo,” amesema.

Akieleza sababu za ongezeko hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Meli za Mizigo Tanzania (Tasaa), Daniel Malongo amesema kubwa ni ukosefu wa usalama katika safari inayotoka Ulaya kuja Afrika.

“Sasa hivi meli hazipiti kwa sababu ya usalama, wale maharamia wa Yemen wanazishambulia. Matokeo yake meli zinazunguka hadi Afrika Kusini, kwa hiyo lazima waongeze gharama,” amesema.

Amesema tatizo la usalama limekuwepo kwa miezi kadhaa, ambapo baadhi ya meli zimebadilisha ruti na nyingine zimesitisha safari kabisa.

“Kuna gharama za mafuta na za usalama, maana meli zinaweka walinzi au kusindikizwa. Hizo gharama zote zinapelekwa kwenye freight (gharama za usafirishaji wa meli),” amesema na kuongeza:

“Halafu safari ya Ulaya ikiathiriwa, inaongeza gharama kwa safari za Asia ili kufidia mizigo ambayo inatoka Ulaya na Marekani.”

“Huko rasi kubwa ya China, Asia na Singapore, mahitaji yakiwa makubwa, gharama zinakwenda juu, kwa sababu makontena yanahitajika mengi, inabidi kupeleka makontena matupu yaende kupakia na gharama zake ili kuwahi hizo oda za China lazima ufidie mzigo unaporudi, ndivyo inavyotokea,” amesema.

Ametaja pia sababu ya mizigo kuongezeka, akisema matokeo yake baadhi ya mizigo inakosa nafasi kwenye meli.

“Ushindani ukiwa mkubwa gharama zinapanda, hiyo ni kanuni ya mahitaji na usambazaji. Hizi biashara hazidhibitiwi na mtu, bali ni nguvu za masoko,” amesema.

Pia alitaja suala la meli kuongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam akisema, zinasababisha meli kusubiri muda mrefu nje ya bandari.

“Meli zikikaa sana, gharama zinazoongezeka na wao wanaziweka kwenye freight, japo bandari inajaribu sana kuongeza meli kuingia, lakini meli zimekuwa nyingi,” amesema.

Hata hivyo, amesema wanategemea ujio wa kampuni ya DP World utaongezeka ufanisi.

Mwananchi lilipomtafuta Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kujua juhudi za Serikali kukabiliana na ongezeko hilo, hakupokea simu. Naibu wake, Exaud Kigahe alipopokea simu, amesema hana taarifa za ongezeko hilo.

Akizungumzia ongezeko hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin Mbwana amesema tayari bei za bidhaa zimeanza kupanda.

“Athari ni kubwa, moja ni mfumuko wa bei na pia watu walikuwa hawajajiandaa kwa sababu hiki kitu kimetokea ghafla wiki mbili zilizopita.

“Bei ya kontena imepanda kutoka Dola za Marekani 2,500 (Sh6.45 milioni) mpaka Dola 9,000 (Sh23.23 milioni) kwa hiyo watu wameshindwa kusafirisha mizigo yao kutoka China na India,” amesema.

Amesema asilimia 80 ya bidhaa zinazouzwa katika soko la Kariakoo zinatoka nchi za China na Uturuki na tayari kampuni kubwa za meli zimeshapandisha gharama za usafirishaji.

Amepia changamoto ya kupata makontena ya kusafirisha mizigo, akisema inaongeza ukubwa wa tatizo.

“Gharama zote zinakwenda kwa mlaji wa mwisho, lazima vitu vipande bei, kwanza kupanda dola na gharama za usafirishaji zimepanda ghafla.

“Ukiangalia kibiashara, baada ya matangazo ya kupandisha bei za usafirishaji, watu wenye mizigo kwenye maghala watapanguza uuzaji wakisubiri bidhaa zipungue au wanaangalia bei hiyo itakaa kwa muda gani. Je, imepanda baadaye ikarudi mahali pake au itakaa hapohapo moja kwa moja?”

Alitaja bidhaa zitakazoathirika kuwa ni pamoja na mavazi zikiwemo nguo za aina tofauti, mabegi, pochi na viatu.

Pia kuna vipuri vya magari na matairi, vifaa vya ujenzi vikiwemo vigae, makufuli, vitasa, aluminiam na bidhaa za kiofisi zikiwemo karatasi.

Hata hivyo, Rais wa Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio amesema hawajapata taarifa rasmi ya ongezeko la gharama hizo.

“Kwa kweli hatujapata taarifa rasmi, sisi kazi yetu ni kushusha na kuondoa mizigo, hizi gharama za kulipia usafirishaji ni za mteja. Ni kweli zitamwathiri kwenye kodi kwa sababu wanakokotoa kupitia CIF (gharama ya bidhaa, kusafirisha na bima) mlaji wa mwisho ndiye anayeumia,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Razack Lokina amesema mbinu pekee ni jumuiya za kimataifa kuhakikisha zinadhibiti machafuko yanayoendelea.

Mbali na mbinu hiyo, alieleza ili kuepuka gharama zaidi hasa za kulipuliwa meli, ni vema kubadilisha njia, jambo ambalo linagharimu muda na fedha.

“Ukisema unabadilisha njia ya safari utalazimika kuongeza siku za kusafirisha mzigo na kutumia fedha nyingi, muhimu ni kusitisha vita ndiyo suluhisho pekee,” amesema Profesa Lokina.

Hali ikiwa hivyo, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Aprili 2024 imeonyesha kupungua kwa uingizwaji wa bidhaa kutoka Dola 17.12 milioni (Sh44.2 trilioni) mwaka 2023 hadi Dola 16.033 milioni (zaidi ya Sh41.38 trilioni) Machi 2024.

Ripoti hiyo imeonyesha kupungua kwa uingizaji wa mashine na mitambo kwa asilimia 1.5 na upungufu mwingine umeshuhudiwa katika bidhaa za mitaji kwa asilimia 10.5

Bidhaa za viwandani zimepungua kwa asilimia 8.1, plastiki kwa asilimia 14.5, mbolea kwa asilimia 49.7, mafuta na vilainishi kwa asilimia 19.7, mafuta ghafi asilimia 21.5.

Nyingine zilizopungua kuingia nchini ni sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani kwa asilimia 17.4, vyakula na  vileo kwa ajili ya majumbani kwa asilimia 16.6, pikipiki kwa asilimia 1.1 na sabuni kwa asilimia 14.9.

Hata hivyo, zipo bidhaa zilizoongezeka kuingizwa nchini ikiwemo karatasi na bidhaa zake (asilimia 28.6), viatu na bidhaa nyingine (asilimia 6.1), nguo (asilimia 11.9) na viuadudu (asilimia 59.6).

Kadhalika, zipo dawa za binadamu (asilimia 0.8), magari kwa matumizi binafsi (asilimia 25), mafuta yaliyosafishwa (asilimia 1.9), ngano (asilimia 18.5), vyakula kwa ajili ya viwandani (asilimia 12.6) na vipuri (asilimia 2).

Bidhaa za chuma ziliongezeka kwa asilimia 21.8, mashine za kielektroniki kwa asilimia 25.7 na vifaa vya usafirishaji viwandani kwa asilimia 0.8.

Ripoti hiyo ya Machi 2023, ilionyesha bidhaa zilizoongoza kwa kuingizwa ni pamoja na mashine na mitambo ya kimakanika, vifaa vya usafirishaji mashine za umeme na bidhaa nyinginezo za mitaji, ikielezwa kuwa ongezeko hilo lilitokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya reli ya kisasa (SGR) na bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Related Posts