Umuhimu wa kuachanisha uzao mmoja na mwingine

Zimebaki  siku chache ili kuadhimisha siku ya Afya Duniani ambayo inaadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Aprili chini ya mwamvuli wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Kampeni ya siku hii kwa mwaka huu inaangazia afya ya uzazi na watoto, na kuzitaka serikali na jumuiya ya afya duniani kuimarisha juhudi za kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika vya uzazi na watoto wachanga.

Vile vile wanatakiwa kuweka kipaumbele kwa afya ya muda mrefu na ustawi wa wanawake.

Umuhimu wa mada hii unaonyeshwa na takwimu za kutisha: Takribani wanawake 300,000 ulimwenguni kote hufa kila mwaka kwa sababu ya ujauzito au shida zinazohusiana na uzazi.

Huku pia zaidi ya watoto milioni mbili hufa ndani ya mwezi wao wa kwanza wa maisha, na karibu milioni mbili zaidi huzaliwa wakiwa wamekufa.

Takwimu hizi hutafsiri takriban kifo kimoja kinachoweza kuzuilika kila sekunde saba.

Kuunga mkono juhudi hizi, leo tutapata ufahamu wa uhitaji wa kuachanisha uzao mmoja na mwingine katika familia. 

Katika maendeleo ya ukuaji na malezi bora kwa mtoto mmoja na mwingine wa tumbo moja, inashauriwa kuzingatia uachanishaji wa uzao mmoja na mwingine katika muda unaokubalika kitabibu.

Tafiti za zinaonyesha muda rafiki kuachanisha kubeba ujauzito mmoja na mwingine ni kati ya miezi 18-24 au mwaka mmoja na nusu mpaka miwili.

Tafiti za kitabibu zinaonyesha yapo matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza kwa kuzaa kwa mkaribiano yaani mpishano wa miezi sita kutoka mimba moja na nyingine.

Matatizo hayo ya kiafya ni pamoja na matatizo ya awali ikiwamo watoto kuzaliwa njiti, kuzaliwa na uzito mdogo, maumbile yasiyo timilifu au kuzaliwa na dosari ya kimaumbile.

Matatizo ya hapo baadaye yanayoweza kujitokeza ni pamoja na hatua za ukuaji kutofikiwa kwa wakati, udumavu, uwezo wa kiakili kuwa mdogo au kuwa katika hatari ya kupata matatizo ya akili.

Kwa watoto wanaoishi katika nchi zenye uchumi mdogo endapo kuna ukaribiano wa kuzaliwa kwa miezi 6-12 huwa katika hatari zaidi ya kupata utapiamlo kutokana na kutopata lishe yakutosha.

Watoto katika maeneo  haya wanapokuwa watoto watatu waliokaribiana, mahitajio yao ya chakula na malezi kutoka kwa wazazi huwa hayawatoshelezi.

Mara nyingi huwa katika hali ya ushindani au kugombania au kunyang’anyana katika kila kila kitu ikiwamo hitajio la ulezi kutoka kwa wazazi na chakula.

Hali kama hii huweza kuwafanya watoto kupata utapiamlo kirahisi na kukosa furaha kutokana na kutotimiziwa mahitaji yao.

Kwa mwanamke ambaye uachanishaji wake ni wa chini ya miezi 12 ambaye kila uzao humhitaji kunyonyesha, huwa katika hali ngumu kiafya ikiwamo kupata upungufu wa virutubisho muhimu mwilini.

Matokeo yake ni kupata upungufu wa damu mara kwa mara na kinga kuwa dhaifu hatimaye kuwa katika hatari ya kuvamiwa kirahisi na vimelea wa maradhi.

Yapo pia madhara yanayojitokeza wakati wa kujifungua ikiwamo majeraha ya njia ya uzazi na viungo ambavyo viko jirani na eneo la nyumba ya uzazi.

Vile vile mkaribiano wa uzazi chini ya miezi 6-12, humfanya viungo vyake vya uzazi kutojianda vyema kustahimili madhara na mabadiliko wakati wa ujauzito.

Tafiti zinaonyesha kuwa ustahimilivu wa mabadiliko ya ujauzito ni imara kwa mwanamke wa umri wa miaka 35 endapo ataachanisha uzao kwa zaidi miezi 12.

Kuachanisha uzao kwa nchi za uchumi wa kati kama Tanzania inaleta matokeo chanya kwa afya ya mama na mtoto.

Muhimu kwa mwanamke kupata ufahamu zaidi wa afya ya uzazi kabla ya kuamua kubeba ujauzito.

Related Posts