Nahodha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta amehitimisha vyema msimu wa 2023/2024 baada ya timu yake PAOK kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ugiriki kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Aris, jana.
Matokeo hayo yameifanya PAOK kumaliza ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ugiriki ikikusanya pointi 80, mbili mbele ya AEK iliyomaliza katika nafasi ya pili.
Brandon Thomas na Taison walikuwa mashujaa wa PAOK kwa kufunga mabao mawili yaliyoihakikishia ubingwa na tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Bao pekee la wenyeji, Aris katika mchezo huo lilifungwa na Loren Moron.
Katika mchezo huo, Samatta alianzia benchi, lakini aliingia uwanjani katika dakika ya 65 kuchukua nafasi ya mfungaji wa bao la kwanza Thomas.
Samatta licha ya kuvaa medali ya ubingwa, amepitia ukame wa muda mrefu wa kufumania nyavu ndani ya timu hiyo msimu huu huku akianzia benchi mara kwa mara na nafasi yake amekuwa akianzishwa Thomas kutoka Hispania.
Kuthibitisha hilo, nahodha huyo wa Taifa Stars amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya Ugiriki msimu huu.
Wakati Samatta akifunga mabao mawili, Brandon Thomas yeye amefumania nyavu mara saba.