SHAHIDI ADAI RAIS RAISI NA UJUMBE ALIOFUATANA NAO WAMEPOTEZA MAISHA


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, Ayatullah Khamenei (kushoto) akiamkiana na Shahidi Seyyid Ebrahim Raisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ebrahim Raisi na viongozi kadhaa aliofuatana nao wamekufa shahidi katika ajali ya helikopta iliyotokea katika eneo la Varzghan mkoani Azerbaijan Mashariki wakiwa katika kazi ya kuwahudumia na kuwatumikia wananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limeripoti kuwa helikopta iliyombeba Rais Raisi na ujumbe aliofuatana nao ambao jana Jumapili walielekea Azerbaijan Mashariki kukagua Bwawa la Khoda Afarin na kuzindua miradi kadhaa ya kitaifa na ya mkoa ilipata ajali na kuanguka wakati ikitoka kwenye eneo la bwawa hilo kuelekea Kiwanda cha Usafishaji Mafuta cha Tabriz kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokuwepo katika eneo la Varzghan.

Licha ya kutumwa vikosi kadhaa vya uokoaji vya usaidizi wa haraka ili kutoa huduma kwa Rais na walioandamana nao, juhudi za kuipata helikopta iliyoanguka zilichukua masaa mengi kutokana na hali ya hewa ya ukungu na ugumu wa kupita kwenye eneo la misitu na milima.

Hatimaye, leo asubuhi, makundi ya misaada ya wananchi na ya Shirika la Hilali Nyekundu yaligundua mahali ilipokuwepo helikopta iliyoanguka kwa kutumia ndege zisizo na rubani za uchunguzi za Iran.

“Katika ajali hiyo ya ndege, Rais Seyed Ebrahim Raisi na walioandamana naye, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, Ayatullah Seyed Mohammad Ali Al-Hashem, Imamu wa Ijumaa wa Tabriz, Malik Rahmati, Gavana wa Azerbaijan Mashariki, pamoja na timu ya walinzi wa rais, marubani na wafanyakazi wa ndege ya helikopta wamekufa” shahidi.

Kufuatia ajali hiyo, Baraza la Mawaziri limefanya kikao cha dharura.

Baraza la Mawaziri limeeleza kuwa litalijuilisha taifa la Iran kuhusu wakati na mahali itakapofanyika shughuli ya kuaga mwili wa Rais Raisi aliyekufa shahidi pamoja na miili ya mashahidi wengine walioandamana naye.

Related Posts