SERIKALI imesema kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa jumla ya watumishi 375,904 wamepandishwa vyeo wakiwemo watumishi 85,471 walioathirika na zoezi la uhakiki katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Hayati John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Aidha, imewaagiza waajiri wote kupeleka taarifa za madeni ya watumishi ambao waliathiriwa na uhakiki uliofanyika katika kipindi hicho, ili walipwe stahiki zao.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu (CCM).
Akiuliwa swali hilo kwa niaba ya Jesca, Husna Sekiboko (CCM), alihoji ni lini Serikali itarekebisha madaraja ya watumishi wa umma hasa walimu waliopandishwa na kunyang’anywa vyeo mwaka 2016, 2017 na 2018 ili kupisha uhakiki wa wakati ule.
Pia alihoji ni alihoji ni upi mpango wa serikali kulipa madeni ya walimu waliopandishwa madaraja, pamoja na watumishi wengine wanaodai madeni yao kwa miaka mitano.
Akijibu maswali hayo Kikwete amesema Serikali ilifanya utaratibu wa kuwajulisha waajiri wote kuleta taarifa za watumishi wenye madai ili walipwe.
Amesema katika mwaka huu wafedha wametenga nafasi 52,551 kwenda kulipa madai yote ambao watumishi wanadai ambao tayari wameshahakikiwa.
“Wale ambao hawajaleta madai ya watumishi msisitizo wangu ni kwa waajiri, leteni madeni tunayodaiwa kwa sababu hii ni haki ya mtumishi wa umma kulipwa madai yao. Serikali ipo tayari kulipa madeni yote,” amesema Kikwete.
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 81,503 wakiwemo wale watumishi walioathirika na zoezi la uhakiki.
Amesema mwaka 2016 Serikali ilisitisha mambo mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo upandishaji vyeo ili kupisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi na vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.
“Katika kutatua changamoto zilizojitokeza kutokana na sitisho hilo mwaka 2021/2022 Serikali ilianza kutekeleza zoezi la kuwarejesha watumishi wa umma katika kada mbalimbali kwenye nafasi na vyeo vyao stahiki,” amesema.