Mkenya ashangazwa na kipigo, aipania ligi

Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma amesema ameshangazwa na matokeo waliyopata dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA), akieleza kuwa ni muda mrefu tangu kuruhusu idadi kubwa ya mabao.

Coastal Union ikicheza jana kwenye Uwanja CCM Kirumba jijini hapa ilikumbana na kichapo cha 3-0 dhidi ya Azam kwenye mchezo wa nusu na kutupwa nje ya michuano hiyo.

Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kwa kocha huyo raia wa Kenya tangu alipojiunga na Wagosi hao wa Jiji la Tanga, Novemba, mwaka jana na kumfanya kuvurugwa akili.

Tangu kukabidhiwa timu hiyo, Ouma aliikuta Coastal Union ikiwa na pointi saba, ambapo hadi sasa wapo nafasi ya nne kwa pointi 38 na matarajio yake ni kumaliza ‘Top Four’ Ligi Kuu msimu huu.

Kocha huyo amesema licha kuandaa vyema mipango na mbinu, lakini walizidiwa na wapinzani na kwamba kipigo hicho ni historia kwake kwani ni miaka mingi hajapoteza kwa idadi hiyo ya mabao.

Amesema kuondoshwa kwenye michuano hiyo, inamfanya kujipanga upya kwa ajili ya Ligi Kuu kuhakikisha mechi tatu zilizobaki wanafanya kweli na kufikia malengo.

“Wachezaji walikosa ushapu, wanapopoteza mipira kwa kukosa utulivu, walipata nafasi kadhaa wakashindwa kuzitumia na tumezidiwa na wapinzani,” amesema.

“Sina kumbukumbu ya kupoteza mechi kwa mabao 3-0.  Tulihitaji kufika fainali ya kombe hili ila haijawezekana, hivyo nguvu zote ni kwenye Ligi Kuu.”

Related Posts