By Ngilisho Tv
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiziguzigu, Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma, Marehemu Mwalimu Martin Mpemba amefariki usiku wa April 3 katika Kijiji cha Kibingo Kata ya Kiziguzigu baada ya kushambuliwa na mtu asiyejulikana.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kigoma, Christopher Palangyo akizungumza na viongozi wa chama na waombolezaji mjini Kakonko amesema CCM imesikitishwa na tukio la kifo cha Diwani Mpemba ambaye ameuawa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani wakati akitokea sokoni kurudi nyumbani kwake jana jioni.
Amelitaka Jeshi la polisi kuhakikisha wauaji wanapatikana haraka na kuchukuliwa hatua za kisheria na kwamba mauaji ya namna hiyo hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika hivyo uchunguzi wa haraka ufanywe, ili kuondoa mashaka na wasiwasi ambao umewakumba wananchi baada ya tukio hilo.
Palangyo ambaye amewasilisha salam za pole za Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi kufuatia msiba huo, amesema Chama kinaungana familia, wana-CCM na wananchi wote katika msiba huo.