Serikali yatoa sababu kukatika kwa umeme

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Judith Kapinga amesema changamoto ya kukatika kwa umeme inayojitokeza katika baadhi ya maeneo, inasababishwa na uchakavu wa miundombinu.

Uchakavu huo kwa mujibu wa Kapinga umetokana na miundombinu hiyo kutumika kwa muda mrefu, huku akifafanua Serikali ipo katika hatua ya kuiboresha.

Kapinga ametoa kauli hiyo juzi Jumamosi Mei 18, 2024 alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika ziara ya kutembelea mradi wa Kituo cha kupokea umeme kutoka bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) na kituo cha kupoza umeme cha Chalinze mkoani Pwani.

Katika ziara hiyo, Kapinga amesema baadhi ya maeneo yanakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme, kunakosababishwa na kuchakaa kwa miundombinu yake.

“Tunawahakikishia Watanzania tunaendelea kuboresha miundombinu ili tuondokane na adha ya kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.

Hata hivyo, katika ziara hiyo, amesema tayari ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze umefikia asilimia asilimia 93.7, huku njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze ukifikia asilimia 99.5 na kwamba Juni kinakamilika.

Kwa mujibu wa Kapinga, tayari mitambo miwili inayosafirisha megawati 235 kila mmoja imewashwa na inasafirisha umeme kupitia njia hiyo ya Chalinze, hali iliyomaliza mgawo wa nishati hiyo nchini.

Meneja wa mradi wa Kituo cha Kupokea kutoka JNHPP hadi Chalinze, Newton Mwakifwamba amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza Oktoba mwaka 2021, utakamilika Agosti mwaka huu na sasa umefikia asilimia 93.7.

Ujenzi huo, amesema umeambatana na ule wa miundombinu wezeshi ya kusafirishia na kupoza umeme kutoka katika bwawa hilo, ambayo tayari imeshakamilika na umeme unapita.

“Hadi Aprili 30 mwaka huu Serikali ilishamlipa mkandarasi anayejenga miundombinu wezeshi ili kusafirisha na kupoza umeme unatoka JNHPP, kiasi cha zaidi ya Sh93.6 bilioni,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kilumbe Ng’enda amesema walipotembelea mradi huo Machi mwaka huu, walipata wasiwasi baada ya kukuta utekelezwaji wake ulikuwa kwa asilimia 55.

“Kutoka asilimia 55 tuliyoikuta wakati huo na sasa kituo hiki kipo kwenye asilimia 93.7 hii ni hatua kubwa yapo mambo yameshafikia asilimia 100 ikiwemo chumba cha uangalizi na mambo yanayohusu mazingira yapo kwenye hatua nzuri,” amesema Ngenda.

Hata hivyo, amesema kamati hiyo ilishawahi kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemguru mkoani Arusha, kinachoandaliwa kwa ajili ya kuuza nishati hiyo nchini Kenya.

Related Posts