Kamanda Mallya aagwa, Chongolo amtabiria makubwa

Songwe. “Heshimu kazi, penda watu na siyo vitu”. Hayo ni maneno ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya kwa askari wa Songwe wakati akiagwa rasmi katika mkoa wa Songwe ambako alihudumu pia katika nafasi hiyo kabla ya kuhamishiwa Dodoma.

Machi 14, 2024, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura aliwabadilisha vituo vya kazi makamanda wa polisi nchini ambapo Mallya alihamishiwa mkoa wa Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Augustino Senga, aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar.

Hafla hiyo ambayo ilifanyika usiku wa kuamkia leo Mei 20, 2024 mkoani hapa iliambatana na kumkaribisha kamanda mpya, Senga na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, watumishi idara mbalimbali zikiwapo taasisi na kampuni binafsi.

Akizungumza huku akilengwa na machozi ya furaha kwa umati uliojitokeza na zawadi mbalimbali, Kamanda Mallya amesema ujumbe kwa watumishi haswa askari ni kuthamini kazi na kupenda watu na siyo vitu.

Pia, amemshauri kamanda mpya, Senga, kupambana na uhalifu kwa watoto na mmomonyoko wa maadili kwa vijana akisema ni janga ambalo limeshika kasi na kwamba lazima watoto walindwe.

“Mzazi fuatilia mtoto wako kila mara kwani hali siyo nzuri na nimuombe Kamanda Senga kushirikiana na wananchi hawa ili kuhakikisha Songwe inaendelea kuwa imara,” amesema na kuongeza:

“Tunashirikiana na kamati ya usalama, viongozi wa dini ambao wao wanakemea uovu, sisi tunakemea uhalifu, hivyo tunashambulia kwa pamoja ili Taifa kuwa salama. Askari tunayo kaulimbiu yetu ya nidhamu, haki uweledi na uadilifu,” amesema kamanda huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amesema kwa kazi aliyoifanya kwa sasa wanaendelea kushawishi kuanzishwa Kamisheni ya Malezi katika Jeshi la Polisi na anayefaa katika nafasi hiyo ni kamanda huyo.

“Wewe umebeba jukumu hili sana na Mungu akujaalie, tunahitaji kuanzishwa kwa Kamisheni ya Malezi katika Jeshi la Polisi na zikipigwa kura ni wazi inajulikana wapi zitaenda,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Chongolo ameongeza kuwa: “Tunapoenda uhalifu utakuwa wa tabia zaidi kuliko wa vitendo, hivyo lazima tuwahi kabla haijaleta madhara, tayari tumewasilisha hii hoja.”

Hata hivyo, katika pongezi hizo, Chongolo kwa niaba ya ofisi yake, amekabidhi zawadi ya ng’ombe mmoja, kuku watatu na kitenge kumuaga kamanda huyo akieleza kuwa ni njia bora ya kumuandaa kustaafu.

“Sisi wote ni wastaafu watarajiwa, hivyo katika kukuandaa vema, tumekununulia ng’ombe wa maziwa, kuku wa mayai na kitenge kwa ajili ya mtoko,” amesema katibu mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Naye Kamanda Senga amesema atahakikisha anaendeleza yale mazuri aliyoyafanya mtangulizi wake katika kuifanya Songwe kuwa imara huku akiomba ushirikiano kwa wananchi.

“Kama ambavyo alifanya mtangulizi wangu, nitapita mlemle kuhakikisha Songwe inaendelea kuwa imara, wananchi naomba ushirikiano kama mlivyofanya kwa Kamanda Theopista,” amesema kamanda huyo.

Akizungumza kwa niaba ya askari polisi mkoani humo, Ofisa Usalama Barabarani mkoa wa Songwe (RTO), Joseph Bukombe amesema pamoja na zawadi walizotoa lakini wanakabidhi hundi ya Sh 2 milioni kwa ajili ya kumuaga Kamanda Mallya na Sh 1 milioni kumkaribisha kamanda mpya.

Related Posts