Dodoma. Katika zama za sasa za maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano, matumizi ya mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya watu, wanasiasa wakiwamo.
WhatsApp, kama moja ya mitandao hiyo, imekuwa jukwaa la mawasiliano ya karibu, mijadala ya kisiasa na hata kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo, licha ya faida hizo, wanasiasa wamejikuta katika changamoto kadhaa ndani ya makundi haya sogozi ya kijamii hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais wa Oktoba 2025.
Ni katika makundi hayo wanasiasa wanapitia mashambulizi ya kihisia na matusi kwa kukosekana udhibiti wa maudhui, jambo ambalo huwapa baadhi ya wana-kundi uhuru wa kutoa lugha za matusi, kejeli na dhihaka.
Ni katika makundi hayo baadhi hujikuta wakivamiwa kwa maneno makali, hata wakati mwingine kwa hoja zisizo za msingi, hali inayoweza kudhoofisha hali yao ya kiakili na kuwavunja moyo.
Adha nyingine ni upotoshaji wa taarifa. Kumekuwa kukisambazwa taarifa pasipo kuthibitishwa, hivyo wanasiasa huathiriwa na habari za uongo, uzushi au propaganda zinazolenga kuchafua majina yao au kudhoofisha nafasi zao kisiasa.
Hali hii si tu huleta mkanganyiko kwa umma, bali pia huathiri taswira ya wanasiasa mbele ya wapigakura.
Katika makundi haya, wanasiasa hukabiliwa na shinikizo kubwa la kutatua matatizo ya kijamii mara moja. Wakati mwingine madai ya haraka na malalamiko ya mara kwa mara hutolewa bila kuelewa mipaka ya mamlaka au vipaumbele vya utekelezaji wa sera, jambo ambalo huwalemea wanasiasa kiakili na kisaikolojia.
Wanasiasa pia hukosa faragha na uhuru wa kujieleza, kwani mara nyingi kila kauli yake hupokewa kwa uchunguzi mkubwa na baadhi ya watu katika makundi huchukua maneno nje ya muktadha kwa makusudi ya kisiasa.
Hali hii huwafanya kuwa waoga wa kujieleza kwa uwazi au kushiriki kikamilifu kwa kuhofia kupotoshwa au kushambuliwa baadaye.
Katika makundi haya, pia hukabiliwa na migongano ya kisiasa kwa wale walio vyama tofauti. Hii huibua mijadala mikali ya kisiasa inayoweza kugeuka kuwa vita vya maneno au hata uhasama wa muda mrefu.
Wapo pia ambao hujikuta wakitengwa kwa kuondolewa makusudi kwenye makundi au kudhalilishwa hadharani ili kuwapunguzia heshima mbele ya jamii. Matendo haya huambatana na uanaharakati wa kisiasa au chuki binafsi, hali ambayo huathiri morali ya kisiasa na kujitolea kwao kwa jamii.
Akizungumzia makundi hayo, mwanasiasa mkongwe nchini na mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya anasema yamekuwa hatari zaidi kwa wanasiasa, hasa yanapotumika na kusimamiwa na wenye lengo la kutia nia kugombea uongozi.
Sakaya anasema makundi hayo kwa sehemu kubwa yanatumika kuwachafua wanasiasa na kupandikiza chuki ili wachukiwe na wapigakura kutokana na kukosa udhibiti.
“Mtu anaibuka anaanza kukushambulia kwenye ma-group ya WhatsApp hata kama hakufahamu vizuri, anazusha uongo kuwa wewe ni mtu mbaya, husaidii wananchi, unatumia ubunge kujinufaisha na wakati si kweli, sasa haya maneno yakisambaa unaanza kuonekana huna maana kwa wale waliokuchagua,” anasema.
Sakaya, mbunge wa zamani wa Kaliua anasema makundi hayo ni hatari zaidi kwa wanasiasa wanawake ambao huanikwa taarifa zao binafsi zinazohusu ndoa na uhusiano kwa kuwekwa picha za waume wao au watoto wao pasipo ridhaa zao.
“Nikiwa mbunge niliambiwa natembea na mwenyekiti wangu wa chama, taarifa ambazo siyo za kweli. Hata mume wangu aliponiuliza nilimwambia taarifa hizo siyo za kweli, bali ni uzushi tu wa kwenye mtandao akanielewa. Uzushi huu ndiyo unaosababisha wanasiasa wengi wanawake kuachika kwenye ndoa zao,” anasema Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara).
Anasema maumivu zaidi huwapata walio madarakani hasa nyakati za kuelekea uchaguzi, kila mmoja hutumia kila njia ili kufikia malengo ya kisiasa.
Hata hivyo, Sakaya anasema hakuna ubaya kama makundi hayo yangekuwa yanatumika vema, kwani yangekuwa na faida kutokana na kurahisisha mawasiliano kwa watu wengi.
Anasema miongoni mwa faida za makundi sogozi ni kutoa na kupokea taarifa sahihi, huku baadhi ya watu wakisaidiwa matibabu, masomo, ada za shule na hata wengine kupata kazi baada ya kueleza changamoto walizonazo na wabunge wao kuzifanyia kazi.
Sakaya anasema kupitia makundi hayo amekuwa akisambaza video na picha kuhusu shughuli zake bungeni na kwenye mikutano ya hadhara, hivyo kupata umaarufu alionao baada ya kuonekana.
Kutokana na hilo, anasisitiza mitandao na makundi sogozi vitumike kwa tija, badala ya kuchafuana.
Aliyekuwa mtia nia ya ubunge Moshi Mjini mwaka 2020, Samweli Tesha anasema makundi sogozi kwa sehemu kubwa yanatumika kuwaumiza wanasiasa badala ya kuwajenga.
Anasema asilimia kubwa ya wapigakura hawapo kwenye makundi hayo yanayoundwa na baadhi ya watu ambao wengi wao hawakai kwenye jimbo husika kwa ajili ya kujadili maendeleo ya jimbo, lakini wamekuwa na utaratibu kutembelea kwa mwaka mara moja.
Tesha anasema mfumo wa kutumia makundi sogozi wakidhani wanajadili maendeleo umesababisha wengi kupata wawakilishi ambao hawana uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Anashauri wanasiasa kwenda moja kwa moja kwa wananchi waliowachagua ili kuwasikiliza na kutatua kero zao badala ya kusubiri kero zinazotumwa kwenye makundi sogozi ambazo nyingi hazina uhalisia.
“Kama mwanasiasa atategemea makundi hayo kutatua kero za wananchi atajichelewesha na hapo anasubiri kushughulikiwa kisiasa, badala yake aende mwenyewe kwa wananchi,” anasema.
Aliyekuwa mgombea ubunge Musoma Mjini mwaka 2020, Julius Mwita (Chadema) amesema makundi hayo ni muhimu kwa sababu yanarahisisha mawasiliano na taarifa zinakwenda haraka katika jamii.
“Lakini makundi haya yamekuwa mwiba mkali kwa wanasiasa kwa muda wote, kutokana na kila mtu kuwa na tafsiri yake. Mnapokuwa kwenye kundi mnajadili jambo fulani, anajitokeza mtu na tafsiri yake ambayo haipo na kuamua kile mlichokuwa mnakizungumza hata kwa nia njema anakibadilisha na kukipeleka kwingine kama umbea.
“Mfano ni juzi kwenye kundi letu la G55 tulikuwa tunajadili hoja zetu na msimamo kupeleka kwenye kikao cha watia nia si kwa lengo baya, lakini mmoja akayachukua na kuyatoa ili kuonekana mwema zaidi na sisi tulionekana wasaliti na tunataka kuasi chama,” amesema Mwita.
Mchambuzi wa siasa, Dk Faraja Kristomus amesema faida ya makundi sogozi ni kuwaunganishia wanasiasa pamoja ili kujadiliana na kuweka mikakati kwa pamoja, kuhimizana na kusaidiana katika kuandaa hoja za kwenda kuongea kwa wananchi au wapigakura.
Pia, kuwasilisha hoja na maswali kwa viongozi wao na kupewa majibu kwa pamoja, kuwapa ushauri viongozi wao inapotokea kuna masuala wanaona hayako sawa. Kusambaza ujumbe wa kampeni kupitia majukwaa mbalimbali na kuwafikia watu wengi zaidi.
Hata hivyo, Dk Kristomus amesema makundi hayo yana hasara pia ikiwemo majadiliano yao kuvuja nje ya makundi yao, hivyo kutokuwa njia salama ya kuweka mikakati na kujadiliana masuala nyeti.
Amesema kutokana na kuongezeka kwa wigo wa matumizi ya teknolojia na habari, kuna uwezekano mkubwa wa taarifa hizo kupotoshwa na kugeuzwa kutumika vibaya dhidi ya baadhi ya wanasiasa.
“Kwenye hayo makundi kunaweza kukawepo na watu wasaliti ambao watakuwa wanachukua mipango inayojadiliwa na kuipeleka upande mwingine, hivyo kuvujisha mikakati hiyo na wapinzani wao kupanga mipango ya kudhibiti kabla ya kufikia utekelezaji,” amesema na kuongeza:
“Baadhi ya wanasiasa kuchukua majina ya wachangiaji wa hoja na kuwahujumu wao binafsi badala ya kushughulikia hoja husika. Ndiyo maana utasikia kwenye mitandao ya kijamii ikielezwa kuwa fulani anamchukia mwanasiasa fulani au mwanasiasa fulani anapendekeza fulani afanyiwe hivi na vile,” amesema.
Mchambuzi wa siasa, Mussa Yusuph amesema makundi sogozi yana faida na hasara zake kwa wabunge na viongozi wengine wa kuchaguliwa lakini kwa wakati huu yamekuwa mwiba na sindano ya kuwachoma waliopo madarakani.
Mussa anasema faida ya makundi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ni ndogo ukilinganisha na hasara ambazo wanapata wanasiasa kwenye maeneo yao.
“Ukweli makundi yana faida kwa kuwafikia watu mara moja na kusikiliza kero za watu, lakini kwa wakati huu ni shubiri kwa wanasiasa wakiwamo wabunge na madiwani ambao wanaishi kama watu wanaowindana,” anasema.
Anasema baadhi ya makundi ambayo yalikuwa na msaada kwa wananchi kwa wakati huu yamekuwa yakitumika vibaya kuwachafua viongozi na kuwaaminisha watu kuwa mhusika hafai kuchaguliwa wakati inakuwa ni mizengwe.
“Unakuta wananchi wanatoa kero na changamoto zao kwenye kundi ambalo mbunge yupo, lakini hachangii chochote hivyo anasababisha hasira kwa wananchi, sasa yeye badala ya kujiongeza anaamua kujiondoa kwenye kundi kwa kudhani wanamkomoa kumbe anazidi kujiharibia, hapo ndipo wanaanza kumshughulikia,” amesema.