Ajira walioishia darasa la saba zaondolewa JWTZ

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeaondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba kwenye Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Mei 20,2024 na Naibu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godfrey Pinda kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.

Cherehani amehoji kuna mpango gani wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne. 

Akijibu swali hilo, Pinda amesema JWTZ huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara.

Amesema utaratibu wa kuandikisha jeshi askari wapya umefafanuliwa kwenye kanuni ya 5 ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala).

“Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba,” amesema.

Kuhusu kuongeza idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne, Pinda amesema hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika.

Amesema Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa kibajeti.

Amesema nafasi hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi.

Katika maswali ya nyongeza Cherehani, amesema hakuna uwiano ya vijana wanaoingia katika mafunzo na wale wanaoajiriwa na kuhoji ni nini mkakati wa muda mfupi na muda mrefu wa vijana hao kuajiriwa.

Amesema pia vijana hao wanapokuwa katika mafunzo kumekuwa na changamoto ya miundombinu na kuhoji nini mkakati wa Serikali kukabiliana na tatizo la miundombinu.

Akijibu maswali hayo, Pinda amesema suala la ajira inategemeana na nafasi zinazotolewa na Serikali.

Kuhusu miundombinu, Pinda amesema Serikali imekuwa ikiviangalia vyombo vya ulinzi na usalama kwa upekee kabisa na hivyo hakuna uhakika wa ukosefu wa vifaa na miundombinu ya kimafunzo katika kambi za jeshi.

“Serikali imeweka miundombinu wezeshi kwa vijana wetu ili waweze kupata mafunzo wezeshi yatakayoweza kwenda kuwasaidia kumaliza mafunzo yao,”amesema.

Related Posts